TANGAZO


Monday, July 29, 2013

Mali yapongezwa kwa uchaguzi mkuu


Wapiga kura kwenye foleni Mali
Uchaguzi mkuu wa Urais nchini Mali umesifiwa kwa ambavyo ulifanywa. Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, amesema kuwa wapiga kura wengi walijitokeza kupiga kura wakati wachunguzi kutoka barani Ulaya wakisema kuwa uchaguzi wenyewe umefanyika bila vurugu.
Hata hivyo idadi ya waliopiga kura katika eneo la Kaskazini ilikuwa chini ikilinganishwa na maeneo mengine ya nchi.
Wapiganaji wa kiisilamu waliteka eneo la Kaskazini mwa nchi kabla ya wanajeshi wa Ufaransa kuja nchini humo kusaidia na harakati za kuwafurusha wapiganaji hao wakisaidiwa na wanajeshi wa Muungano wa Afrika.
Kura zimeanza kuhesabiwa katika uchaguzi wa urais ambao unatarajiwa kulianzisha upya taifa hilo kufuatia mapinduzi ya kijeshi mwaka uliopita.
Wadadisi wanasema huenda kukawa na duuru ya pili ya uchaguzi huo.
Wachunguzi wameelezea kuwa wapiga kura walijitokeza kwa wingi katika mji mkuu wa Bamako pamoja na maeneo mengine ya Kusini mwa taifa hilo.
Mwandishi wa habari wa BBC nchini humo amesema kuwa wengi wa wapiga kura walitaka vidole vyao kutotiwa wino.
Amesema waasi wa Tuareg ambao wanadhibiti eneo kubwa la Kaskazini wamepinga uchaguzi huo licha ya kukubali shughuli hiyo kuendelea.
Wagombea 27 walishiriki kwenye uchaguzi huo na ikiwa hapatakuwa na mshindi bayana huenda duru ya pili ikafanyika tarehe 11 mwezi Agosti.
Hata hivyo wachanganuzi wamekuwa wakihoji ikiwa nchi hiyo iko tayari kwa uchaguzi.
Takriban watu milioni 6.8 walikuwa na uwezo wa kupiga kura katika vituo 21,000 kote nchini.

No comments:

Post a Comment