TANGAZO


Thursday, April 27, 2017

RC NCHIMBI AZIAGIZA HALMASHAURI ZA SINGIDA KUANZISHA MABWAWA YA UFUGAJI WA SAMAKI

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (wa pili kulia) akishiriki kuvua samaki aina ya kambare kwenye bwawa lililopo kwenye shamba la samaki la Mikumbi mjini hapa ikiwa ni sehemu ya uzinduzi uvuvi kwenye shamba hilo.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (wa kwanza kulia) akitoa maelekezo kwa mmiliki wa shamba la ufugaji samaki la Mikumbi Bw. Charles Kidua (wa pili kulia) wakati akikagua shamba hilo lenye mabwawa sita yaliyofungwa samaki aina ya sato na kambare.  
Mmiliki wa shamba la samaki Mikumbi mjini Singida na afisa maliasili Mkoa wa Singida Charles Kidua (aliyenyoosha mkono) akimweleza jambo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (wa kwanza kulia) muda mfupi kabla ya kuzinduliwa kwa uvuvi kwenye shamba hilo asubuhi ya leo.
Baadhi ya samaki aina ya kambare waliovuliwa mapema leo kwenye uzinduzi wa uvuvi shamba la samaki la Mikumbi lililopo mjini hapa. 

MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ameziagiza halmshauri zote za Mkoa wa Singida kuanzisha mabwawa ya ufugaji wa samaki ili kutunza mazingira, kuongeza kipato na kuwa darasa la kufundishia vikundi na wananchi wengine.

Dkt. Nchimbi ametoa agizo hilo mapema asubuhi ya leo katika shamba ya ufugaji wa samaki la Mikumbi lililopo manispaa ya Singida linalomilikiwa na Bwana Charles Kidua wakati wa uzinduzi wa mavuno ya kwanza ya samaki aina ya kambare katika mabwawa matatu kati ya sita yaliyopo katika shamba hilo.

Amesema halmashauri zionyeshe mfano kwa kuiga mbinu ya ufugaji wa samaki katika kutunza mazingira kwakuwa itaongeza kipato cha halmashauri pia halmashauri iangalie namna ya kufundisha ufugaji wa samaki vikundi vya vijana kuliko kuwapa mikopo ya pesa ambayo huishia kutumika vibaya.

Dkt. Nchimbi ameongeza kuwa uwepo wa mabwawa hayo ya ufugaji wa samaki unaonyesha kuwa Mkoa wa Singida sio kame na wala sio mkoa masikini na uko tayari kuandaa chakula kulisha mikoa ya jirani hasa makao makuu ya nchi ambayo ni Dodoma.

“Tumejipanga na tuko vizuri kuhakikisha Dodoma inapata chakula kizuri na cha uhakika, Singida sio kame wala masikini, samaki hawafugwi kwenye ukame, Singida sio kame hata kidogo” amesisitiza Dkt. Nchimbi.

Ameongeza kuwa watendaji wote wanapaswa kuziishi taaluma zao kama ambavyo mmiliki wa mabwawa hayo ambaye ni afisa maliasili ambaye ameweza kuanzisha bwawa la samaki na hivyo kuwataka watendaji wengine mfano maafisa kilimo, mifugo kuwa mifano kwa jamii kwa kuonyesha manufaa ya taaluma hizo.

Naye mmiliki wa mabwawa hayo Bw. Charles Kidua amesema amekuwa na wazo la kuanzisha mabwawa ya ufugaji wa samaki kwa muda mrefu lakini amefanikiwa kuanzisha mradi huo mwaka 2016 kwa gharama ya shilingi milioni 12.

Kidua amesema kuanzishwa kwa mabwawa hayo kumewafaidisha baadhi ya wananchi amabo tayari wamejifunza kutka kwake na kuchukua vifaranga vya samaki kwake.

“Ukiwa na eneo zuri lenye maji uanzishaji wa ufugaji wa samaki kwa bwawa moja unaweza kukugharimu shilingi laki tatu tu, jirani yangu hapa yeye ameanzisha bwawa lake na kuchukua vifaranga hapa kwangu, kuna wananchi wengine pia wameanzisha mabwawa yao kupitia elimu wanayojifunza kutoka hapa” amesema Kidua.

Ameongeza kuwa changamoto aliyokumbana nayo katika kuanzisha mradi huo ni pamoja na ukosefu wa vifaranga wa samaki katika mikoa jirani na hivyo kumlazimu kuvifuata Mwanza hali ambayo inaongeza gharama.

Baadhi ya maofisa wa serikali na wananchi walioshuhudia uvunaji wa samaki hao wamekiri kuhamasika na wao kuanzisha ufugaji wa samaki. Mavuno ya samaki aina ya kambare katika shamba hilo yatafuatiwa na uvunaji wa samaki wengine aina ya sato ambao pia wapo katika mabwawa ya shamba hilohilo.

TAARIFA: RAIS DKT. MAGUFULI KUPOKEA TAARIFA YA ZOEZI LA UHAKIKI WA VYETI KWA WATUMISHI WA UMMA


WAZIRI UMMY ASISITIZA WANAFUNZI WANAOPATA UJAUZITO WAENDELEE NA MASOMO

Mkuu wa Chuo cha DUCE Profesa William Anangisye akihutubia jopo la Wadau na wanafunzi katika mkutano wa masuala ya Usawa na huku akisisitiza wazazi na walezi kuwatia moyo wanafunzi wa kike kupenda  masomo ya sayansi ili kupata  wanasayansi wanawake nchini. 
Profesa Rwekaza Mukandala Makamu Mkuu wa Chuo kikuu cha Dar Es Salaam akihutubia wadau na wanafunzi  waliojitokeza katika mkutano wa kwanza wa masuala ya Jinsia na Usawa yaliyofanyika katika chuo kikuu cha Uwalimu DUCE jijini Dar Es Salaam. 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na watoto Mh. Ummy Mwalimu akimuwakilisha Makamu wa Raisi Bi Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa  mkutano wa kwanza wa Masuala ya Usawa wakijinsia  ulioandiliwa na Chuo Cha Ualimu (DUCE) jijini Dar Es salaam. 
Wadau wa Masuala ya Usawa wa kijinsia wakifuatilia kwa ukaribu ujumbe uliokuwa ukitolewa na Mh.Ummy Mwalimu Waziri wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na watoto aliyekuwa akimuwakilisha Makamu wa Raisi Bi Samia Suluhu Hassan katika viunga vya Chuo cha Uwalimu DUCE jijini Dar Es Salaam. 
Picha ya pamoja ya wadau wa masuala ya Usawa wakijinsia katika mkutano wa kwanza wa masuala ya Usawa wakijinsia uliowakutanisha kujadili na kuhamasisha  juu ya kumlinda mtoto wa kike ili apate Elimu sawa kama ile apatayo mtoto wakiume katika jamii yetu.

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesisitiza kuwa wanafunzi wa kike wanaopata mimba wakiwa mashuleni waendelee na masomo yao ili kufikia malengo walioyanayo nchini.

Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa maswala ya kijinsia ulioandiliwa na Chuo Cha Ualimu (DUCE) alipomuwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri8 ya Muungano waq Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo jijini Dar es salaam.

“Tunapokataza watoto wa kike wasiendelee na masomo pindi wanapopata ujauzito wakiwa mashuleni  tunawaadhibu watoto wa masikini washindwe kutimiza malengo yao kwa wakati waliotarajia”alisema Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy amesema kuwa anaunga mkono uamuzi wa  Rais wa Tanzania Dkt. Jonh Pombe  Magufuli kwa  kutoa elimu bure nchini kwani kunaongeza idadi ya watoto wa kike  kuwepo mashuleni tofauti na kipindi cha nyuma.

Mbali na hayo Waziri Ummy ametoa wito kwa wazazi kuwahamasisha watoto wao wa kike kupenda masomo ya sayansi ili kukuza rasilimali watu katika kujenga uchumi unaotokana na viwanda nchini.


Kwa upande wa Mkuu wa Chuo cha DUCE Prof. William Anangisye amesema kuwa lengo la  mkutano huo ni kuleta chachu ya kuwatia moyo wanafunzi wa kike kupenda  masomo ya sayansi ili kupata  wanasayansi wanawake nchini.

KITETE WAPATA JENGO LA WANAOSUBIRI KUONA WAGONJWA

Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Dkt. Thea Ntara

Tiganya Vincent, RS-Tabora
27.4.2017
WANANCHI wa Mkoa wa Tabora wanakwenda kuona wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete wameondokana na adha ya muda mrefu ya kunyeshewa mvua na kukaa juani baada ya kukamilika na kuzinduliwa kwa Jengo la Mahali pa Kungonjea kuona wagonjwa.
 
Jengo hilo lililojengwa na Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Tabora na umegharimu shilingi milioni 18 hadi kukamilika.

Uzinduzi huo umefanywa leo na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora Queen Mlozi wakati wa sherehe fupi zilzofanyika katika Hospiali ya Rufaa ya Mkoa huo Kitete.

Alisema kuwa kukamilika  kwa jengo hilo kwa muda kumesaidia kuondoa kilio cha muda mrefu cha viongozi na wananchi cha kutaka lijengwe eneo la watu kupumuzika wakati wakisubiri muda wa kuona wagonjwa wao wanapata matibabu katika Hosptali hiyo.

Kaimu Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora aliipongeza Seketarieti ya Mkoa wa Tabora kwa kuwa wabuni hadi kufanikisha ujenzi huo kwa kiwango cha juu na gharama nafuu.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Dkt. Thea Ntara alisema kuwa ujenzi wa jengo hilo umefanywa kwa kutumia fedha za usimamizi wa miradi ambapo Seketarieti ya Mkoa huo imepunguza katika fedha zake za kufuatilia miradi.

Alisema kuwa hatua hiyo imesaidia kupatikana kwa fedha hizo zilizosaidia kukamilisha kwa jengo ambalo ambalo litasiadia kuepusha wananchi hao na hatari za kugongwa na baiskeli au pikipiki kutokana na kukaa kando kando ya barabara.

Katibu Tawala huyo wa Mkoa aliongeza kuwa kabla ya ujenzi huo walitaka kumtumia Mhandisi kutoka nje ambapo alidai apatiwe shilingi milioni 35 ili afanikishe ujenzi huo , lakini walipoamua kutumia mwandishi wa ndani wameokoa kiasi cha milioni 17.

Aidha , Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Tabora ametoa wito kwa Wakurugenzi wote Watendaji wa Halmashauri nane(8) za mkoani Tabora kuhakikisha wanajenga jengo kwa kila Hospitali la Mahali pa wananchi kuongejea kuona wagonjwa wao.

Alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuwaondelea kero wananchi na kutekeleza ahadi ya Serikali ya awamu ya tano ya kuwajali wanyonge.

Aidha, Dkt. Ntara aliwaahidi wananchi kuwa baada ya kukamilika kwa jengo hilo atajitadi kuwanunulia runinga ili wanapokuwa wanasubiri kuona wagonjwa wafutilie taarifa mbalimbali za habari zinaendelea za ndani na nje ya nchi.

Katika hatua nyingine Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Tabora wanatarajia kujenga Kliniki mbili katika eneo la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete kwa ajili ya vijana na wakinamama.

Alisema kuwa lengo la kutaka kufanya hivyo ni kutaka kutoa elimu kwa vijana hasa mabinti kwa ajili ya kupunguza ndoa na mimba za utotoni mkoani Tabora.

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete ilijengwa katika miaka ya 1909 lakini ilikuwa haina sehemu ya watu kukaa wakati wakisiburi kuona wagonjwa.

BUNGENI LEO: WAAJIRI TEKELEZENI SHERIA YA KAZI ILI KULINDA HAKI ZA WAFANYAKAZI-NAIBU WAZIRI MAVUNDE

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Tulia Ackson akiongoza kikao cha kumi na tatu cha Mkutano wa saba wa Bunge la 11 leo Mjini Dodoma Aprili 27, 2017.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamadi Masauni akijibu maswali mbalimbali ya wabunge katika  katika kikao cha kumi na tatu cha Mkutano wa saba wa Bunge la 11 leo Mjini Dodoma Aprili 27, 2017. 
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Edwin Nyonyani akijibu maswali mbalimbali ya wabunge katika  katika kikao cha kumi na tatu cha Mkutano wa saba wa Bunge la 11 leo Mjini Dodoma Aprili 27, 2017.  
Naibu Waziri  Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Ajira Kazi na watu wenye Ulemavu  Mhe. Anthony Mavunde akijibu maswali mbalimbali ya wabunge katika kikao cha kumi na tatu cha Mkutano wa saba wa Bunge la 11 leo Mjini Dodoma Aprili 27, 2017.

Na Daudi Manongi-Maelezo, Dodoma.
WAAJIRI wote nchini yakiwemo makampuni ya Madini wametakiwa kutekeleza matakwa ya Sheria ya kazi kwa lengo la kulinda haki za wafanyakazi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri  Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Ajira Kazi na watu wenye Ulemavu  Mhe. Anthony Mavunde wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge leo Mjini Dodoma.

“Makampuni haya yana wajibu mkubwa wa kulinda haki za wafanyakazi,kupunguza migogoro isiyo ya lazima sehemu za kazi na kuongeza tija na uzalishaji mahala pa kazi.”Aliongeza Mhe.Mavunde.

Aidha amesema Ofisi yake imeendelea kutekeleza majukumu yake ya usimamizi wa Sheria kwa kufanya kaguzi sehemu za kazi kwa lengo la kuhakikisha kuwa waajiri wanazingatia matakwa ya Sheria,elimu ya Sheria za kazi inatolewa kwa waajiri,wafanyakazi na vyama vyao ili kuongeza uelewa wao katika kutekeleza Sheria.

Kuhusu ukaguzi wa mikataba kwa kampuni zinazofanya kazi migodini amesema  Serikali iliunda kikosi ambacho kilishirikisha Maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu,NSSF,SSRA,OSHA ,Mamlaka ya Mapato Tanzania na Wakala wa Ukaguzi wa Madini.

Amesema kikosi kazi hiki kilipewa jukumu la kufanya ukaguzi wa kina kwenye migodi iliyopo kanda ya ziwa na kaskazini kwa lengo la kuangalia hali halisi ya utekelezaji wa Sheria za kazi,afya na usalama mahali pa kazi,masuala ya hifadhi ya jamii,fedha na kodi.

Pamoja na hayo amesema kuwa Serikali inatambua umhimu wa uwekezaji katika kukuza fursa za ajira kwa watanzania na kuchangia kukua uchumi kwa ujumla.

“Serikali itaendelea kusimamia sheria za kazi ili kuhakikisha kuwa waajiri wote nchini wanatimiza wajibu wao na wawekezaji wamepata nafasi ya kuwekeza na kuchangia kukua kwa uchumi wa nchi yetu kwa kufuata sheria zilizoko nchini”Alisisitiza Mhe.Mavunde.

MANISPAA YA SINGIDA WAADHIMISHA MUUNGANO KWA KUFANYA USAFI WA MAZINGIRA

Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo (mwenye kofia nyeupe) akiongoza wakazi wa Manispaa ya Singida kuadhimisha miaka 53 ya Muungano kwa kufanya usafi sehemu mbalimbali za mji wa Singida jana. Mwenye gloves nyekundu ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida Bravo Kizito Lyampembile.
Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo (mwenye kofia nyeupe) akiongoza wakazi wa Manispaa ya Singida kuadhimisha miaka 53 ya Muungano kwa kufanya usafi sehemu mbalimbali za mji wa Singida jana. Mwenye gloves nyekundu ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida Bravo Kizito Lyampembile. 
Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo (mwenye kofia nyeupe) akiongoza wakazi wa Manispaa ya Singida kuadhimisha miaka 53 ya Muungano kwa kufanya usafi sehemu mbalimbali za mji wa Singida jana. Mwenye gloves nyekundu ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida Bravo Kizito Lyampembile. 
Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo (mwenye kofia nyeupe) akihimiza Watanzania kujenga utamaduni wa kushiriki maadhimisho ya Muungano wa Tanzania ili kuuenzi. Mwenye gloves nyekundu ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida Bravo Kizito Lyampembile. 

MKUU wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo amewaongoza wakazi wa manispaa ya Singida katika kuadhimisha miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kufanya usafi katika sehemu mbalimbali za mji wa Singida.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa zoezi la usafi, Tarimo amesema Watanzania wakiwemo wa wilaya ya Singida wanapaswa kuuenzi Muungano huu kwa kushiriki kikamilifu maadhimisho yake.

Amesema bila Muungano huu ulioasisiwa na viongozi wetu hayati mwalimu Nyerere na mzee Abeid Karume, Tanzania ya leo isingekuwepo.

“Maadhimisho haya sasa yameboreshwa kwa maana yanaweza kufanyika kwa kufanya usafi kama tulivyofanya sisi leo au kwa mazoezi ya mwili. Niwasihi tu Watanzania wenzangu kuyathamini maadhimisho haya na kushiriki bila kukosa kila mwaka”, amesema.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida Bravo Lyampembile amesema wananchi wa manispaa hiyo wamejitokeza kwa wingi na kushiriki vema kuadhimisha siku kuu ya Mungano.

“Ofisi yangu nayo imeshiriki watumishi wote ambao kwa siku ya leo afya zao ziko vizuri, wamejitokeza na kufanya usafi kama njia ya kuadhimisha siku kuu ya Muungano”, amesema Bravo.

TGGA YAZINDUA UPANDAJI MITI 600 KILA MKOA TANZANIA

Wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari Mtumba Manispaa ya Dodoma wakiwa na miche ya miti kila mmoja wao kabla ya kuipanda kwenye uzinduzi wa upandaji miti uliofanywa kitaifa na Girl Guides Tanzania mkoani humo. (Picha zote na John Banda; Kamanda wa Matukio Blog)

John Banda, Dodoma

CHAMA cha Tanzania Girl Guides (TGGA) kimezindua mradi wa upandaji miti kitaifa katika Shule ya Msingi ya Mtumba Manispaa ya Dodoma kwa lengo la kuifanya nchi kuwa ya kijani ili kuweza kuepukana na mabadiliko ya tabia nchi.

Akizungumza katika uzinduzi huo Kamishna Mkuu wa Tanzania Girl Guides nchini, Simphorosa Hangi  alisema wanakamilisha uzinduzi huo  wa kitaifa huku tayari shirika hilo likiwa limeshaanza upandaji wa miti hiyo katika mikoa mingine ya  Arusha, Lindi na Mwanza


Hangi alisema kuwa kwa sasa wapo katika mikoa 22 na wanaendelea kufanya juhudi ili waweze kukamailisha mikoa yote ikiwemo Zanzibar ambapo kila mkoa watapanda miti 600 huku wakiacha kila mkoa kuendelea na zoezi hilo ili kulifanya Taifa kuwa la kijani.


Naye Mwenyekiti wa Shirika hilo kitaifa, Martha Qorro  Alisema zoezi hilo linafanyika mashuleni na kuachwa kwa viongozi wa Girl Guides wa mkoa husika ambao watahakikisha wanapeleka na kupanda miti katika shule ambazo maji yapo yakutosha ili kuifanya miti hiyo kukua.


Kwa upande wake Mgeni Rasmi Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Dodoma, Aziza Mumba katika uzinduzi huo alisema juhudi hizo zinazofanywa na Shirika hilo zinafaa kuigwa ili kusaidia kurejesha uoto wa kijani ambao utasaidia kuyaweka mazingira kuwa mazuri yenye rutuba ya kutosha kutokana na mvua zitakazokuwa zikinyesha kila mahali. 

Wanachama wa Tanzania Girl Guides wakichimba moja ya mashimo ya kupanda mti katika Shule ya Msingi Mtumba Manispaa ya Dodoma wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupanda miti katika shule mbalimbali nchini.
Wanafunzi wanachama wa TGGA.
Wasanii wakitumbuiza kwa ngoma ya kabila la Wagogo wakati wa uzinduzi wa upandaji miti shuleni hapo.
Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Dodoma, Aziza Mumba akipanda mti katika Shule ya Msingi Mtumba wakati wa uzinduzi wa upandaji miti uliofanyika kitaifa shuleni hapo juzi.

Mwenyekiti wa TGGA, Marha Qorro akimwagilia mti baada ya kuupanda.
Viongozi na wanachama wa TGGA wakiwa katika picha ya pamoja.
Viongozi wa TGGA Makao Makuu Dar es Salaam, wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mkoa wa Dodoma.
Viongozi wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wanachama wa TGGA.
Wanafunzi wanachama wa TGGA wakiwa na miche ili waendelee na zoezi la kupanda miti shuleni hapo.