Na Beatrice Mlyansi, Maelezo
WAJASIRIAMALI nchini pamoja na vijana wameshauriwa kutumia fursa mbalimbali za maonyesho ya bidhaa za wajasiriamali katika kutangaza Biashara zao pamoja na kutengeneza fursa ya kupata masoko ya kudumu ya bidhaa wanazozalisha kwa lengo la kujiajiri, kujiongezea kipato na kukua kibiashara
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Kampuni ya African Centre for Business Consultancy (ACBC Consultancy) Bw.Rashid Adam wakati akizungumzia maonyesho yajulikanayo kama “Free Marketing Zone Exhibition” yatakayofanyika katika Viwanja vya Nyerere (Nyerere Square) Mkoani Dodoma kuanzia tarehe 31 Agosti hadi 6 Septemba 2013.
Bw. Adam amesema kuwa maonyesho ya Free Marketing Zone yamelenga zaidi kuwatafutia masoko ya kudumu wajasiriliamali mbalimbali pamoja na makampuni yatakayoshiriki kwa lengo la kukuza biashara zao pamoja na kuwakutanisha wajasiriamali na makampuni tofauti ambapo watabadilishana uzoefu na fursa mbalimbali za kibiashara
Aidha Mkurugenzi huyo amesema kuwa wajasiriamali wengi wanatengeneza bidhaa nzuri lakini wanakosa masoko ya uhakika kutokana na bidhaa zao kutojulikana kwa walaji .
“Wajasiriamali wengi wanatengeneza bidhaa nzuri ,nyingine ukiziona huwezi amini kama zinatengenezwa nchini lakini wanashindwa kuuza bidhaa hizo kutokana na kukosa wateja na masoko kwa kutojulikana kwa bidhaa hizo .na wateja.”alisema Bw.Adam
Bw.Adam amewakaribisha wananchi na wajasiriamali kushiriki katika Maonyesho hayo ili wapate fursa ya kukutana na watu tofauti wenye ujuzi na mawazo tofauti yatakayosaidia kuboresha huduma na bidhaa wanazozalisha,vilevile kuwawezesha wateja kuwajua na kupata bidhaa hizo moja kwa moja.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa wajasiriamali watakaoshiriki watapewa vyeti vya ushiriki pamoja na nafasi ya kutangaza biashara zao katika jarida litakalokuwa na anuani za washiriki wote, zikionesha biashara zao na sehemu wanapopatikana ili wateja waweze kuwafiki kiurahisi baada ya maonyesho hayo pamoja na kuwatangaza zaidi kibiashara.
Bw. Adam amewakaribisha wajasiriamali wote wanaopenda kushiriki maonyesho hayo ya Free Marketing Zone Exhibition ili waweze kuwafikia kiurahisi wateja wao na kutanua wigo wa masoko kwa bidhaa zao, huduma zao na Biashara zao.
Kwa kampuni na wajasiriamali wanaopenda kushiriki katika maonyesho ya Free Marketing Zone Exhibition wanaweza kuwasiliana na African Centre for Business Consultancy kupitia barua pepe acbc.consultancy@gmail.com au kwa simu namba 0655141185, 0713966552.
No comments:
Post a Comment