TANGAZO


Thursday, May 12, 2016

ZIJUE FADHILA ZA MWEZI WA SHAABAN

Msikiti Mtakatifu wa Makka
Leo ni tarehe 12 Mei 2016 sawa na tarehe 4 Shaaban 1437H
KUKIWA kumesalia siku chache ili tuingie katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, inatupasa tuangalie kwa ufupi mwezi huu tulionao wa Shaabani

Mwezi wa Shaaban ni mwezi wa nane katika miezi ya kiislamu. Mwezi huu upo kati ya Rajab na Ramadhan. Rajab. Ni mwezi ambao Muislamu anatakiwa ajihimu katika kufanya ibada. Pia ni mwezi ambao mja autumie katika kujiandaa zaidi na Ramadhani ili asiweze kupoteza fursa ya 
Ramadhani ikiwa Allah atamjaalia kufika. 

Miongoni mwa  mambo ambayo yamependekezwa sana mja ayafanye ndani ya mwezi wa Shaaban ni kufunga.

Katika mambo ambayo yanaufanya mwezi huu kuwa ubora ni pamoja na funga(swaumu) ndani ya Shaaban. Licha ya funga ndani ya Mwezi huu, kufunga ni jambo muhimu sana kwa mwanadamu, Imepokewa na Abi said Al Khudri (RA), “Amesema Mtume wa Allah "Hakuna mtu yoyote anayefunga siku yeyote katika njia ya Mwenyezi Mungu Mtukufu isipokuwa Mwenyezi Mungu huuweka mbali uso wake na moto kwa siku hiyo aliyofunga miaka sabiini 

".(Bukhari na Muslim). Pia imepokewa na Amri Ibn Abass (RA), Amesema Mtume Muhammad "Mwenye kufunga siku yeyote katika njia ya Allah moto huwa mbali naye kwa mwendo wa miaka mia moja”.(Attbraniy)

Utagundua sasa uzito wa mja kufunga siku moja tu kwa ajili ya Allah Mwenyezimungu. Hivyo ndugu yangu Muislamu usiwe mzito kwa kusema hizi funga za sunna tu. Kimbilia funga za sunna ili uweze kupata kheri kama hizo. Na zifunge saumu zako kwa kutaraji malipo kutoka kwa Allah (subhanahu wata‘ala).

Pia tunaona kuna umuhimu wa kufunga nadani ya mwezi huu kama alivyopokea Bibi Aysha (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: “Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) alikuwa akifunga hadi tukadhani kuwa hatofungua kamwe, na alikuwa akiacha kufunga hadi tukadhani hatofunga tena. Sijamuona Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) kufunga mwezi mzima kama alivyokuwa akifunga Ramadhaan, na sijamuona akifunga mara nyingi kama alivyofunga katika Shaabaan” (Bukhaariy na Muslim)

Hii ilikuwa ni tabia ya Mtume Muhammad ya kukikithirisha zaidi kufunga ndani ya mwezi wa Shaaban kuliko miezi mengine yoyote ukitoa mwezi wa Ramadhan. Na katika hili Mtume Muhammad mwenyewe alieleza ni kwa nini hufunga zaidi ndani ya mwezi wa Shaaban. 

Anasimulia Usama Ibn Zaid (RA): Nilisema ewe Mjumbe wa Allah sikukuona ukifunga katika mwezi wowote katika miezi kama siku unazofunga katika mwezi wa Shaaban? 

Akasema Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) Huo ni mwezi ambao watu wameghaflika nao baina ya Rajab na Ramadhan nao ni mwezi ambao (hurufaishwa) hupandishwa ndani yake amali za watu kwa Bwana wa Viumbe na napenda zipandishwe amali zangu na hali ni mwenye kufunga.” (An-nasai). 

Huyu ni kipenzi cha Allah ambae amesamehewa dhambi zake zilizopita na zinazokuja ila alikuwa akijihimu kwa kufunga ili a’amali zake zipelekwe kwa Allah hali ya kuwa amefunga. Je vipi mimi na wewe ambao daima ni wenye kumkosea Allah? Kwa nini na sisi tusijikurubishe kwa Allah kwa kufunga sana ndani ya mwezi wa Shaaban? Isitupite fursa hiyo na tujihimize katika suala zima la kufunga sisi wenyewe pamoja na watu wetu.
Pamoja na ubora na kufunga siku nyingi ndani ya mwezi huu, haitakiwi kufunga mwezi mzima yaani siku thelathini au ishirini tisa. 

Katika kauli yenye nguvu zaidi wanazuoni wanasema kuwa Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) hakuwahi kufunga mwezi wowote kamili ambao ni sunna kufunga. Na hili  linatokana na ushahidi kuwa  imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas (RA ) amesema "‘‘Mtume Muhammad hakuwahi kufunga mwezi wowote kikamilifu isipokuwa Ramadhan." (Bukhaariy).

Vile vile Imekatazwa kufunga katika mwisho wa Shaban kwa nia ya kutozikosa siku za mwanzo wa Ramadhani. Na hili linathbitishwa kuwa imeripotiwa kutoka kwa Abu Hurayrah (RA) kuwa Mtume Muhammad amesema: “Kufunga katika mwisho wa Shaaban kumekatazwa ili kuweka tofauti kati ya Swawm za Sunnah (shaabani) na Swawm za faradhi (ramadhani).”

Kadhalika Mtume Muhammad amesema : “Asiitangulie mmoja wenu Ramadhani kwa saumu ya siku moja au mbili isipokuwa akiwa mtu alikuwa akifunga saumu yake basi na aifunge siku hiyo” (Bukhari na Muslim). 

Hii haimuhusu yule mwenye kuzoea kufunga siku za jumatatu na alhamisi au siku tatu za kila mwezi au saumu ya Nabii Daud, ikawafiki saumu yake siku hiyo basi na afunge kama kawaida yake kwa sababu makatazo hayamuelekei yeye, kinyume cha mwenye kuanzia kufunga hali ya kuwa si wajibu kwake na wala hatakiwi kulipa wala si ada kwake, haitakiwi kwake kufunga. 

Pia Yaumu Shakka kumekatazwa mtu kufunga. Yawmu Shakk (siku yenye shaka) ni ile siku ambayo watu hawana uhakika juu ya kuanza kwa Ramadhan, kwa sababu ya hali ya mawingu kufunga na mwezi kutoonekana au sababu nyinginezo. 

Kama alivyosimulia Swila Ibn Zufar anasema “Tulikuwa kwa Ammar Ibn Yaser akaletewa mbuzi wa kuchoma akasema" Kuleni " akakaa mbali mmoja katika watu akasema “Hakika mimi ni mwenye kufunga” akasema Ammar “mwenye kufunga siku ambayo watu huitilia shaka basi amemuasi Abal Qassim (swalla Allahu alayhi wasallam). (Bukhari).
  
pamoja na fadhila za funga Muislamu anatakiwa ajihimu katika kufanya mambo mengine mbali mbali ya kheri kama kuswali swala za sunna, kuleta istighfaar na adhkaaar nyenginezo kwa wingi, kutoa sadaka kwa wingi na kheri nyengine. Haya yote mwenye kuyafanya yatamuandaa katika kuitumia Ramadhani yake vile ipasavyo na atalipwa malipo makubwa.

Mwisho nawasihi wote wenye madeni ya swaumu za ramadhani, basi wasiwache kulipa madeni yao. Kwani hairuhusiwi mtu kuchelewesha kulipa deni la Ramadhani hadi ikaingia Ramadhani nyengine. Na mtu anaweza kuzilipa funga hizo ndani ya Shaaban kwa ushahidi kutoka kwa Mama wa Waumini Aysha (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema : “Ilikuwa ninazo siku za kulipa za Ramadhaan na sikuweza kuzilipa isipokuwa (katika mwezi wa) Shaaban.” Al-Bukhaariy. 

Yeyote aliyekuwa na uwezo wa kulipa Swawm zilizompita kabla ya Ramadhaan (ya pili) kuingia na asifanye hivyo, basi atalazimika kuzilipa baada ya Ramadhaan (ya pili), pia analazimika kutubia na kumlisha maskini mmoja kwa kila siku iliyompita.(Imam Maalik, Ash-Shafi’iy na Ahmad).
SHEIKH SWED TWAIBU SWED, MWENYEKITI MTENDAJI (TCDO)

No comments:

Post a Comment