TANGAZO


Saturday, August 16, 2014

Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki awataka wajasiriamali kuchangamkia Masoko








Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo, John Mahaley akitoa neno kwenye Maonesho ya Bidhaa za Wajasiriamali wa Bagamoyo 2014, kwenye viwanda vya kituo cha mabasi mjini  Bagamoyo jana.






Msomaji wa Risala ya Wajasiriamali kwa niaba ya Teddy Davis akisoma risala hiyo mbele ya mgeni rasmi (hayupo pichani) katika Maonesho ya Bidhaa za Wajasiriamali wa Bagamoyo 2014.





Msoma Risala akimkabidhi Mgeni Rasmi wa Maonesho ya Bidhaa za Wajasiriamali wa Bagamoyo 2014, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Joyce Mapunjo.





Mgeni Rasmi wa Maonesho ya Bidhaa za Wajasiriamali wa Bagamoyo 2014, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Joyce Mapunjo akiwahutubia washiriki wa maonesho (hawapo pichani).





Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Joyce Mapunjo, akisaini kitabu cha mahudhurio cha Shirika la Viwango Tanzania (TBS) alitembelea banda hilo.Kulia ni Kaimu Mkuu wa Uthibitishaji wa shirika hilo Ashura Kilewela. 





Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Joyce Mapunjo, akingalia mvinyo wa Bagamoyo wakati alipotembelea banda la Smoke House Store kwenye maonesho hayo.




Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Joyce Mapunjo, akisalimia na  Mfanyabiashara wa Nyaraka za Kihistoria wa Bagamoyo Profesa Samahani Kejeli wakati alipomtembelea kwenye banda lake.




Mkurugenzi wa kiwanda cha Smoke House Store Teddy Davis akisoma risala kwa mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo.





Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Joyce Mapunjo, akifungua kitambaa kuashiria kufungua kiwanda cha Smoke House Store huku Mkurugenzi wa kiwanda hicho na wadau wengine wakishuhudia ufunguzi huo.




Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Joyce Mapunjo,  akikata mlo maalum wa ndafu baada ya kufungua kiwanda cha Smoke House Store.



Baadhi ya wajasiriamali walioshiriki kwenye ufunguzi wa kiwanda hicho. (Picha zote na Hussein Makame-MAELEZO)



KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Joyce Mapunjo, amewataka wajasiriamali wa Bagamoyo na Watanzania kwa ujumla kuwa wabunifu na kuongeza thamani za bidhaa zao ili kuhakikisha wanafaidika na fursa za masoko ya bidhaa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
 
Ameyasema hayo jana, wakati akifungua Maonesho ya Bidhaa za Wajasiriamali wa Bagamoyo 2014, yaliyohudhuriwa na wajasiriamali na wadau mbalimbali kutoka wilaya hiyo ya mkowa wa Pwani.
Alisema Bagamoyo inazungukwa na maeneo muhimu ambayo ni fursa za masoko ya bidhaa mbalimbali ikiwemo soko la bidhaa la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo yanahitaji kuchangamkiwa.

Aliwataka wajasiriamali kuhakikisha wanazalisha bidhaa zao kukidhi mahitaji ya soko la dunia, hivyo wanatakiwa kufikiria soko kubwa zaidi li kufaidika na fursa kubwa ya soko hilo.

“Nashauri kwa wajasiriamali tuzidi kuwa wabunifu, tuzidi kufikiria kwa mapana, usifikirie Tanzania, fikiria kimataifa kwamba bidhaa unayozalisha, je katika dunia hii inaweza kupata soko kokote pale duniani” alisema Katibu Mkuu Mapunjo.

Aliongeza kuwa ni vyema wajasiriamali wakajikita zaidi kuboresha ufungashaji wa bidhaa zao na kuhakikisha zinapimwa na kuwa na viwango vinavyotakiwa kwani bila ya kuzingatia viwango hawawezi kupata soko la kimataifa.

Naye mwenyekiti wa kamati ya maandalizi Teddy Davis, alisema lengo la maonesho hayo ni kuwakutanisha wajasiriamali wa nje na ndani ya wilaya ya Bagamoyo kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili.

“Pia lengo ni kushirikiana kutambua fursa zilizopo katika wilaya ya Bagamoyo ikiwemo mabonde ya maji kwa kwa umwagiliaji, kuwepo kwa taasisi za kifedha na kuangalia jinsi ya kuzitumia ili kufaidika nazo” alisema Teddy.

Akizungumzia changamoto zinazowakabili, Teddy alisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ufinyu wa maeneo, riba kubwa za taasisi za fedha ikiwemo benki na ukosefu wa elimu ya kutosha ya ujasiriamali.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Mapunjo alifungua kiwanda cha Smoke Huose Store kinachotengeneza mvinyo wa Bagamoyo na kuwataka wajasiriamali wengine kuiga mfano wa mkurugenzi wa kiwanda hicho Teddy Davis.

Aliwataka Watanzania wafanye uchambuzi wa kutosha kuhusu masuala ya ujasiriamali kwani Serikali imekuwa ikiweka mazingira ya kisera kuhakikisha wananchi wanafaidika na shughuli za ujasiriamali.
“Kuna mchango wa kitaasisi kwa ajili ya kuboresha masuala ya ujasiriamali kuanzia mafunzo na kuwezesha ujasiriamalikwa mfano kuna Wizara ya Viwanda na Bishara iliyo na idara nzima inayoshughulikia ujasiriamali” alisema Katibu Mkuu Mapunjo.

Alitaja Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) ambalo lina ofisi katika kila wilaya na ambalo kazi yake kubwa ni kuweza kutoa mafunzo na kutoa vitendea kazi pale vinapohitajika kwa wajasiriamali.
“Kwa mfano huyu mjasiriamali hapa, ametuambia kwamba mafunzo ya kwanza kuhusu namna ya usindikaji aliyapata SIDO, lakini pia alivyona kuna vitu anavihitaji aliwezeshwa na SIDO, na ametuambia sasa amepata TBS na sasa amefikia hatua kubwa katika shughuli zake” aliongeza Katibu Mkuu Mapunjo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Teddy alisema kiwanda hicho kilianzishwa na kusajiliwa mwaka 2009 na kuanza na uzalishaji wa lita 40 za mvinyo lakini sasa kinazalisha lita 1200 huku kikiwa kimeajiri vijana 25, watano kati yao ni waajiriwa wa kudumu. 
 
Alisema kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya soko la uhakika hali inayomfanya kuhitaji kukitangaza kiwanda chake ili kupanua soko la bidhaa zinazozalishwa ikiwemo mvinyo na juisi ya lozera.
Maonesho hayo ya ujasiriamali hufanyika kila mwaka wilayani Bagamoyo huku kaulimbiu yamwaka huu ikiwa ni “Jiajiri, ongeza kipato, futa umasikini, tangaza nchi yako”.

No comments:

Post a Comment