TANGAZO


Friday, January 19, 2018

NAIBU WAZIRI WA MADINI MHE BITEKO AWATAKA WACHIMBAJI WADOGO KUTAMBUA UMUHIMU WA KULIPA KODI

Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza jambo wakati wa mkutano na wachimbaji wa madini ya Jasi na Chumvi Mkoani Mtwara, Leo 19 Januari 2018.(Picha Zote Na Mathias Canal)
Wachimbaji wa madini ya Jasi na Chumvi Mkoani Mtwara wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko wakati wa Mkutano wa pamoja na wachimbaji hao kwenye ofisi za Madini Kanda ya kusini, Leo 19 Januari 2018.
Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo Kanda ya kusini Ndg Peter Ludovick akieleza kero za wachimbaji mbele ya Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko wakati wa mkutano na wachimbaji wadogo, Leo 19 Januyari 2018.

Na Mathias Canal, Mtwara
WIZARA ya Madini imesisitiza wachimbaji wadogo na wakubwa nchini kutambua umuhimu wa ulipaji kodi kwa kila wanachozalisha kwani itasaidia kuongeza pato la Taifa kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi ikiwemo ukarabati wa miundombinu, Ujenzi na uimarishaji Wa sekta ya afya, elimu, Sekta ya umeme na sekta ya maji.

Akizungumza Mkoani Mtwara wakati wa mkutano na wachimbaji wa madini ya Jasi na Chumvi Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko amesema kuwa jamii bado haina elimu ya kutosha juu ya ulipaji kodi hivyo ofisi za madini nchini zinapaswa kuongeza msukumo Wa utoaji elimu juu ya ulipaji kodi na utunzaji wa kumbukumbuku za shughuli za uvunaji Madini kwa kila mahali kwenye leseni.

Mhe Biteko alisema kuwa wachimbaji wadogo kote nchini wanapaswa kutambua kuwa hawatakiwi kusalia kukwepa kodi badala yake wanapaswa kutoka kwenye uchuuzi na hatimaye kuhamia kwenye ufanyabiashara na kuhifadhi taarifa zote kwa mujibu wa kanuni kwa kipindi cha miaka 5.

Alisema kuwa mtu yeyote anapoitwa mfanyabiashara anatambulika katika jamii na serikali kwa ujumla wake hivyo kigezo kikubwa na muhimu kwa mfanyabiashara ni kulipa kodi kwa mujibu Wa kanuni, sheria na taratibu.

Akizungumza kwa msisitizo Mhe Biteko alisema kuwa watanzania wamempata Mhe Dkt John Pombe Magufuli kuongoza Taifa akiwa Rais Wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania katika kipindi cha miaka mitano hivyo wanapaswa kuunga mkono juhudi za utendaji wake kwa kulipa kodi kwa manufaa ya jamii nzima.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Wa Madini ameupongeza uongozi Wa Ofisi ya Madini Kanda ya Mtwara kwa ushirikiano mzuri na wachimbaji jambo ambalo limeimarisha utendaji wao pasina malalamiko dhidi ya serikali.

Kwa upande wake Mwenyekiti Wa Chama Cha wachimbaji Mkoa Wa Mtwara Ndg Festo Balegele akizungumza wakati Wa mkutano huo alimsihi Naibu Waziri wa Madini kutilia mkazo uongezaji thamani wa chumvi inayozalishwa nchini kwa kuikausha (Drying) na kuisaga (Grinding) sambamba na kuongeza Madini joto kwani itapelekea serikali kuokoa fedha nyingi za kigeni zinazotumiwa na serikali kuagiza chumvi nje ya nchi.

Alisema kuwa kila mwaka jumla ya tani 350 za chumvi huagizwa nje ya nchi ambapo ikiwasili nchini inauzwa kwa shilingi 500 kwa gramu 500 sawa na shilingi 50,000 kwa kilo 50 kiasi ambacho ni kikubwa Mara tano ya gharama za chumvi inayozalishwa nchini kwani inauzwa kwa shilingi 5000 kwa kilo 50.

Alisema kuwa chumvi inayoagizwa nje ya nchi ni kiasi cha Tani 350,000 kila mwaka huku akisisitiza kuwa serikali ingetilia mkazo na kuboresha miundombinu nchini ingerahisisha upatikanaji wa chumvi nyingi nchini ambayo inauzwa kwa kiasi kidogo chenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya watanzania.

No comments:

Post a Comment