Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akizungumza na wafanyakazi wa mzani wa Makambako, wakati alipotembelea mzani huo kufahamu changamoto wanazozipata katika utendaji wao wa kazi, Mkoani Njombe.
Muonekano wa mzani wa Makambako, mkoani Njombe, wenye uwezo wa kudhibiti uzito wa magari makubwa yanayozidi 3500kg (tani 3.50).
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, ameuagiza uongozi Wakala wa Barabara (TANROADS), Makao makuu kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja wanaweka mzani mwingine wa kuhamishika katika eneo la mzani wa Makambako ili kuweza kutatua changamoto ya msongamano wa magari katika eneo hilo.
Naibu Waziri huyo ametoa agizo hilo mkoani Njombe, mara baada ya kufika katika mzani huo ambapo amejionea changamoto zake na kusisitiza kuwa, kuongeza mzani wa kuhamishika katika eneo hilo kutasaidia kupunguza kero hiyo ya msongammano wakati Serikali ikitafuta ufumbuzi wa kudumu wa kujenga mzani mwengine katika eneo hilo.
"Naagiza TANROADS Makao makuu mfanye kila linalowezekana ndani ya mwezi mmoja mlete mzani wa kuhamishika hapa Makambako, tunataka tutoe huduma ya haraka kwa madereva ili pasiwe na msongamano katika eneo hili", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Amewaonya wale madereva wote wanaotumia kisingizio cha uwepo wa foleni katika mzani huo kwa kufanya mambo yao binafsi kuacha mara moja tabia hiyo, kwani ikibainika kwa dereva yeyote ambae ameshapatiwa huduma lakini bado ameegesha gari lake katika eneo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria dhidi yake.
Ameagiza Taasisi zote zinazotoa huduma katika mzani huo kushirikiana na kuandaa maoni yao kuhusu namna ya kupunguza msongamano katika mzani huo na kuyawasilisha Wizarani ili yaweze kufanyiwa kazi.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Njombe, Mhandisi, Yusuph Mazana, ametaja baadhi ya changamoto zilizopo katika Mzani huo kuwa ni kuharibika kwa mzani mara kwa mara kutokana na mzani huo kuwa ni wa siku nyingi na kuwepo na muingiliano wa huduma kutoka Taasisi mbalimbali za serikali kama Uhamiaji, Polisi na TRA.
Ameongeza kuwa changamoto nyingine ni baadhi ya magari kuegeshwa nje ya maeneo ya mzani baada ya kupima na hivyo kusababisha msongamano wa magari yanayotakiwa kuingia ndani ya eneo la mzani kwa ajili ya kupata huduma ya upimaji au kufanya taratibu nyingine.
Naibu Waziri Kwandikwa amemaliza ziara ya kikazi katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ambapo alipata fursa ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Sekta yake.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment