TANGAZO


Wednesday, August 15, 2012

Rais Dk. Shein apatanisha mzozo wa wavuvi wa Marumbi na Chwaka

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akisalimiana na viongozi mbalimbali, alipowasili katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Marumbi, kuzungumza na wananchi na wavuvi katika kijiji hicho leo. (Picha zote na Ramadhan Othman,Ikulu)

Baadhi ya wananchi na wavuvi  wa kijiji cha Marumbi, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, alipowasili Shule ya Sekondari ya Marumbi, kuzungumza na wananchi na wavuvi katika kijiji hicho leo.

Msemaji wa wananchi na wavuvi wa kijiji cha Marumbi, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, Ufuzo Haji, akitoa maelezo ya malalamiko ya wananchi hao, mbele ya Rais wa Zanzibar, alipowasili Shule ya Sekondari ya Marumbi kusikiliza kilio chao, kutokana na mzozo na watu wa kijiji cha Chwaka  leo.

Akina mama wa kijiji cha Marumbi, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, alipofika Shule ya Sekondari ya Marumbi, kuzungumza na wananchi na wavuvi katika kijiji hicho leo, kusikiliza kilio chao cha kuchomewa moto boti zao mbili. 
 Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Issa Haji Gavu, akitoa maelezo mbele  ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, wakati alipofika katika Shule ya Marumbi, kusikiliza malalamiko ya mzozo wa wananchi wa kijiji cha Marumbi na wananchi wa Chwaka, baada ya wananchi wa Chwaka walipozichukua boti mbili na kuzichoma  moto hivi karibuni.

Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Abdilah Jihadi Hassan, akitoa maelezo mbele ya   Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, wakati alipofika katika Shule ya Marumbi, kusikiliza malalamiko ya mzozo wa wananchi wa kijiji cha Marumbi na wananchi wa Chwaka, baada ya wa Chwaka walipozichukua boti mbili na kuzichoma  moto hivi karibuni.

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Mustafa Aboud Jumbe, akitoa maelezo mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, wakati alipofika katika Shule ya Marumbi kusikiliza malalamiko ya mzozo wa wananchi wa kijiji cha Marumbi na wananchi wa Chwaka, baada ya wa Chwaka walipozichukua boti mbili na kuzichoma moto hivi karibuni.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, alipokuwa akizungumza na  na viongozi na wananchi pamoja na wavuvi wa kijiji cha Marumbu, Wilaya ya Kati, Mkoa Kusini Unguja leo, katika  Shule ya Sekondari ya Marumbi, kuhusu tatizo la mzozo wa wavuvi wa kijiji hicho, kuchukuliwa boti zao na wavuvi wa kijiji cha Chwaka na hatimaye kuzichoma moto boti hizo.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza katika mkutano na viongozi na wananchi pamoja na wavuvi wa kijiji cha Marumbu, Wilaya ya Kati, Mkoa Kusini Unguja leo, katika  Shule ya Sekondari ya Marumbi, kuhusu tatizo la mzozo wa wavuvi wa kijiji hicho, kuchukuliwa boti zao na wavuvi wa kijiji cha Chwaka na hatimaye kuzichoma moto boti hizo.

Rais Shein azungumza na wananchi wa Marumbi
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Zanzibar                                                                                              15.8.2012

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amefanya mazungumzo na wananchi wa kijiji cha Marumbi na kuwataka kufungua ukurasa mpya wa kumaliza mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 30 kati yao na wanakijiji wa Chwaka na kujenga uhusiano mwema baina yao.
Mazungumzo hayo yalifanyika huko katika katika Skuli ya Marumbi kati ya Rasi na wananchi wakiwemo wavuvi wa kijiji hicho kiliopo, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, kufuatia mgogoro huo uliodumu muda mrefu juu ya suala zima la uvuvi haramu unaofanyika katika eneo la mpaka wa bahari kati ya Marumbi na Chwaka.
Katika maelezo yake Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao wa kike na kiume waliojaa mbele ya viwanja vya skuli hiyo ya Marumbi wakiwa na hamu ya kumsikikiliza kiongozi huyo kama walivyoomba baada ya kukataa kuzungumza na viongozi wengine wote wa ngazi mbali mbali, wakiwemo wa Wilaya na Mkoa.
Dk. Shein katika mazungumzo yake na wananchi hao wa Marumbi aliwakata kujenga uhusiano mwema baina yao na ndugu zao wa Chwaka pamoja na kujenga imani na pia, kuwataka washirikiane na viongozi wao kwani wote ni wamoja huku akiahidi kwenda kuzungumza na wananchi wa Chwaka hapo baadae ili kuumaliza kabisa mgogoro huo.
Alieleza kuwa amefurahishwa na wananchi hao kwa kumuomba aende kuwasikila matatizo yao yanayowakabili na kueleza kuwa kweli amegundua kuwepo kwa tatizo la uvuvi haramu unaofanywa katika Ghuba hiyo ya Chwaka na kuviagiza vyombo husika kulichukulia hatua mara moja.
Alisema kuwa kuna haja ya kufuatwa Sheria na taratibu zilizowekwa juu ya uvuvi wa bahari, Sheria ambazo zimewekwa na Serikali kwa mashirikiano na wananchi na wavuvi wenyewe wa Unguja na Pemba.
“Najua mna hoja ya msingi ya kunitaka mimi kuja Marumbi leo, tumekumbushwa kuwa ni lazima tuishi vizuri na majirani… kufuata sheria na taratibu za Serikali na lazima tuelewe kuwa lengo ni kupata suluhisho, haiwezekani mwanaadamu wa karne hii wakagombana wakati wote”,alisema Dk. Shein.
Aidha, alieleza kusikitishwa kwake na baadhi ya watu mgogoro huo kuuhusisha na mambo ya siasa na kueleza kuwa ni ukweli usiopingika kuwa ajira hazitoshi na ndio maana wananchi waliowengi katika maeneo hayo hujishughulisha na shughuli za uvuvi, hivyo ipo haja ya kuyaezi na kuyatunza mazingira ya bahari ili yalete tija.
Dk. Shein alisem kuwa lengo la Serikali ni kuiimarisha sekta ya uvuvi ili iwe endelevu kwa kuwaendeleza wavuvi kwa  kuwatafutia mikopo na mitaji ili waweze kuvua zaidi hadi kufikia bahari kuu kwani ndio utaratibu unaoandaliwa na serikali na hautochukua muda pindipo kama mipango itakwenda vizuri.
Alisema kuwa watu wa Marumbi wanahistoria kubwa katika kujiletea maendeleo sanjari na kuwa wastaarabu hivyo aliwataka wasikubali kuchokozeka wala kuchukua sheria mikononi mwao na yale yanayohusu serikali waiachie serikali iyafanyie kazi.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein aliwasisitiza wananchi wa Marumbi na maeneo mengine nchini kutunza mazingira kutokana na hali ya Tabia nchi inavyojitokeza hivi sasa hatua ambayo imepelekea joto kuwa kali pamoja na kupungua kwa kiwango cha maji katika ardhi na kuzidi kiwango cha maji ya bahari.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Shein alisisitiza kuwa Serikali haitochelea kuchukua Sheria kwa yeyote Yule atakae ivunja na kuvitaka vyombo vya Sheria kufanya wajibu wao na kulitaka Jeshi la Polisi kuwasaidia wananchi katika kusimamia Sheria.
Pia, alizitaka Mahakama nazo ziendelee kufanya wajibu wao kama ilivyokawaida pamoja na kazi zao vizuri bila ya kuingiliwa huku akiutaka uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kufanya kazi ipasavyo.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwasisitiza wananchi hao wa Marumbi kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa linalotarajiwa kufanyika mwezi huu na kuachana na mgomo waliokuwa wameuweka hapo kabla kwani zoezi hilo litawasaidia katika maendeleo yao.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwaahidi wananchi hao wa Marumbi kuwa ahadi alizoziahidi Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Idd zipi pale pale ikiwa ni pamoja na kueleza kuwa kwa kushirikiana nae watawapelekea mashua mbili na vifaa vyengine vitapelekwa na Wizara husika.
Akitoa maelezo kwa niaba ya wananchi wa Marumbi Bwana Ufuzo Haji alitoa shukurani kwa ujio wa Dk. Shein na kumueleza kuwa  katika eneo hilo la Ghuba ya Chwaka kumekuwa na mgogoro wa siku nyingi hali ambayo ilipelekea hadi kuchomwa moto vyombo vyao vya uvuvi pamoja na vifaa vyengine.
Wananchi hao walieleza kuwa kutokana na kuwepo kwa mgogoro huo wa muda mrefu ndipo walipokataa kukutana na viongozi wengine wote ila Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwani yeye ndio atakaewasaidia kutatua.
Aidha, walieleza kuwa mbali ya hatua hiyo ya kumuomba Rais pia walikwishaanza kususia shughuli zote za chama na Serikali hadi wakabidhiwe vifaa vyao vilivyoharibiwa.
Bwana Ufuzo alieleza kuwa sio kweli kama alivyoambiwa Rais katika ziara zake za Mikoa hivi karibuni kuwa mgogoro huo umeshamaliza bali ulikuwa bado unaendelea huku akisisitiza kilio chao kikubwa ni kuwepo kwa uvuvi haramu unaosababishwa na watu wachache.
Naye Waziri husika wa Wizara hiyo alieleza juhudi za makusudi zlizozichukua tokea alipoingia katika Wizara hiyo lakini alikiri kuwa zimegonga mwamba licha ya kuahidiwa na wananchi hao kuwa suluhisho limeshapatikana.
Mapema Makurugenzi wa Uvuvi, Mussa Aboud Jumbe alimueleza Dk. Shein kuwa Sheria ya Uvuvi ipo na juhudi za makusudi zilichukuliwa katika kuhakikisha wavuvi wanashirikishwa katika utungaji wake sanjari na kupata maoni kutoka kwa Kamati zote za uvuvi
“Sheria ipo, na kwa mara ya kwanza ni mchango wa wananchi wote wa Unguja na Pemba wakiwemo wananchi wa Marumbi”,alisema Mussa.
Alisema kuwa suala la doria limekuwa ni gumu kufanyika kwani hujitokeza baadhi ya wananchi wa Marumbi na kuwaambia wananchi wa Chwaka siku inayokusudiwa kufanywa doria na kusababisha kutofanikiwa zoezi hilo huku akikiri kuwa uvuvi haramu kwenye Ghuba ya Chwaka umekisiri.
Mkurugenzi Mussa alisisitiza kuwa Sheria imepiga marufuku uvuvi wa nyavu ya kukokota,uharibifu wa nyavu za mtando, mabomu na matumizi ya umangu, matumzi ya sumu ambayo yote haya ndani ya sheria yametajwa.
Viongozi wengine waliotakiwa na Rais kutoa maelezo yao mbali ya hao ni Mkuu wa Wilaya na Mwakilishi wa kiongozi wa KMKM ambao nao walikiri kuwepo kwa mgogoro huo na kueleza juhudi zilizochukuliwa huku mkuu wa Wizaya akisikitishwa na hatua za wananchi hao kutkataa kuzungumza na viongozi wa ngazi za chini kabla ya kumuomba Rais.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi na Kaibu Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mhe. Abdalla Mwinyi Khamis aliusifu ustaarabu wa wananchi wa Marumbi kwa kutoa maelezo yao kwa uwazi na ukweli bila ya kuonesha ghadhabu na hasira mbele ya kiongozi wao mkuu wan chi kwa lengo la kutafuta suluhisho la mgogoro huo.





No comments:

Post a Comment