TANGAZO


Thursday, November 28, 2013

Mbio za Serengeti Marathon kutimua vumbi Disemba 4

Mratibu wa mashindano ya Serengeti Marathon Xavier Mhagama akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kuhusu mbio hizo zinazotarajia kutimua kivumbi desemba nne, kulia ni Mwenyekiti wa Bodi toka Kampuni ya bia ya Serengeti Jaji Mstaafu Mark Bomani.
Mwenyekiti wa bodi toka Kampuni ya bia ya Serengeti Jaji Mstaafu Mark Bomani akieleza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kuhusu kampuni ya Serengeti ilivyojipanga kudhamini michezo mbalimbali hapa nchini, kushoto ni Mratibu wa mashindano ya Serengeti Marathon Xavier Mhagama.
Meneja Masoko wa kampuni ya bia ya Serengeti akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema hii leo jijini Dar es Salaam, juu ya mikakati ya kampuni hiyo katika kuinua michezo hapa nchini, kushoto ni Mwenyekiti wa bodi toka Kampuni ya bia ya Serengeti Jaji Mstaafu Mark Bomani. (Picha zote na Eliphace Marwa - MAELEZO)



Na Eliphace Marwa - Maelezo
Mashindano ya riadha yajulikanayo kama Serengeti  marathon yanatarajia kutimua vumbi desemba nne mwaka huu ambapo wanariadha,  viongozi na wananchi kutoka sehemu mbalimbali nchini watashiriki mashindano hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo jijini Dar es Salaam, mratibu wa mashindano hayo Xavier Mhagama amesema kuwa viongozi watakimbia umbali wa kilometa tano wakati washiriki wengine watakimbia umbali wa kilometa ishirini na maoja hadi arobaini na mbili.

“Mashindano ya mwaka huu yataanzia kilometa tatu ndani ya hifadhi ya Serengeti na kupita Serengetistopover, Ndabaka Lodge, Lamadi, Kuelekea Kalemela na kamalizikia katika viwanja vya Serengeti Stopover Lodge jirani na Lango la Ndabaka,” alisema bwana Mhagama

Aidha Mwenyekiti wa Bodi toka kampuni ya bia ya Serengeti Jaji Mstaafu Mark Bomani alisema kuwa wamefurahi sana kuwa moja wa wadhamini wa mashindano hayo kwani lengo la mashindano hayo ni zuri na limekuja wakati muafaka.

“Kama inavyosema kauli mbiu ya mashindano haya kuwa  ni kupiga vita ujangili, kupiga vita mauaji ya watoto wenye ulemavu wa ngozi na kupinga unyanyasaji kijinsia hususani ukeketaji unaondelea katika mikoa ya kanda ya ziwa,” alisema Jaji Bomani.

Mashindano haya ya Serengeti Marathon msimu wa pili yatafunguliwa na Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda  ambapo mshindi wa kwanza atajinyakulia kitita cha shilingi milioni mbili na nusu.

No comments:

Post a Comment