Balozi Seif Ali Iddi (kulia) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania Mh. Mwigulu Lameck Nchemba ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
05/10/2016.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Mipaka ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania bado inaendelea kuwa na utulivu kutokana na kazi kubwa ya ulinzi inayotekelezwa na Jeshi la Polisi inayofanywa kwa kushirikisha vikosi vyengine vya ulinzi.
Alisema hali hiyo imeifanya jumuiya ya kimataifa yakiwemo mashirika na taasisi za Kimataifa kuisifu Tanzania kwa hatua hiyo jambo ambalo linapaswa kuenziwa ili Tanzania iendelee kubakia kuwa kisiwa cha amani Duniani.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mwigulu Lameck Nchemba aliyefika kumsalimia baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kushika wadhifa huo mazungumzo yaliyofanyika Vuga Mjini Zanzibar.
Hata hivyo Balozi Seif alitanabahisha kwamba pamoja na mafanikio hayo ya ulinzi wa mipaka lakini bado vyombo vya dola vina jukumu la kuwadhibiti na kuwachukulia hatua za kisheria watu au vikundi vinavyohusika kusafirisha watu wanaowaingiza Nchini kinyume na sheria za Nchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikumbusha kwamba jukumu la ulinzi wa raia na mali zao hapa nchini bado litaendelea kusimamiwa na kuwa mikononi mwa jeshi la Polisi chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Balozi Seif aliiomba Wizara hiyo kupitia Jeshi la Polisi kushirikiana na zaidi na Viongozi pamoja na Wananchi katika kuimarisha ulindi ndani ya mitaa katika dhana nzima ya ulinzi shirikishi.
Akigusia uwepo wa heshima kwa jeshi la Polisi Nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameikumbusha Wizara ya Mambo ya Ndani kurejesha mpango wa zamani wa ujenzi wa nyumba za makaazi ya askari wake ili kurejesha heshima ya askari wa Jeshi hilo.
Alisema wapo askari Polisi katika baadhi ya maeneo Nchini wanashindwa kutekeleza vyema wajibu wao kwa kuhofia kulaumiwa kutokana na ukaribu wao wa ndani na raia katika maeneo au nyumba wanazoishi na raia hao kiasi kwamba muhali unachukuwa nafasi zaidi na kuharibu kazi.
Alilipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua lililochukuwa la kufanya uchunguzi dhidi ya askari wa usalama Bara barani wa Jeshi hilo aliyetuhumiwa kuchukuwa rushwa ya fedha taslim kwa raia mmoja wa kigeni baada ya kumkamata akiendesha gari bila ya kufunga ukanda Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Balozi Seif alisema kitendo hicho ambacho kilirikodiwa na kusambazwa katika mitandao ya kijamii kimelitia aibu Jeshi la Polisi Nchini kiasi kwamba Uongozi wa Jeshi hilo utalazimika kuwa mkali katika kukabiliana na uzembe kama huo kwa kuwafukuza kazi moja kwa moja wale wanaopatilana na na makosa ya rushwa.
Mapema Waziri wa Mambo ya Ndani Tanzania Mh. Mwigulu Lameck Nchemba ameziomba Taasisi zinazohusika na sheria ya usalama bara barani Zanzibar kukamilisha Kanuni zilizofanyiwa marekebisho ili ziende sambamba na zile zilizoanza kutumika Tanzania Bara.
Mh. Nchemba alisema katika kukabiliana na makosa yanaofanywa na baadhi ya madereva wazembe bara barani shughuli za ukaguzi unaosimamiwa na jeshi la Polisi inapaswa ziwe rasmi ili kudhibiti utumiaji mbaya wa bara bara unayofanywa na baadhi ya madereva.
Waziri wa Mambo ya Ndani Tanzania alimueleza Balozi Seif kwamba ongezeko kubwa la vyombo vya moto vya usafiri wa bara barani pamoja na uzembe wa madereva umeisababishia Serikali kuamua kufanya marekebisho ya sheria katika kukabiliana na matukio hayo.
Alisema Kanuni inayosimamiwa na Jeshi la Polisi ya kutoa adhabu ya faini ya papo kwa papo dhidi ya madereva wanaoendesha vyonvo vya moto bara barani bila ya kuzingatia sheria na taratibu za bara bara imesaidia kupunguza makosa na ajali kwenye bara bara nyingi nchini.
Alieleza kwamba kwa upande mwengine mpango huo wa marekebisho ya Kanuni za usalama bara barani ulioanza kutumika upande wa Tanzania Bara tayari umelisaidia Taifa kuongeza mapato yake katika ukusanyaji wa Kodi.
Waziri Mwigulu Lameck Nchemba alifahamisha na kusisitiza kwamba kiu ya Watendaji wa Wizara yake pamoja na Vikosi vya ulinzi vilivyo chini ya Wizara hiyo ni kujituma kwa uadilifu ili kufikia matarajio yaliyowekwa na Taifa.
No comments:
Post a Comment