Kamishna Msaidizi wa Ujenzi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Bw. Nathan Alute akitoa ufafanuzi Teknolojia mpya ya Ujenzi wa nyumba zenye gharama nafuu(UBM), kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo ukumbi wa Idara ya Habari kulia ni Msemaji wa Wizara hiyo Lt. Kanali Juma Sipe.
Meneja Mradi wa UBM Raphael Bandiho (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa Habari Kuhusu ubora wa nyumba zinazotokana na teknolojia hiyo, kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo ukumbi wa Idara ya Habari kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Bi. Zamaradi Kawawa.
WIZARA ya Ulinzi na Jeshi
la Kujenga Taifa imeanzisha matumizi ya teknolojia mpya ya ujenzi ijulikanayo
kama “Ultimate Building Machine (UBM)”, inayowezesha ujenzi kufanyika haraka na
katika hali yoyote ya maumbile ya nchi.
Teknolojia
ya UBM ilianza kutumika nchini kwa majaribio katika kambi za Jeshi Mgulani, Dar
es Salaamu. Hatimaye Wizara iliridhia teknolojia hiyo kutumika katika ujenzi
mkubwa wa Shule ya Mafunzo ya Awali, Kihangaiko (Msata), Mkoani Pwani katika
mwaka wa Fedha 2012/13. Pamoja na ufinyu mkubwa wa fedha kutoka Serikalini, UBM
imewezesha hatua kubwa kupigwa katika ujenzi huo muhimu.
UBM ni mtambo wa ujenzi unaotembezwa juu ya gari maalumu. Mtambo huu
ambao hutumia kompyuta unaweza kuendeshwa kwa urahisi na kwa ufanisi,
husafirishwa moja kwa moja hadi eneo la ujenzi kwa kutumia lori maalumu au
ndege ya mizigo ili kuwezesha ujenzi wa haraka wakati wa majanga.
Faida za teknolojia ya UBM ni pamoja na kuwezesha ujenzi
wa haraka (Rapidity) kutokana na uwezo wa mtambo kutengeneza/ kuzalisha maumbo
mbali mbali ya mabati katika mitindo tofauti tofauti pale pale kwenye eneo la
ujenzi, urahisi na uharaka wa uunganishaji wa maumbo kiasi cha kuwezesha watu
10-12 kukamilisha jengo moja lenye futi za mraba 10,000 ndani ya siku moja
(endapo msingi wake uko tayari) na kupunguza muda wa ujenzi kwa kuwa teknolojia
hii haihitaji nguzo za kushikiza (columns), vishikio (Screws, panels, beams,
trusses, nuts, bolts, fasteners), misumari (screws), wala gundi maalumu ya
kuzuia kuvuja (sealants).
Faida nyingine ni kupatikana kwa “thamani
ya fedha” (Cost-Effectiveness) kwani gharama za ujenzi ni kati ya asilimia 40
na 60 ya ujenzi wa kawaida au teknolojia ya “prefabricated” kutokana na
kupunguza idadi ya wajenzi na usimamizi wa wahandisi wanaohitajika kwa
teknolojia ya kawaida. Aidha, teknolojia inarahisisha pia usafirishaji wa
Mtambo na Vifaa kwani matumizi ya “Galvanized,
Pre-painted Steel Coil” yanapunguza hadi asilimia 80 ya mahitaji ya vifaa.
Mjenzi anaweza kunufaika pia na ujenzi
wa maumbo mbali mbali (Flexible designs) kutokana na mtambo wa UBM kuwa na uwezo
wa kuzalisha maumbo mbali mbali ya mabati katika
mitindo tofauti tofauti kulingana na hitajio la mwenye nyumba. Umbo, muonekano,
kimo na upana wa jengo pia hutofautiana kulingana na mahitaji, na bado jengo
likabaki na uwezekano wa kupanuliwa siku za usoni.
Majengo ya teknolojia ya UBM yana faida pia ya maisha
marefu na gharama ndogo za matengenezo (Durable and Low
Maintenance cost) kutokana na umadhubuti wa mabati yanayotumika na uwezo wake
wa kuhimili mikikimikiki ya kimbunga, tetemeko la ardhi, moto na upepo
mkali.
Tafiti duniani zinaonesha kuwa teknologia ya
UBM inakubalika kuwa ya kiwango cha juu kiusalama kimataifa ikiwemo kukidhi
viwango vya Jumuiya ya Ulaya (European CE compliance). Teknolojia ya UBM imethibitika pia kuwa si kwa ajili
ya ujenzi wa haraka wakati wa majanga tu, bali inaweza kulisaidia Taifa
kukamilisha ujenzi wa aina mbali mbali kwa haraka na kwa gharama nafuu ili
kuleta manufaa haraka.
Kuridhia
kwa Serikali na Taasisi binafsi kutumia teknolojia hii kutaifanya UBM kuwa
mkombozi katika ujenzi wa maabara na mabweni mashuleni, ujenzi wa maghala ya
mazao katika maeneo mbali mbali ya uzalishaji nchini, pamoja na aina yoyoye
nyingine ya ujenzi wa haraka kwa kadri mmiliki wa jengo atakavyohitaji na
watakavyokubaliana na wataalamu wa Wizara ya Ulinzi na JKT.
Teknolojia ya Ultimate Building Machine
(UBM) iliyoasisiwa na Kampuni ya MIC Industries,
Inc. ya nchini Marekani na baadae kuenea hadi
barani Ulaya na Asia. SUMAJKT wamepewa dhamana ya kutumia teknolojia hiyo
nchini.
Imeandaliwa
na kutolewa na Luteni Kanali Juma Nkangaa Sipe,
Msemaji,
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,
No comments:
Post a Comment