Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje
Na Immaculate Makilika- Maelezo
SERIKALI inaandaa mtaala wa kuongeza ustadi na ujuzi kwa watanzania wanaofanya kazi za ndani katika nchi za Mashariki ya Kati.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Abdallah Kilima alipokuwa akikanusha habari iliyotolewa na Gazeti la Tanzania Mpya la Oktoba 04,Mwaka huu,Toleo namba 23 katika Ukurasa wa 4, lililokuwa na habari iliyosema “Watanzania wateswa nchini Oman na wengine hunyofolewa figo zao na kupewa ndugu wa waajiri wenye mahitaji”.
Kutokana na hayo Balozi Kilima alifafanua kuwa habari hiyo haina ukweli wowote, isipokuwa ni maoni binafsi ya mwandishi wa gazeti hilo na hayawakilishi msimamo wa Serikali kuhusu masula ya wafanyakazi za ndani wakitanzania nchini Omani.
Aidha, Balozi huyo amesisitiza kuwa nia ya Serikali ya kuanzisha mtaala huo ni katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakumba nazo watanzania wanaofanyakazi za ndani nchini Oman.
“Serikali imeazimia kutumia Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) ili kutoa mtaala utakaosaidia kutoa mafunzo kwa maana ya utaratibu na utamaduni wa nchi wanazokwenda kufanyakazi, ili kusaidia watanzania kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu kazi husika na changamoto zake kabla ya kukubali kufanyakazi hizo,” alisema Balozi Kilima.
Sambamba na hilo Serikali imeendelea kuwataka watanzania kufuata utaratibu kabla ya kwenda kufanyakazi katika nchi hizo kwa kutumia mawakala rasmi wa ajira walioandikishwa na mamlaka husika pamoja na kuwepo mkataba wa ajira unaotambuliwa na Mamlaka za nchi wanazookwenda ili kuepuka usumbufu na changamoto wanazoweza kuzipata ikiwemo kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na ukatili.
Balozi Mwilima ameongoza kuwa katika kupata suluhisho la kudumu katika kuwasaidia watanzania kupata fursa za ajira nje ya nchi,Wizara kwa kushiririkiana na wadau imeendelea kufanya jitihada za kusaini Mikataba ya Ushirikiano katika Sekta ya ajira na kazi baina ya Serikali ya Tanzania na nchi mbalimbali.
Watanzania 5600 wanakadiriwa kufanyakazi katika kada za madaktari, walimu, wauguzi, wahadhiri, wapishi, wahudumu wa mashambani na bustani na watumishi wa nyumbani, na kati ya hao karibu watanzania 200 ndio wanaofanyakazi za ndani katika nchi za Mashariki ya Kati.
No comments:
Post a Comment