Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mh. Mizengo Kayanza Peter Pinda kesho tarehe 29, Novemba 2013
anatarajia kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Tovuti Kuu ya Serikali katika
Ukumbi wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
Uzinduzi wa Tovuti Kuu hiyo
inayopatikana kwa anuani ya www.tanzania.go.tz utahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa
Serikali, Wananchi, Wafanyabiashara, Washirika wa Maendeleo, Taasisi zisizo za
Serikali na Wawakilishi kutoka vyuo Vikuu.
Tovuti Kuu hiyo ni mojawapo ya
juhudi za Serikali katika kuhakikisha kuwa taarifa na huduma zinazotolewa na
Serikali zinapatikana na kuwafikia wananchi kwa urahisi, wakati wowote na
mahali popote ndani na nje ya nchi. Tovuti Kuu hiyo pia ni moja ya mafanikio
makubwa katika kutimiza dira ya muda mrefu ya kuwa na dirisha moja linalotoa
taarifa na huduma zinazotolewa na Taasisi za Serikali kwa urahisi.
Taarifa na huduma katika Tovuti Kuu
hiyozimegawanywa katika maeneo makuu sita ya ambayo ni Serikali, Wananchi, Taifa
letu, biashara, Sekta na Mambo ya Nje inalenga kutoa huduma mbalimbali kama
upatikanaji wa nyaraka zote za Serikali, huduma zinazotolewa na Serikali kwa
njia ya simu na mtandao, Viwango vya fedha, Hali ya Hewa, na Soko la Hisa.
Huduma nyingine katika Tovuti Kuu
hiyo imetengwa katika ukarasa wa Nifanyeje? ambao unamjengea uwezo mwananchi wa
kufahamu taratibu za upatikanaji wa huduma zinazotolewa na taasisi mbali mbali
za Serikali kama nifanyeje kupata pasipoti, kibali cha kazi, TIN, Cheti cha
kuzaliwa na mikopo ya chuo.
Aidha tovuti hiyo pia inalenga
kuziunganisha Tovuti na mifumo ya Taasisi mbali mbali inayotoa taarifa na huduma
kwa wananchi na wafanyabiashara katika dirisha moja.
Tovuti Kuu hiyo ilianza kutengenezwa
mwaka 2009 na kupatikana kwa anuani ya www.egov.go.tz chini ya Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Tovuti hiyo iliboreshwa na kuunganishwa na
iliyokuwa Tovuti ya Taifa kwa anuani ya www.tanzania.go.tz mwaka 2012 chini ya
Wakala ya Serikali Mtandao.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI
(MAELEZO)
28/11/2013, DAR ES
SALAAM.
No comments:
Post a Comment