TANGAZO


Wednesday, July 31, 2013

EWURA yaja na rai mpya kuhusu ukandarai wa Umeme nchini


Meneja Mawasiliano na Uhusiano  wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Titus Kaguo, akizungumza na waandishi wa habari leo, jijini Dar es Salaam kuhusu  utaratibu wa kuwa na leseni  ya uwekaji umeme (electrical installation licence), ili kuhakikisha ufungaji wa mifumo ya umeme unafanywa na watu wenye ujuzi wa kutosha wa fani hiyo. 
Meneja Mawasiliano na Uhusiano  wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Titus Kaguo, akizungumza na waandishi wa habari leo, jijini Dar es Salaam kuhusu  utaratibu wa kuwa na leseni  ya uwekaji umeme (electrical installation licence), ili kuhakikisha ufungaji wa mifumo ya umeme unafanywa na watu wenye ujuzi wa kutosha wa fani hiyo. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari, Bi. Zamaradi Kawawa. (Picha zote na Frank Mvungi-Maelezo)


MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeundwa chini ya sheria ya EWURA, sura namba 414 ya Sheria za Tanzania. EWURA ina majukumu ya kusimamia shughuli za udhibiti, kiufundi na kiuchumi  katika sekta Nne (4)  za Petroli, Umeme, Gasi Asili na Maji Safi na Maji Taka.
Miongoni mwa shughuli ambazo zinadhibitiwa na EWURA chini ya Sheria ya sasa ya Umeme ya mwaka 2008, Sura ya 131,ni pamoja na kutoa leseni za umeme kwa ajili ya uzalishaji, usafirishaji, usambazaji, ugavi na utandazaji wa nyaya (electrical installation). Hapo awali kazi hii  ilikuwa ikifanywa na Wizara ya Nishati na Madini; na mwaka 2008 EWURA ilikabidhiwa kazi hiyo rasmi.
Tanzania inaelelekea kwenye mfumo wa uchumi wa kati, ambapo kumekuwapo na miradi  mingi  ya maendeleo inayohitaji miundo mbinu ya umeme.  Miundombinu hii mipya;  kama vile majengo makubwa na viwanda inahitaji  misongo mbalimbali ya umeme.  Kutokana na hali hiyo  kunahitajika uwapo wa  wakandarasi bora kuanzia kiwango cha mafundi wenye madaraja ya chini (waliomaliza VETA) , mafundi wa  kati (Mafundi mchundo na wale wenye vyeti vya NACTE/ Diploma) na  Wahandisi kwa ajili ya uwekaji umeme kwenye miradi hiyo.
Kwa mfano,  miaka ya nyuma Dar es Salaam  peke yake haikuwa hivi, Karikoo yenyewe magorofa yalikuwa ya kuhesabika, leo hii majengo mengi yamejengwa, na bila shaka kazi nyingi za umeme kwenye magorofa haya zimefanywa na mafundi kutoka VETA , vyuo vikuu, na taasisi nyingine za ufundi hapa nchini,  wengine wakiwa na leseni na wengine wakiwa  hawana kabisa.
Kuanzia mwaka 2007 hadi  Juni 2013 taarifa  ya malalamiko ya wateja waliofika EWURA kutoa taarifa za  ajali za moto kwenye nyumba zao na za biashara ni 214. Haya ni matukio mengi ambayo yameleta hasara kwa jamii.
Madhumuni ya kuwa na leseni  ya uwekaji umeme (electrical installation licence) ni kuhakikisha kwamba, ufungaji wa mifumo ya umeme inafanywa na watu wenye ujuzi wa kutosha wa fani hiyo ili,pamoja na mambo mengine:
1.                Kupunguza upotevu wa umeme kutokana na ufungaji wa nyaya usiofuata kanuni za kitaalamu wa umeme;
2.                 Kupunguza matukio ya ajali za moto zitokanazo na mifumo mibovu ya umeme inayofanywa na watu  wasio na  utaalam stahiki , au  “ Vishoka”  kama inavyojulikana TANESCO;
3.                Kuwa na orodha ya watu wote wanaofanya kazi za umeme nchini ili kusaidia EWURA kufuatilia malalamiko ya wananchi kuhusu makandarasi wa umeme wanaofanya kazi mbaya za umeme ili hatua kali zichukuliwe dhidi yao; 
4.                Kwa kushirikiana na TANESCO  kubaini fundi mwenye leseni ya umeme kutoka EWURA , aliyefanya kazi mbaya katika  miradi mbalimbali ili hatua stahiki  zichukuliwe dhidi yake; na
5.                Kuhakikisha Kampuni za ukandarasi zinaajiri watu walio na utaalamu kulingana na ngazi na aina ya kazi wanayotakiwa kufanya.
Leseni zinatolewa na EWURA zipo katika madaraja saba , daraja A, B,C, D , E, F, na  Wiremen (mafundi wa waya wa mwisho). Daraja A , ndilo daraja la juu kabisa ambalo hutolewa kwa wenye mafunzo ya ufundi ngazi ya mafundi mchundo (FTC)  hadi ngazi ya uhandisi,  na daraja la ‘Wireman “ ni la kiwango cha chini kabisa  linatolewa kwa mafundi  wenye elimu kuanzia  kiwango cha daraja la tatu  kutoka VETA au taasisi nyingine ya kiwango hicho. Daraja la ‘E’ ni la wale wanaofanya kazi maalum katika fani ya umeme, mfano mafundi wanaoshughulika na umeme utokanao na jua, usukaji wa mashine mbalimbali za umeme. 
Tangu mwaka 2008 , EWURA imeweza kutoa leseni  840 kwa mafundi na wahandisi mbalimbali ,  kati ya hizo zikiwa ni maombi mapya na nyingine zikiwa ni ubadilishaji wa leseni za zamani zilizokuwa zinatolewa na Wizara ya Nishati na Madini na kubadilishwa kuwa  leseni mpya za EWURA .
Daraja la A zimeshatolewa leseni 66, Daraja B zimetolewa leseni 167, Daraja C zimetolewa leseni 303, Daraja D zimetolewa leseni 187, Daraja Wiremen zimetolewa leseni 116 na  Daraja F  leseni moja (1).
Katika kutekeleza maombi ya utoaji wa leseni za umeme, EWURA huzingatia vigezo  vifuatavyo:
1.                Vigezo vya elimu na ujuzi alionao mwombaji huangaliwa kwa makini wakati wa tathmini;
2.                Mapendekezo ya  kimaandishi anayotoa  shahidi wa mwombaji  wa leseni, inayomwezesha kumsimamia kazi mwombaji wa leseni yanatiliwa maanani;
3.                Endapo kutaonekana jambo lolote linalotia shaka kuhusu taarifa zilizopokelewa kuhusu maombi ya leseni, basi ataitwa kwenye usaili; na
4.                Maombi yatakayokidhi vigezo vya leseni husika yatapelekwa kwenye Bodi kwa ajili ya kuidhinisha maamuzi ya kupewa leseni husika; kwa wale watakaokatiliwa maombi yao, Bodi hutoa maelekezo ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa, na mwombaji huarifiwa.
Ili kufanikisha shughuli hii EWURA imekuwa ikishirikiana na  vyombo vinavyoshughulikia sekta hii ya umeme, ikiwa ni  pamoja na TANESCO, Bodi ya Usajili ya Makandarasi (CRB),  Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), na Shirika la Viwango Tanzania (TBS)  katika kuhakikisha kazi za umeme zinafanywa kwa ubora na weledi unaostahili.
IMETOLEWA NA
BW. TITUS KAGUO
MENEJA MAWASILIANO NA UHUSIANO
EWURA

No comments:

Post a Comment