Hapa ni kwenye Uwanja wa Namboole jijini Kampala, ambapo wanaonekana mchezaji wa Uganda akichuana na wa Zambia mechi iliyoisha kwa Uganda kushinda bao 1-0. Ilipofika mikwaju ya penati, Zambia ikashinda kwa penati 9-8.
Wachezaji wa timu ya taifa ya Nigeria, wakishangilia bao lililofungwa na John Mikel Obi (wa kwanza kushoto)
Kikosi cha kwanza cha Uganda.
Wachezaji wa Zambia wakishangilia penati ya Stophira Sunzu iliyowapa tiketi ya kufuzu AFCON 2013 nchini Afrika Kusini mwakani.
Wachezaji wa Mali wakishangilia bao lililowapa tiketi ya AFCON 2013.
KAMPALA, Uganda
Katika mechi za jana usiku, timu za taifa za Zambia, Nigeria, Ghana, Ivory Coast, Mali, Tunisia na Morocco zilijikatia tiketi kuungana nawenyeji Afrika Kusini, wakati mbivu ama mbichi za Cameroon zilijulikana jana jijini Yaounde
MATAIFA 14 yalikuwa viwanjani jana Jumamosi usiku, katika mechi za marudiano kuwania tiketi ya kufuzu Fainali za Mataifa Afrika (AFCON 2013), zinazotarajiwa kufanyika nchini Afrika Kusini, huku pambano la Uganda na mabingwa watetezi Zambia likitazamwa mno na mashabiki.
Pambano hilo lililofanyika kwenye dimba la Taifa jijini Kampala, lilivuta hisia za wengi kutokana na ukweli kuwa, lilikuwa limeshikilia hatima ya watetezi hao – baada ya ushindi mwembamba wa bao 1-0 ilipocheza nyumbani kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola Septemba 8.
Katika mechi hiyo kwenye Uwanja wa Taifa wa Uganda (Namboole) jijini Kampala, bao la dakika ya 25 la Geofrey Massa, lilisawazisha lile la Chipolopolo la Septemba 8 lililofungwa na nahodha Christopher Katongo dakika ya 18, lakini jitihada za Uganda kupata bao la pili la kuivua ubingwa Zambia hazikuzaa matunda.
Mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi Djamel Haimoudi wa Algeria, ikaisha kwa bao hilo 1-0 na kulazimisha mikwaju ya penati iamue timu ya kwenda Afrika Kusini, ambapo shujaa wa kudumu wa Zambia Cris Katongo akakosa penati ya kwanza, kati ya tano, kama ilivyokuwa kwa Andrew Mwesigwa wa Uganda.
Katika matuta hayo matano, nyota wanne wa Uganda, Godfrey Walusimbi, Simeon Masaba, kipa Denis Onyango na Emmanuel Okwi, wakafunga huku Emmanuel Mayuka, Isaac Chansa, Nathan Sinkala na kipa Kenedy Mweene wakiifungia Zambia na kulazimisha mikwaju hiyo sasa kuingia katika piga nikupige.
Katika upigaji huo, Hamisi Kiiza akaifungia Uganda penati ya kwanza, kabla ya Felix Katongo kuilipa vema. Tonny Maweje akaifungia Uganda penati nyingine, iliyokuja kusawazishwa na Jonas Sakuwaha wa Zambia.
Moses Oloya akaifungia Uganda tuta la saba, lililosawazishwa na Chintu Kampamba. Geoffrey Kizito akaipachikia Uganda penati ya nane kati ya tisa, kabla ya Davies Nkausu kuifungia Zambia. Tuta la Patrick Ochan likaota mbawa, na kumfanya Stophira Sunzu kupiga tuta la ushindi kwa Zambia.
Mkwaju huo wa Sunzu, ukaipa Zambia tiketi ya kufuzu Mataifa Afrika 2013 nchini Afrika Kusini, inakokwenda kama mtetezi – aliyevuka kigingi kizito dhidi ya Uganda ambayo ilikuwa ikijaribu kusaka fainali ya kwanza tangu mwaka 1978 aliposhiriki na kutinga fainali ilikochapwa na Ghana mabao 2-0.
Miamba mingine nayo ilivyofuzu AFCON 2013
Ukiondoa pambano la Uganda na Zambia lililoipa Chipolopolo tiketi ya kufuzu AFCON 2013, jumla ya timu sita nyingine zilijikatia tiketi zao kwenye viwanja tofauti na kuzalisha timu nane zilizojihakikishia tiketi zao – pamoja na watetezi na wenyeji Afrika Kusini ‘Bafana Bafana.’
Mali ilijikatia tiketi ya AFCON 2013 baada ya ushindi wake wa jumla wa mabao 7-1 dhidi ya Botswana. Baada ya kuibuka na ushindi wa 3-0 nyumbani jijini Bamako Septemba 8, juzi Mali ikarejea ushindi mnono wa mabao 4-1 jijini Gaborone, shukrani kwa mabao ya Cheick Diabate, Modibo Maiga, Mamadou Samassa na Kalilou Traore.
Ghana maarufu kama Black Stars, nayo iliungana na Zambia, Afrika Kusini na Mali, baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Malawi ndani ya dimba la Civo jijini Lilongwe shukrani kwa bao la Afriyie Aquah, ushindi uliokuja baada ya ule wa mabao 2-0 katika mechi ya awali jijini Accra.
Baada ya sare ya 2-2 ugenini ilipoifuata Liberia jijini Monrovia Septemba 8, Tai wa Nigeria juzi walijitupa kwenye dimba la U.J.Esuene mjini Calabar na kuibuka na ushindi mnono wa mabao 6-1 na kufuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 8-3.
Victor Moses alifunga mara mbili, huku bao moja moja kutoka kwa Efe Ambrose, Ahmed Musa, John Mikel Obi na Ikechukwu Uche, yaliipa ushindi muhimu Nigeria, huku Liberia ikijifuta machozi kwa bao la Patrick Ronaldinho Wleh.
Msumbiji ikiwa na mtaji wa ushindi wa mabao 2-0 iliyouvuna nyumbani Estadio da Machava jijini Maputo Septemba 9, ikaifuata Morocco ikiwa na matumaini makubwa ya kufuzu AFCON 2013, kilichowakuta kwenye Uwanja wa Stade de Marrakech jijini Marrakech, hawatokisahau.
Wakaangukia pua kwa mabao 4-0 na kushindwa kabisa kuhimili kishindo cha Waarabu hao. Mabao ya Abdelaziz Barrada, Houssine Kharja, Youssef El Arabi na Nordin Hamrabat, yakatosha kuivusha Morocco na kuwarudisha nyumbani The Mambaz wakiwa hawaamini macho yao.
Tunisia nao wamefuzu AFCON 2013, licha ya kumaliza dakika 90 za pambano lake la nyumbani Stade MustaphaBen Jannet dhidi ya wageni wao Siera Leone. Tunisia imebebwa na sare ya mabao 2-2 iliyopata ugenini jijini Freetown, katika mechi ya kwanza Septema 8.
Mabao mawili ya mshambuliaji nyota wa Shanghai Shenhua ya China, Didier Drogba, ugenini kwenye uwanja wa Leopord Senghor jijini Dakar, yakaipa Ivory Coast tiketi ya AFCON 2013, baada ya kushinda 2-0 dhidi ya wenyeji Simba wa Teranga Senegal. Mechi ya kwanza Ivory Coast ilishinda kwa mabao 4-2.
Mataifa mengine nane nayo yasakwa leo usiku
Katika mfululizo wa mechi hizo za kuwania kufuzu AFCON 2013, leo usiku kutakuwa na mechi nane, ambapo washindi wa jumla wa mechi hizo, wataungana na miamba saba waliojikatika tiketi hizo juzi, sanjari na mwenyeji Bafana Bafana kwa ajili ya fainali hizo zilizopangwa ili kupishanisha na fainali za Kombe la Dunia.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo leo iko ugenini kwenye Uwanja wa Nuevo de Malabo, ikiwa na mtaji mnono wa ushindi wa mabao 4-0 iliyopata katika mechi ya kwanza dhidi ya Equatorial Guinea.
Sudan nao wamesafiri kuwafuata Ethiopia. Katika mechi ya awali, Sudan iliichapa Ethiopia kwa mabao 5-3, matokeo yanayofanya pambano la leo liwe gumu lenye nafasi kwa kila nchi kati ya mataifa hayo ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Simba Wasifugika Cameroon, nao watakuwa nyumbani Stade Ahmadou Ahdjo jijini Yaounde, kujaribu kusawazisha ushindi wa mabao 2-0 wa Cape Verde, kisha kusaka ushindi utakaowanusuru kukosa fainali za pili mfululizo za AFCON, baada ya kukosa zilizopita mapema mwaka huu huko Equatorial Guinea.
Je nani atacheka na nani atanuna? Bila shaka jibu utalipata kutokana na matokeo ya mechi hizo zinazochezwa kwa nyakati tofauti barani Afrika.
RATIBA YA MECHI ZA LEO OKTOBA 14, 2012
Burkina Faso v Afrika ya Kati
Matokeo ya awali: Afrika ya Kati 1-0 Burkina Faso
Togo vs Gabon
Matokeo mechi ya awali: Gabon 1-1 Togo
Equatorial Guinea v Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Matokeo mechi ya awali: DRC 4-0 Equatorial Guinea
Algeria vs Libya
Matokeo mechi ya awali: Libya 0-1 Algeria
Ethiopia vs Sudan
Matokeo mechi ya awali: Sudan 5-3 Ethiopia
Niger vs Guinea
Matokeo mechi ya awali: Guinea 1-0 Niger
Cameroon vs Cape Verde
Matokeo mechi ya awali: Cape Verde 2-0 Cameroon
Angola vs Zimbabwe
Matokeo mechi ya awali: Zimbabwe 3-1 Angola
No comments:
Post a Comment