Mahakama ya kijeshi nchini Misri imetoa hukumu ya vifungo vya muda mrefu jela kwa wafuasi wa Rais aliyepinduliwa Mohammed Morsi.
Watu hao walihukumiwa baada ya kupatikana na hatia ya kushambulia wanajeshi.
Mmoja wa washukiwa alifungwa jela maisha, wengine watatu wakipewa vifungo vya kati ya miaka 5, 15 na 45, kwa mujibu wa taarifa za jeshi.
Walishtakiwa kwa kuwafyatulia risasi wanajeshi wakati wa ghasia na vurugu katika mji wa bandarini wa Suez mwezi jana.
Vurugu hizo zilitokea baada ya msako mkali uliofanywa na maafisa wa usalama dhidi ya wafuasi wa Moris waliokuwa wamepiga kambi mjini Cairo.
Mamia ya watu, wengi wao wanachama wa vuguvugu la Muslim Brotherhood, waliuawa wakati wafuasi wa Morsi walipokuwa wamepiga kambi nje ya msikiti wa Rabaa al-Adawiya na katika medani ya Nahda wakitaka Morsi aachiliwe, ingawa waliondolewa kwenye kambi hizo tarehe 14 mwezi Agosti.
Vurugu zilizotokea mjini Suez, Mashariki mwa Cairo, kati ya tarehe 14 na 16 mwezi Agosti zilisababisha vifo vya zaidi ya watu 30.
Hata hivyo haijulikani ikiwa wale waliohukumiwa Jumanne ni wanachama wa Brotherhood. Lakini ikiwa ni wanachama wa vuguvugu hilo, hukumu walizopewa bila shaka zitaathiri sana chama hicho hasa ikizingatiwa ni za kwanza kutolewa kwa vugu vugu hilo tangu kuondolewa mamlakani kwa Morsi.
Viongozi wa mashtaka walitangaza tarehe 1 Septemba miezi miwili baada ya kuzuiliwa kwa Morsi kuwa anatufunguliwa mashtaka kwa kuchochea mauaji.
No comments:
Post a Comment