Baadhi ya Vijana wa DSW wakifuatilia mada wakati wa
mdahalo wa vijana kuhusu Stadi za Maisha ikiwa ni moja ya programu katika
kuadhimisha Wiki ya Vijana ambayo kitaifa inafanyika mkoani Tabora. (Picha zot na
Frank Shija, Tabora)
SHIRIKA lisilo la Kiserikali linalojihusiha na changamoto
zitokanazo na ongezeko la idadi ya watu, DSW limefungua jumla ya vituo 33 kote
nchini kwa ajili ya kuwaelimisha vijana kuhusu masuala ya afya na uzazi, kujitambua
na kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza katika Maonyesho ya Wiki ya Vijana yanayoendelea
mjini Tabora, Meneja Mkazi wa Miradi wa shirika la DSW nchini Tanzania Bw. Avit
Buchwa alisema vituo hivyo vimefunguliwa kwa ajili ya kuwaelimisha vijana
kuhusu masuala ya afya ya uzazi ili wabadilike na kuibadilisha jamii.
Vituo
hivyoni sehemu muhimu kwa vijana kwani wanaweza kutoa mawazo yao kwa uwazi kwa
jamii inayowazunguka.
Bw. Buchwa ametaja mikoa ambayo shirika hilo limefungua
vituo kuwa ni pamoja na Arusha, Kilimanjaro, Lindi, Mtwara na Manyara.
Katika
mikoa hiyo vituo hivyo vinawafanya vijana kuwa karibu na jamii husika ambayo
inakuwa rahisi kuona na kutambua changamoto zao na kuzishughulikia kikamilifu.
“Vijana wanapata fursa ya kuelimishwa kupitia Vituo vyetu
vilivyoko katika maeneo mbalimbali hapa nchini na kwa sasa tumejikita zaidi
katika kuelimisha Vijana kujitambua na kutatua changamoto zinazowakabiri
kupitia njia ijulikanayo kama kijana kwa Kijana Project”Alisema Buchwa.
Amesema kuwa katika vituo hivyo mtazamo rafiki kuhusu
masuala ya afya ya uzazi kwa vijana unatumika katika shughuli zao. Hii
imesaidia katika kuvifanya vituo hivyo kuwa na ufanisi mkubwa katika utendaji
wa kila siku.
DSW linawawezesha vijana kujitambua na kufanya maamuzi
sahihi, kuwajengea uwezo kiuchumi kwa kuwaunganisha na taasisi za fedha kwa
ajili ya kupata mikopo ya maendeleo, kuwafundisha vijana stadi za kazi ikiwemo
masuala ya uongozi na kuwaandalia ziara za kimafunzo ndani nanje ya nchi ili
kuwapatia uzoefu mbalimbali, alisema Bw. Buchwa.
Aidha Buchwa alitoa raia kwa Serikali kupitia Halmashauri
zote nchi kuona umuhi wa suala la Afya ya Uzazi kwa Vijana linaingizwa katika
mipango yao (CCHP) na kutengea fedha kwa ajili ya utekelezaji ambapo alisema
kwa kufanya hivyo kutatimiza haki ya msingi ya Kijana kupata mahitaji ya
Kiafya.
Kwa upande mwingine, Katibu wa Kituo cha Vijana Wilaya ya
Hai,Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Aziz Salim amesema DSW imewasaidia sana vijana
kupata mafunzo mbali mbali kuhusu stadi za maisha pia na kupatiwa pesa mbegu
kwa ajili ya miradi ya vijana.
Ameongeza kuwa vijana makini ambao wamepata fursa ya kupata
huduma katika Vituo vya Vijana (YEC) vinavyoendeshwa na DSW wamefanikiwa sana
kubadilika kimaisha na kuwa na mtazamo chanya wa kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment