TANGAZO


Monday, July 29, 2013

TRA yauelezea Mfumo mpya wa kulipa ada za mwaka za magari kwa njia ya mtandao

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) Bw. Richard Kayombo (kulia) akieleza kwa waandishi wa habari kuhusu mfumo mpya wa ulipaji kodi za magari kwa njia ya mtandao, kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo ukumbi wa Idara ya Habari kushoto ni Meneja wa Mradi wa Mamlaka hiyo Bw. Ramadhani Sengali.
Kaimu Meneja Magari kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) Bw. Julius Mchihiyo (kulia)akitoa ufafanuzi juu ya utekelezaji wa mfumo mpya wa ulipaji kodi za magari kwa njia ya mtandao, kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo ukumbi wa Idara ya Habari kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Bi. Zamaradi Kawawa.

Meneja wa Mradi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Ramadhani Sengali akijibu swali la waandishi wa habari waliotaka kujua jinsi gani mfumo huo utaleta tija hasa katika ukususanyaji wa kodi, kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo ukumbi wa Idara ya Habari, kulia ni Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka Mamlaka hiyo Bw. Richard Kayombo. (Picha zote na Hassan Silayo, Maelezo) 



KUANZIA mwezi Agosti 2013 malipo yote ya ada za mwaka za magari (annual road license) yatafanywa kwa njia ya mtandao kwa maana ya kutumia simu za kiganjani, benki na wakala wa Maxmalipo.

Hii inatokana na maboresho ya mifumo ya kielektroniki ambayo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea kuyafanya ikiwa ni juhudi za kutoa huduma bora kwa walipakodi na kuhakikisha kuwa mapato ya Serikali yanayokusanywa na yanawasilishwa kwa wakati kwenye mfuko mkuu wa Serikali, Benki Kuu.
Mfumo huu utatumika kulipa ada za mwaka za magari ambapo mlipakodi anaweza kupata taarifa ya kiasi cha kodi anachotakiwa kulipa.

Faida za mfumo.
Mfumo huu umeanzishwa kutokana na faida nyingi kama:
·      Mfumo huu ni rahisi kutumia na utapunguza misongamano isiyo ya lazima katika ofisi za Mamlaka ya Mapato na benki na hivyo kumwezesha mlipakodi kulipa ada ya gari lake akiwa mahali popote nchini.

·      Mfumo huu una panua wigo wa njia za kulipa kodi kwahiyo unampa mlipakodi uhuru wa kuchagua njia ambayo anaona ni rahisi kutumia kutokana na mazingira atakayo kuwamo.

·      Vilevile kwa kutumia utaratibu huu mlipakodi anaweza kuhakiki kiwango cha ada ya gari anachotakiwa kulipa na hivyo kuepuka udanganyifu unaofanywa na vishoka ambao huwarubuni wananchi kwa kuwapa taarifa za viwango vya ada za magari visivyo sahihi.

·      Mfumo huu ni salama kwani kuna uhakika kwamba malipo yote ya kodi yanakwenda Benki Kuu kwani unaondoa mwingiliano wa wafanyakazi wa TRA na walipakodi.
·      Kwa upande mwingine mfumo huu unaiwezesha TRA kukusanya kodi kwa gharama nafuu.

Utaratibu wa kutumia mtandao kulipa ada za magari ni kama ifuatavyo:
1.    Kufahamu kiwango cha kodi. Tuma ujumbe wenye neno “Kadiria” au “Assess” acha nafasi andika namba za  gari mfano KADIRIA T171AUC kwenda namba 15341.  
2.    Kulipa: Tuma ujumbe wenye neno; “sajili” acha nafasi na kuandika namba ya gari husika. Tuma ujumbe huo kwenda namba 15341. Baada ya hapo mlipakodi atapata ujumbe wa namba ya kumbukumbu ya malipo (Reference number).
3.    Fanya malipo kwa kutumia TIGOPESA, MPESA, AIRTELMONEY au wakala wa MAXMALIPO kwa kutumia namba ya kumbukumbu uliyopata.
4.    Kuchukua cheti: (sticker ya gari): nenda katika ofisi yoyote ya TRA ukiwa na namba ya kumbukumbu uliyoitumia kufanya malipo.

Zingatia.
Ili kuweza kuchukua kadi ya gari mlipakodi anatakiwa kuwa na kitambulisho chochote kama vile kitambulisho cha Taifa, Hati ya kusafiria, Lesseni ya udereva, Kitambulisho cha mpiga kura n.k.

Mfumo wa kulipa ada za magari za mwaka ni muendelezo wa maboresho ya mfumo wa kulipa kodi kwa mtandao (Revenue Gateway)  ambao ulibuniwa na TRA kwa kushirikiana na Benki Kuu (BOT). Mfumo huu umeanza kutumika rasmi Julai Mosi 2013.
Mfumo wa RG pamoja na kuwa unaunganisha mifumo ya TRA na Benki Kuu pia unaiunganisha TRA na walipakodi, Benki za Biashara, Makampuni ya simu (M-PESA, TIGOPESA, AIRTELMONEY n.k) pamoja na wadau wengine kama vile Hazina na NIDA.
Wito.
Tunatoa wito kwa wananchi wote kuungana na TRA katika maboresho ya mifumo yanayoendelea kwa kuitumia mifumo hiyo kwani imewekwa kwa ajili yao ili waweze kulipa kodi stahiki bila usumbufu wowote.
Pia tunawaomba wananchi wote wanaolipa ada mbalimbali za magari kuitumia fursa hii ya kulipa kwa njia ya mtandao ili waweze kuendelea vema na shughuli za ujenzi wa taifa badala ya kutumia muda mwingi katika misurusu kwenye mabenki.
 PAMOJA TUNAJENGA TAIFA LETU
RICHARD M. KAYOMBO
MKURUGENZI WA HUDUMA NA ELIMU KWA MLIPAKODI
MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA


No comments:

Post a Comment