TANGAZO


Sunday, October 14, 2012

Serikali yatakiwa kushirikiana na Sekta binafsi katika kuboresha elimu ya afya juu ya vifaa tiba nchini


Mtaalamu wa maabara na mshauri wa mashine za mionzi (vifaa tiba ) za binaddamu, Dk. Pilly Ally akitoa mada katika semina ya mafunzo ya kiafya juu ya vifaa tiba iliyoandaliwa na Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa na madaktari mbalimbali kutoka hospitali binafsi na za Serikali. Kushoto ni Mtaalamu na Mshauri wa Uchunguzi na Utafiti wa magonjwa ya binadamu wa hospitali hiyo, Dk. Nimish Chhaya.


Baadhi ya Madaktari waliohudhuria semina hiyo, wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zikitolewa kwenye semina hiyo.



Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya TMJ, Dk. Tayabal Jefferji, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, wakati wa semina   ya mafunzo ya kiafya juu ya vifaa tiba, iliyoandaliwa na hospitali hiyo jana. Semina hiyo, ilihudhuriwa na madaktari mbalimbali kutoka hospitali binafsi na za Serikali za jijini.


Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

SERIKALI kupitia wizara ya Afya na Ustawi wa jamii, imetakiwa kutoa ushirikiano wa moja kwa moja na sekta binafsi ya afya ili kuboresha  elimu ya afya juu ya vifaa tiba kutokana na kukua na kupanuka kwa teknolojia duniani  hali inayopelekea kuzuka kwa uhaba wa vifaa na wataalamu wa kutumia vifaa hivyo katika kuwahudumia wagonjwa kwa wakati.
Hayo yamesemwa na madaktari mbalimbali waliohudhuria mafunzo ya elimu ya afya juu ya uchunguzi, utafiti na kutibia iliyoandaliwa na Hospitali ya TMJ,  jijini Dar es Salaam jana na kujumuisha madaktari kutoka sekta binafsi ya afya na wengine kutoka katika hospitali za sereikali eneo la jiji la Dar esSalaam. 
Akiongea  na waandishi wa habari waliohudhuria katika  semina hiyo, mkurugenzi mtendaji wa wa Hospitali ya TMJ Dr Tayabal Jefferji amesema kuwa sekta ya afya inakabiliwa na changamoto nyingi hasa katika nchi zinazoendelea kutokana na kukua na kupanuka kwa teknolojia ya afya na kupelekea kubuniwa na kutengezwa kwa vifaa tiba vipya kadri siku zinaposonga mbele na kuongeza changamoto kubwa kwa watoa huduma za kiafya waliosoma taaluma hiyo kipindi cha nyuma sana.
“Mimi nilimaliza elimu yangu ya udaktari mnamo mwaka 1972, wakati huo na leo karibu ni kipindi kirefu sana ambacho kwa namna moja au nyingine kuna mabadiliko makubwa sana katika kutoa huduma kwa mgonjwa kwani wakati huo hata kifaa cha kujifunzia na kupimia magonjwa mbalimbali ilikuwa microscope ya kuchungulia kwa jicho moja lakini leo tuna vifaa vikubwa vinavyotumia computer” alisema Jefferji na kuongeza kuwa ni jukumu la serekali kupitia wizara husika kuendesha mafunzo mbalimbali kupitia semina ili kutoa fursa kwa madaktari wetu kujifunza mbinu na kanuni mbalimbali katika kutoa huduma kwa wagonjwa na kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya vifaa tiba, madawa na magonjwa mapya.
Kwa upande wake mganga mkuu wa Hospitali ya Apolo Medical Centre ilipo jijini Dar esSalaam Dr. Nazir H Arab amesema kuendesha semina na mafunzo ya mda mfupi kwa madaktari hapa nchini inaweza kuleta tija na mafanikio katika sekta ya afya hasa katika utafiti na uchunguzi kwa mgonjwa lakini mafanikio na mabbadiliko makubwa zaidi ni pale serikali ikianzisha shule mbalimbali za afya hasa za kuzalisha wataalamu wa maabara na wataalamu wa upauji pamoja na kuwekeza katika vifaa tiba adimu na muhimu katika kutoa huduma kwa wagonjwa ili kupunguza sio tu idadi ya wagonjwa kusafirishwa kwenda kutibiwa nje ya nchi bali pia kupunguza vifo visivyo vya lazima vinavyotokana na uhaba wa vifaa tiba au wataalamu.
Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya pua koo na masikia Dr. Emmanuel Ole Lengine kutoka hospitali ya taifa Muhimbili amesema Tanzania ni moja kati ya nchi zinazoendelea vizuri katika kuzalisha wataalamu wa afya katika eneo la Afrika lakini ikibakia kukabiliwa na changamoto ya uhaba wa vifaa tiba, “ Tanzania ina wataalamu wa kutosha kutoa huduma za afya lakini vifaa vya kutibia hakuna ndio maana wagonjwa wengi wanapelekwa kutibiwa nje ya nchi hasa India hali ambayo inaongeza gharama kubwa sana kwa mgonjwa, ndugu pamoja na taifa kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuongeza maumivu kwa mgonjwa kwa mda mrefu akisubiri kusafiri.” Alisema Dr Ole na kuongeza kuwa TMJ inastahili pongezi kubwa kwa kuona kuna umuhimu wa kuandaa na kuendesha mafunzo kwa madaktari bila kubagua pamoja na ukweli kuwa Hospitali hiyo ni ya binafsi.
Vifaa tiba vilivyofundishwa na kuelezewa namna ya ufanyaji kazi wake ni pamoja na Digital X- Ray ,CT SCANNER na MRI ambavyo kwa pamoja zina uwezo wa kuona ndani ya nyama laini za binadamu, mifupa, Ubongo, Damu na sehemu zingine za mwili kwa ukaribu na kutambua tatizo la mgonjwa, vifaa vyote hivi vinapatikana katika Hospitali ya TMJ ambapo watoa mada katika semina hiyo alikuwa Daktari mkuu kitengo cha maabara, uchunguzi na utafiti Dr. Nimish Chhaya kutoka Hospitali ya TMJ na Dr Pilly Ally mtaalamu wa picha za sehemu za ndani ya mwili Hospitali ya TMJ.

No comments:

Post a Comment