TANGAZO


Wednesday, July 31, 2013

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi yatoa taarifa kuhusu mafaniko ya Serikali katika kuwarejesha makwao wakimbizi waliokuwa wamehifadhiwa kwenye makambi nchini

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isack Nantanga akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, kuhusu Maofisa Magereza waliofukuzwa kazi baada ya  kukamatwa  na nyara za serikali.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Isack Nantanga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio ya  Serikali katika zoezi la kuwarejesha katika nchi zao wakimbizi waliokuwa wamehifadhiwa hapa nchini. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Zamaradi Kawawa. (Picha zote na Frank Mvungi-Maelezo)

NDUGU waandishi wa Habari, kwanza kabisa napenda kuwashukuru kwa kuhudhuria kikao hiki na leo nitaelezea mafanikio yaliyofikiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika kufanikisha zoezi la kuwarejesha kwao kwa hiari wakimbizi waliokuwa hapa nchini.
1. Historia ya uwepo wa wakimbizi hapa nchini inaanzia miaka ya kabla na baada ya uhuru mwaka 1961 lakini ujio mkubwa wa wakimbizi ulianzia miaka ya 1970 ambapo hadi kufikia mwaka 1995 idadi ya wakimbizi hao ilifikia zaidi ya milioni moja.  Idadi kubwa ya wakimbizi hawa walitokea katika nchi za Maziwa Makuu, hususan Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)  kutokana na machafuko katika nchi zao.

Kutokana na wingi wao wakimbizi hawa walihifadhiwa katika makambi mbalimbali ambapo kwa msaada wa Jumuiya ya Kimataifa kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) waliweza kupatiwa huduma zote muhimu za chakula, afya na elimu.
Hata hivyo, wakimbizi wa Rwanda ambao wote walikuwa wamehifadhiwa katika mkoa wa Kagera walirejea kwao mwaka 1996/1997.

Wakimbizi waliobaki kutoka nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) waliendelea kuhifadhiwa katika makambi yaliyokuwa mkoani Katavi na Kigoma.

2. Zoezi la kuwarejesha kwao wakimbizi wa Burundi na DRC waliokuwa hapa nchini:
                   
Baada ya kuona kuwa hali ya usalama imerejea katika nchi za Maziwa Makuu ambazo bado zilikuwa na raia wao hapa nchini, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), mwaka 2002, ilianzisha zoezi la kuwarejesha kwao kwa hiari wakimbizi wa Burundi waliokuwa hapa nchini.  
Idadi ya wakimbizi waliorejeshwa kwao tangu zoezi hilo lianze  mwezi Machi mwaka 2002 hadi kufikia mwanzoni mwa mwaka huu ni 502,358.  Zoezi kama hilo lilianza kutekelezwa kwa wakimbizi wa DRC mwaka 2005 ambapo wakimbizi wapatao 66,660 walirejeshwa kwao toka kwenye makambi yaliyokuwa mkoani Kigoma.
3.  Kufungwa kwa Kambi za wakimbizi: Kutokana na mafanikio yaliyopatikana ya kuwarejesha kwao wakimbizi hawa, jumla ya kambi 12 kati ya 13 za wakimbizi zilizokuwa hapa nchini zilifungwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2007 hadi 2013.  Kambi hizo ni:
      i.        Muyovosi iliyokuwa wilayani Kasulu mkoani Kigoma iliyokuwa ikihifadhi wakimbizi toka Burundi.
    ii.        Mkugwa iliyokuwa  wilayani Kibondo mkoani Kigoma iliyokuwa ikihifadhi wakimbizi mchanganyiko kutoka nchi mbalimbali.
   iii.        Lukole A katika wilaya ya Ngara mkoani Kagera iliyokuwa ikihifadhi wakimbizi mchanganyiko.
   iv.        Lukole B katika wilaya   ya Ngara mkoani Kagera iliyokuwa inahifadhi wakimbizi kutoka Burundi.
    v.        Lugufu I iliyokuwa wilayani  Kigoma Vijijini iliyokuwa  ikihifadhi wakimbizi toka Jamhuriya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
   vi.        Lugufu II iliyokuwa wilayani Kigoma Vijijini iliyokuwa ikihifadhi wakimbizi toka DRC.
  vii.        Mtendeli iliyokuwa wilayani Kibondo mkoani Kigoma iliyokuwa ikihifadhi wakimbizi wa Burundi.
viii.        Kanembwa iliyokuwa wilayani Kibondo mkoani Kigoma iliyokuwa ikihifadhi wakimbizi wa Burundi.
   ix.        Nduta iliyokuwa wilayani Kibondo mkoani Kigoma iliyokuwa ikihifadhi wakimbizi wa Burundi.
    x.        Karago iliyokuwa wilayani  Kibondo mkoani Kigoma iliyokuwa ikihifadhi wakimbizi wa Burundi.
   xi.        Kitali iliyokuwa wilayani  Ngara mkoani Kagera iliyokuwa, awali, ikihifadhi wakimbizi toka Rwanda na baadaye wakimbizi toka Burundi.
  xii.        Mtabila iliyokuwa wilayani Kasulu mkoani Kigoma, iliyokuwa ikihifadhi wakimbizi toka Burundi.  Zoezi la kuwarejesha kwao wakimbizi waliokuwa katika kambi hii lilikamilika mwishoni mwa mwaka jana na imekabidhiwa rasmi kwa Serikali ya Tanzania Jumatatu iliyopita, tarehe 22 Julai, 2013.

Kambi pekee ya wakimbizi ambayo imebaki ni ya Nyarugusu ambayo iko wilayani Kasulu mkoani Kigoma inayohifadhi wakimbizi kutoka DRC (63,728) na kutoka Burundi  (4,153) na nchi nyingine za Kiafrika (212).

4.   Wakimbizi wengine walioko katika Makazi:
Licha ya wakimbizi waliokuwa kwenye makambi, pia wapo wengine ambao wapo katikamakazi. Jumla ya wakimbizi 173,763 wako katika makazi ya wakimbizi ya Mishamo na Katumba wilayani Mpanda mkoani Katavi, na Ulyankulu mkoani Tabora. Kwa sasa Serikali iko katika mchakato wa kuwatafutia suluhisho la kudumu wakimbizi hawa ambao waliingia nchini katika miaka ya 1970 na walipewa makazi hayo ambapo walikuwa wanajitegemea.

Aidha wakimbizi wengine 2,117 kutoka Somalia ambao wana asili ya Kibantu wako katikamakazi ya Chogo mkoani Tanga ambapo nao utaratibu unafanywa wa kutafuta suluhisho la kudumu la uwepo wao hapa nchini.  Wakimbizi hawa toka Somalia ambao wana asili ya Tanga, waliingia nchini miaka ya 1990 baada ya kuzuka kwa machafuko katika nchi yao.

5.  Wakimbizi waliohamishiwa katika Nchi ya Tatu: Pale ambapo wakimbizi hawawezi kurejeshwa kwao au kupewa uraia, ufumbuzi mwingine ni kuwapeleka nchi nyingine mwanachama wa Umoja wa Mataifa.  Hadi sasa kiasi cha wakimbizi 14,000 wa Burundi wamepelekwa na wanaishi nchini Marekani.

Lengo la Serikali ni kuona kuwa suala la kuhifadhi wakimbizi hapa nchini linafikia tamati na juhudi zinaendelea kuona kuwa hata Kambi ya Nyarugusu ambayo ndio kambi pekee iliyobaki inafungwa baada ya wakimbizi walio katika kambi hiyo kurejeshwa kwao, pale hali ya usalama nchini DRC itakapokuwa imeimarika.

Pamoja na kutoa nafasi kwa Serikali na wananchi kutumia kwa shughuli nyingine za kimaendeleo maeneo makubwa yaliyotengwa kuhifadhi wakimbizi, kuondoka kwao pia kunatoa nafasi nzuri ya kuweza kukabiliana na changamoto za kiusalama katika maeneo hayo ambayo yapo katika mikoa ya mpakani mwa nchi.

Aidha, kutasaidia pia kupunguza msongo katika maeneo hayo ambao ulichangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta uharibifu wa mazingira na uvunaji holela wa rasilimali katika maeneo ya misitu na hifadhi za taifa.
6. SHUKRANI:
Serikali ya Tanzania inapenda kuishukuru Jumuiya ya Kimataifa kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), kwa misaada ya hali na mali waliyotoa na wanayoendelea kutoa kusaidia hifadhi ya wakimbizi hapa nchini. 

Pia inapenda kuwashukuru Watanzania wote na hasa wale wa Mikoa ya Katavi, Kigoma na Kagera kwa ushirikiano wao waliotoa kwa wakimbizi waliokuwa wamehifadhiwa katika maeneo yao, na nchi za Burundi, Congo na Rwanda kwa ushirikiano wao uliowezesha kuwarejesha raia wao waliokuwa wamehifadhiwa hapa nchini.

Mashirika mengine ambayo pia yalihusika na yanaendelea kutoa huduma za kibinaadamu kwa wakimbizi ni pamoja na Shirika la Chakula Duniani (WFP), Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF), Kamati ya Kimataifa ya Uokozi (IRC), na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS).
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment