Waziri
wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa MaKame Mbarawa (kushoto akizungumza na Postamasta Mkuu wa
Shirika la Posta Tanzania (TPC) Bwana Deos Mndeme kabla ya Waziri kufungua
mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo katika ukumbi wa British
Council jijini Dar es Salaam jana.
Profesa
Mbarawa (kulia) na Bwana Mndeme wakielekea katika ukumbi wa mkutano huo.Baadhi ya Mameneja wa mikoa na Shirika hilo waliohudhuria mkutano huo. Kutoka kishoto ni Lawrence Mwasikili (Dar es Salaam), Rehema Marijani (Tanga), Batuli Marungu (Kilimanjaro) na kulia ni Meneja Huduma za Fedha wa Makao Makuu Janeti Msofe.
Katibu wa Baraza hilo Emmanuel Lugomela akizungumza wakati wa mkutano huo.
Mameneja wa Makao Makuu wa Shirika hilo kutoka kushoto Fadya Zam wa Huduma za Barua na Logistiki, Aicha Nangawe wa UPU, na John Tinga wa EMS wakiwa katika mkutano huo.
Postamasta Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo Bwana Deos Mndeme akizungumza wakati wa mkutano huo.
Mameneja wa mikoa wa Shirika hilo wakisikiliza kwa makini hotuba ya Waziri. Kutoka kulia ni Mary Nsangila wa Kagera, Abdul Mwinyimtama wa Arusha, Rouchus Assenga wa Ruvuma na Evord Mwauzi wa Kigoma.
Meneja barua na Logistiki Fadya Zam akichangia hoja.
Baadhi ya wajumbe, wakiwa kwenye mkutano huo wa Baraza la Wafanyakazi.
Meneja wa Mkoa wa Singida Matembele Mkukzi akichangia mada.
Mameneja wa mikoa na wawakilishi wa wafanyakazi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania, Dk. Yamungu Kayandabila akimkaribisha Mheshimiwa Waziri wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.
Profesa Mbarawa akihutubia.
v
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania,
v
Mwenyekiti wa Baraza Kuu na
Postamasta Mkuu wa Shirika,
v
Katibu wa Baraza,
v
Wajumbe wa Baraza hili,
v
Wanahabari,
v
Wageni Waalikwa,
v
Mabibi na Mabwana.
1.0
SHUKRANI
Kwanza
kabisa napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha
kujumuika hapa siku hii ya leo. Aidha, naomba niwashukuru kwa kunialika ili niwafungulie rasmi mkutano wa 22 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa
Shirika la Posta Tanzania.
2.0 PONGEZI
Pia napenda niwapongeze kwa kuwa na utaratibu wa kuandaa
mikutano kama hii ambayo inatoa fursa ya ushirikishwaji wa kada mbalimbali za
wafanyakazi wenu waliosambaa nchini kote.
3.0 UMUHIMU WA
BARAZA LA WAFANYAKAZI
Ndugu Wajumbe,
Kwa mujibu wa Agizo la Rais Namba Moja la mwaka 1970,
Baraza la Wafanyakazi ni muhimu katika:-
3.1 kujenga mtizamo
wa pamoja kati ya uongozi na wafanyakazi kuanzia ngazi ya chini kabisa,
menejimenti hadi Bodi ya Wakurugenzi;
3.2
kuongeza uwajibikaji, morali na tija
katika utendaji;
3.3 kupunguza
migogoro na migongano katika sehemu za kazi.
4.0 MADA NA AGENDA ZA MKUTANO HUU
Salaam za ukaribisho zimetujulisha kuwa mkutano huu wa
siku tatu utajadili masuala muhimu ambayo ni;
4.1 Mapendekezo
ya Mpango Mkakati wa Shirika wa miaka
mitano kuanzia mwaka kesho 2014 hadi
mwaka 2018.
4.2 Taarifa
ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya mwaka huu na mapendekezo ya Mpango wa
Maendeleo na Bajeti ya mwaka ujao wa 2014.
4.3 Aidha, mtapata fursa ya kujadili mada juu ya mafao ya
Mfuko wa Pensheni
wa PPF, huduma zinazotolewa na
Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya (NHIF), fursa za
mikopo ya nyumba
za makazi kutoka Benki ya CRDB
na pia Shirika la
Nyumba la Taifa (NHC).
5.0 DIRA
YA SHIRIKA
Ndugu Mwenyekiti,
5.1 Nafahamu kwamba mwaka jana wakati wa mkutano wa Baraza hili,
mlijadili mapendekezo ya Mpango wa muda mrefu (Master Plan) wa Shirika hili
kuelekea miaka kumi ijayo (2014/2023).
5.2 Sina
shaka mtakubaliana nami kuwa uhai na uendelevu wa Shirika hili licha ya kuwepo
changamoto, umetokana na mipango shirikishi inayogusa maeneo yote muhimu.
5.3 Ni
matarajio yangu kuwa Mpango Mkakati mtakaojadili wakati wa mkutano huu
mtazingatia hali halisi na mazingira ya sasa na ya baadae ya Shirika hili
katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
5.4 Mtapaswa
kujadili mafanikio mliyopata na changamoto mlizokumbana nazo katika utekelezaji
wa majukumu na mipango ya Shirika pamoja na kujiwekea malengo na Mpango Kazi
utakaowezesha kuendeleza ustawi wa Shirika, kuboresha huduma zilizopo,
kuanzisha huduma mpya zinazozingatia mahitaji ya soko na kubuni vyanzo vipya ya
mapato hatimaye muweze kuboresha maslahi ya watumishi na kutoa gawio kwa
Serikali.
Ndugu
Mwenyekiti,
5.5 Wizara
yangu inatambua jitihada zenu ambazo zimewezesha kupata mafanikio katika
ongezeko la mapato na pia ubora wa huduma, lakini mimi kama Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, ninaamini kwa dhati kuwa bado kuna fursa ya
kufanya vizuri zaidi hususan endapo mtapambanua na kutangaza huduma zenu kwa
wadau wakubwa kama Wizara, Taasisi na Ofisi za Serikali pamoja na Makampuni na Asasi
binafsi ambazo zingependa kutumia Shirika hili katika kufikisha huduma na
bidhaa zao kwa wananchi wa kawaida ambao wako nje ya miji mikuu ya mikoa.
6.0
CHANGAMOTO ZA SHIRIKA
Ndugu Mwenyekiti,
6.1 Wizara
yangu inatambua kuwepo kwa changamoto zinazohusu nakisi ya mtaji wa Shirika na
kuchelewa kulipa madeni ambayo Shirika lilirithi hususan pensheni.
6.2 Ninapenda
kutumia fursa hii kuwajulisha kuwa utaratibu wa kuboresha mtaji utabainishwa
baada ya kukamilika zoezi la kurekebisha mizania ya Shirika. Aidha Wizara yangu itaendelea kushirikiana na
Wizara ya Fedha ili kuhakikisha madeni yaliyosalia ya pensheni yanalipwa.
6.3 Jitihada
hizi zitaambatana na kuweka mfumo utakaowezesha kulipatia Shirika ruzuku ya
kugharamia ufikishaji wa huduma za msingi za Posta katika maeneo yenye
changamoto za kiuchumi. Hatua hii itawezekana endapo mtaweza kubainisha manufaa
ya huduma hizo, gharama zinazohusika na kuwasilisha maombi katika Mfuko wa
Mawasiliano kwa wote (UCSAF).
Ndugu
Mwenyekiti,
6.4 Ziko
changamoto za ushindani katika kutoa huduma, mabadiliko ya mahitaji ya wateja
na maendeleo ya teknolojia.
6.5 Ushindani
katika kutoa huduma unatoa fursa za maboresho, kupunguza urasimu na uzembe na
mazoea yasiyo na tija. Aidha ushindani unawapa
wateja fursa ya kuchagua huduma na
bidhaa bora zinazokidhi mahitaji yao.
Kwa misingi hiyo, ni lazima Shirika
lijiimarishe zaidi katika ushindani wa soko.
Serikali itaendelea kuweka sera, sheria na kanuni stahiki pamoja na
kujenga na kuboresha miundombinu ya kitaifa kama vile mkongo wa mawasiliano,
anuani za makazi na Misimbo ya Posta, njia za usafiri na usafirishaji, n.k. Aidha Serikali kupitia Mamlaka zinazosimamia
Udhibiti itaendelea kuhakikisha kuwepo
kwa ushindani unaokubalika (level playing
field) na unaojali maslahi ya jamii na taifa kwa ujumla.
Matakwa ya Wateja
6.6 Sambamba
na masuala haya, mahitaji na matarajio ya wateja na wananchi yanabadilika kwa
kasi. Mnapaswa kufahamu kuwa wateja wenu
wa sasa wako tofauti sana na wateja wa miaka iliyopita.
Kwa mfano, wateja wanaotuma vipeto na
vifurushi kutoka hapa Tanzania kwenda nje ya nchi, ni muhimu kuwapa hakikisho
kuhusu muda wa kufika na hivyo kujenga imani.
Hivyo hivyo hata kwa mteja anayetuma vitu vyake kutoka na kwenda hapa nchini atapenda kupata uhakika huo
pamoja na kupata taarifa hizo katika kompyuta na/au simu yake.
7.0
MATUMIZI YA TEHAMA
Ndugu
Mwenyekiti
7.1 Shirika hili linatakiwa kuongeza
matumizi ya TEHAMA katika uendeshaji wa huduma zake ikiwa ni pamoja na
kuunganisha ofisi zote za Posta za mikoa na wilaya katika mtandao wa
kielekitroniki.
7.2 Ninafahamu kuwa kwa wakati huu Posta
Kuu za mikoa zimeunganishwa katika mtandao huo, lakini kiwango hiki ni kidogo
na hasa ikizingatiwa kuwa Shirika ni mtoa huduma za msingi kwa jamii (designated
public operator).
7.3 Matumizi ya teknolojia mpya sio suala
la hiari bali ni suala muhimu na la lazima.
Tumieni kikamilifu fursa zinazotokana na maendeleo ya TEHAMA, uwepo wa Anuani
za Makazi na Misimbo ya Posta na maboresho ya huduma za fedha katika kuanzisha
huduma za kisasa na kujiimarisha kwenye usambazaji wa vipeto, vifurushi na
mizigo yenye bidhaa mbalimbali na hivyo kushiriki katika maboresho ya shughuli
za wajasiriamali (Small and Medium Enterprenuers).
7.4 Kuhusu usambazaji wa huduma Vijijini,
bado Shirika halijafikia kiwango kinachohitajika katika maeneo ya
vijijini. Hamna budi kuongeza kasi
katika eneo hili ili kukidhi matakwa ya leseni ya kutoa huduma za msingi kwa
jamii. Mwelekeo wenu uwe katika kutumia teknolojia ya kisasa na pia kutumia mawakala katika kuendesha vituo
ambavyo mahitaji ya huduma hayalingani na gharama za kuweka watumishi wenye
ajira za kudumu.
8.0
MATUMIZI YA FURSA ZILIZOPO
Ndugu Mwenyekiti,
8.1 Pamoja na changamoto zinazolikabili Shirika
hili, bado kwa upande mwingine changamoto hizi huleta fursa nzuri ambazo zitaliwezesha
Shirika kuimarika zaidi. Ningependa
niwakumbushe baadhi ya fursa hizi ambazo kama mtazichangamkia, Shirika hili
linaweza kupiga hatua zaidi.
Mtandao wa Kitaifa
8.2 Katika ngazi ya kitaifa, Shirika hili
ni miongoni mwa taasisi zenye mtandao wa ofisi zilizosambaa nchini kote. Kwa
mfano; takwimu zenu zinaonyesha
kuwa ofisi za Posta 164 zinaendeshwa na watumishi wenye ajira za kudumu. Aidha huduma za internet hutolewa kwenye ofisi 44 ambapo vituo 185
vinaendeshwa na wakala ambao hawatoi baadhi ya huduma za Posta.
8.3 Wizara yangu ingependa kuona Makao
Makuu ya kila wilaya kuna ofisi ya Posta
inayoendeshwa na watumishi wenye ajira za kudumu na wenye uwezo wa kutoa huduma
zote za Posta, internet na huduma za uwakala.
Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya
Mawasiliano ya Elektroni na Posta (EPOCA) na kanuni zake, Shirika hili limepewa
mamlaka ya kuwa msafirishaji pekee wa barua na nyaraka zenye uzito usiozidi
gramu 50 na vipeto visivyozidi kilo 10.
Nawaelekeza muendeleze kampeni ya kuhamasisha na kuelimisha Taasisi za
Serikali na Asasi Binafsi waweze kuelewa manufaa ya kutumia kwa wingi huduma
zenu za EMS courier na City Urgent Mail
(pCUM) pamoja na kutumia ofisi na vituo vya Posta kufikisha huduma zinazotokana
na mtandao (electronic services)
karibu na wananchi.
Mtandao wa
Kimataifa
Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe,
8.4 Wizara yangu inatambua kuwa ofisi za Posta
hapa nchini zimeunganishwa katika mtandao wa ofisi za Posta duniani (global
connectivity) ambao una ofisi za Posta zipatazo 660,000 zilizoko katika nchi
196 wananchama wa Umoja wa Posta Duniani.
8.5 Mtandao huu wa kimataifa utumike kama
fursa adhimu ya kuboresha huduma za
biashara za ndani na biashara za nje (Export and Import) kwa kiwango cha
kimataifa. Kwa mfano mwaka jana Shirika
hili limetunukiwa na Umoja wa Posta Duniani (UPU) hati ya daraja la “C” ya
utoaji wa huduma bora hususan kwenye kasi na usalama wa mifumo ya kushughulikia
barua na vifurushi. Sasa ni wakati wa
kudhamiria kupata hati ya daraja “B” na
hata “A”.
8.6 Jitihada zenu ziambatane na kuwapatia
watumishi wenu mafunzo ya kikazi (on the job training) na kufanya vikao vya kuelimisha na
kuhabarisha, hivyo kuwajengea umahairi wa kumudu majukumu yao.
8.7 Ni lazima viongozi na watumishi wa
kada zote kujenga nidhamu ya kazi, kujituma, kuheshimu kanuni na taratibu,
kuongeza ubunifu na kufanya kazi kwa uaminifu na ufanisi wenye tija kwa
Shirika. Maslahi bora kwa watumishi
yatatokana na ongezeko la ufanisi na tija, hakuna njia mbadala.
9.0
DIRA YA MAENDELEO YA TAIFA YA MWAKA
2025
Ndugu Mwenyekiti,
9.1 Wote tunafahamu kuwa malengo ya Dira ya
Taifa ni kuleta maendeleo ya haraka nchini na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya
uchumi wa kati ifikapo mwaka 2015.
9.2 Mojawapo ya malengo hayo ni pamoja na
kuondoa umaskini, kupanua huduma za kifedha, kuongeza matumizi ya sayansi na
teknolojia, kupanua na kuboresha miundombinu na kurahisisha upatikanaji wa
mawasiliano, elimu na huduma za afya kwa jamii.
9.3 Shirika la Posta Tanzania ni mojawapo
ya taasisi muhimu katika kufanikisha malengo haya. Kwa hiyo hii ni changamoto
kwenu ninyi viongozi wa Shirika hili kubuni na kutekeleza programu zenye
kuwiana na malengo ya kitaifa na kimataifa.
10.0 MFUMO WA “TEKELEZA SASA KWA MATOKEO MAKUBWA”
Ndugu Mwenyekiti,
10.1 Ili kufikia malengo ya Dira na
Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2015, Serikali imeamua kutekeleza mfumo wa “Tekeleza
sasa kwa Matokeo Makubwa” (Big Results Now) ambao umeambatana na kuanzisha Mikataba ya
Utendaji kazi katika Utumishi wa Umma.
10.2 Ninachukua fursa hii kutoa maelekezo
kwa Uongozi wa Shirika kuhakikisha ngazi zote za uongozi na usimamizi zinaingia
katika mkataba wa utendaji unaoweka bayana vigezo na viashiria vya utendaji
kazi ambavyo vitatokana na dira/shabaha, vipaumbele na malengo ya Shirika
yaliyomo katika Mpango Mkakati na Malengo ya Bajeti.
10.3 Aidha, ni muhimu na lazima kujenga
mfumo wa uwajibikaji ambapo tathmini na mrejesho kuhusu utendaji kazi utafanywa
kwa kila ngazi ya utumishi ndani ya Shirika na kuchukua hatua stahiki
zinazotokana na matokeo. Tuzo kwa matokeo mazuri na hatua za kinidhamu kwa
matokeo mabaya.
11.0 HITIMISHO
Ndugu
Mwenyekiti,
11.1 Wote tunafahamu kuwa Shirika hili la
Posta Tanzania ni chombo cha Muungano wetu wa Tanzania Bara na Visiwani. Mwezi Januari mwakani nchi ya Zanzibar
itaadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi na mwezi Aprili mwakani tutaadhimisha miaka
50 ya Muungano wetu. Ni jambo la
kujivunia kuwa Shirika hili mmeliendesha vyema ndani ya Muungano huu ambapo shughuli
zake sio sehemu ya kero za Muungano.
Nawapongeza sana.
11.2 Mkutano huu umefanyika wakati Shirika
la Posta Tanzania linaelekea kutimiza miaka 20 tangu lilipoanza kazi mwezi
Januari mwaka 1994. Ilikuwa ni safari
ndefu yenye mafanikio na changamoto. Mafanikio myaendeleze na changamoto
mzifanyie kazi.
11.3 Aidha, nawapongeza kwa uamuzi wenu wa
kubuni Mpango Kabambe wa miaka kumi (Master Plan 2014/2023) na Mpango Mkakati
wa miaka mitano (Strategic Business Plan 2014/2018). Aidha, ni muhimu Uongozi
wa Shirika uwasilishe Wizarani kwangu nakala ya mipango hiyo baada ya kuridhiwa
na Bodi yenu ili tuweze kufuatilia utekelezaji wake.
11.4 Ni mategemeo yangu kuwa baada ya
mkutano huu mtaondoka hapa mkiwa manahodha bora zaidi wa kuongoza vyema shughuli
za Shirika hili hadi kufikia shabaha na malengo ya kuanzishwa kwake.
11.5 Ni lazima mtambue na kuzingatia kuwa
wadau wote wa Shirika hili wanawategemea ninyi viongozi. Msiwaangushe.
Baada ya
kuyasema haya, sasa natamka kuwa
Mkutano huu wa 22 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania umefunguliwa
rasmi.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Imetolewa na:-
MHE. WAZIRI WA MAWASILIANO,
SAYANSI NA TEKNOLOJIA
DAR ES SALAAM
Novemba, 2013
Picha ya pamoja na Waziri Makame Mbarawe (wa tatu kutoka kushoto waliokaa) na wajumbe wa mkutano huo. Kulia kwake ni Postamasta Mkuu Deos Mndeme.
No comments:
Post a Comment