WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama
ameipongeza Mamlaka ya Serikali Matandao (eGA) kwa kutengeneza mfumo
utakaowezesha mifumo mbalimbali ya Serikali kubadilishana taarifa, jambo hili
ni hatua kubwa katika utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha mifumo ya TEHAMA ndani ya
Serikali inawasiliana na kubadilishana taarifa wakati wowote.
Akizungumza na watumishi wa Mamlaka
hiyo jijini Dodoma, Waziri Mhagama amefurahishwa
na utekelezaji wa haraka wa agizo hilo na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha
ili kuhakikisha mifumo yote ya TEHAMA inayotumiwa ndani ya Serikali inawasiliana
na kubadilishana taarifa ili kurahisisha utoaji huduma kwa umma.
“Ninatoa pongezi nyingi kwa Mamlaka kwa
kutekeleza agizo la Mhe. Rais kwa wakati na ninafahamu kuna baadhi ya taasisi za
umma zimeshaunganishwa katika mfumo huo, hivyo ninaagiza kazi ya kuunganisha
taasisi zilizobaki ikamilike kwa wakati na kufanya kazi kama ilivyodhamiriwa” Alisema
Mhe.Mhagama.
Aidha, Mhe. Mhagama ametoa wito kwa
watanzania kuendelea kutumia mifumo ya TEHAMA iliyobuniwa, kusanifiwa na
kutengenezwa na wataalamu wa ndani katika shughuli zao za kila siku kwani
zinarahisisha sana utendaji kazi, kupunguza gharama na mianya ya rushwa.
Pia, Mhe. Mhagama amesisitiza na
kuwataka watumishi wa umma nchini kufanya kazi kwa kufuata maadili ya Utumishi
wa Umma hasa wanapotumia mifumo ya kidijitali kwa uzalendo na uwajibikaji ili
kumsaidia Mhe. Rais katika kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi kama kaulimbiu
ya awamu ya sita ya “Kazi Iendelee”
inavyosadifu.
Akiwasilisha taarifa ya utendaji wa
Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama, Mkurugenzi Mkuu wa eGA Mhandisi Benedict Benny Ndomba amesema katika utekelezaji
wa agizo la Mhe. Rais, Mamlaka imetengeneza mifumo mbalimbali ya TEHAMA ikiwemo
Mfumo wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini (MUTAS) ambao mpaka sasa umeunganisha
na unatumiwa na taasisi kumi kwa hatua ya majaribio.
Katika taarifa yake, Mhandisi Ndomba
ameainisha baadhi ya mifumo mingine iliyotengenezwa na eGA kwa kushirikiana na taasisi
husika na kwa kutumia wataalamu wa ndani kuwa ni Mfumo wa Ukusanyaji Malipo ya
Serikali Kielektroni (GePG) unaosimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango, Mfumo
wa Pamoja wa Utoaji Ankara kwa Mamlaka za Maji nchini (MAJIIS) unaosimamiwa na
Wizara ya Maji, Mfumo wa Kusimamia Rasilimaliwatu Serikalini (New HCMIS)
unaosimamiwa na Ofisi ya Rais Utumishi, Mfumo wa kusimamia Shughuli na
Rasilimali za Taasisi (ERMS), Mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office) na Mfumo wa
Baruapepe Serikalini (GMS).
Ziara hiyo ya Waziri Mhagama kwenye
Ofisi ya Mamalaka ya Serikali Mtandao jijini Dodoma iliyofanyika Februari 11,
2022 ni sehemu ya kuzitambua taasisi zote zilizopo chini ya Wizara yake ya Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
We are available 24 hours a day, 7 days a week and can even arrange a free call-back service or a home visit if you prefer and know about back injury at work claims
ReplyDelete