Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA),
Dk. Joyce Ndalichako, akiwa pamoja na baadhi ya watendaji wenzake, Naibu Katibu Mtendaji wa Baraza, Dk. Charles Msonde (kushoto na Mkuu wa Idara ya Fedha na Utawala, Daniel Mafie, akiwaonesha waandishi wa habari moja ya kielelezo cha wizi wa mitihani
alichokamatwa nacho mmoja wa watahiniwa, wakati akipokuwa akitangaza mitihani ya Maarifa (QT) na Kidato cha nne (CSEE), Dar es Salaam hivi karibuni.
NA ZAHIRA BILALI SAID
MAELEZO ZANZIBAR
Kamati ya Wazee wa
Wanafunzi walofutiwa matokeo yao ya Mitihani wa Kidato cha Nne Zanzibar imesema
haikubaliani na uamuzi wa kuwafutia matokeo wanafunzi wale tu walioshutumiwa
kufanya udanganyifu badala yake imetaka Wanafunzi wote kufutiwa matokeo yote kwa
vile mitihani ilivuja.
Katika taarifa yao
iliyotolewa kwa Vyombo vya Habari Kamati hiyo imesema Baraza la Mitihani
linapaswa kuurejea Mtihani huo kwa Zanzibar na Tanzania Bara kwani kufanya
hivyo kutapunguza malalamiko na dhana iliyoibuaka ya tatizo hilo kuwa kasoro
nyengine mpya ya Muungano.
Mwenyekiti wa Kamati
hiyo Ali Hassan Khamis amesema ikiwa Baraza la Mitihani NECTA litaona ugumu
kuurudia mtihani basi libainishe kwa walimu wao makosa ya kila mwanafunzi kwa
wale waliofutiwa na wale wenye mashaka na matokeo yao.
Ali amesema
Wazanzibari wameanza kupoteza imani na Baraza hilo hasa baada ya kutoa matokeo
kwa baadhi ya wanafunzi ambao tayari walishafutiwa matokeo yao hapo kabla na
kupewa ufaulu wa Daraja la Nne na Daraja Ziro.
Akitaja mapungufu
ambayo yalijitokeza katika Baraza hilo amesema kuna baadhi ya wanafunzi
walifanya mitihani ya masomo ya Sanaa lakini wakapewa matokeo ya masomo ya
Sayansi na baadhi yao walifanya masomo ya Sayansi na kupewa matokeo ya Sanaa.
Aidha amesema Baraza
hilo limekosa umakini katika kufanya kazi zake kwani kuna baadhi ya wanafunzi
wameandikiwa "Absent" kwa maana hawakufanya mtihani lakini kiukweli
wanafunzi hao walifanya mitihani yao kikamilifu.
Kwa upande wake
Mkurungezi Mtendaji wa Jumuiya ya Kuzuia,Kukinga na Kuondosha Maafa na Majanga
Zanzibar Najma Murtaza Giga amelishauri Baraza la Mitihani kuukubali ukweli
kwamba mitihani ilivuja na hivyo waondoshe adhabu waliyoitoa kwa wanafunzi hasa
ikizingatiwa muhusika wa kwanza wa kosa hajajulikana.
Najma amesema ikiwa
Baraza la Mitihani halitozingatia taarifa yao na kuitolea jibu muafaka Jumuiya
italazimika kushirikiana na Kamati ya Wazazi kupeleka ombi lao Mahakama Kuu ya
Zanzibar Vuga kwa kutumia hoja za msingi za kisheria ili Mahakama hiyo iweze
kutoa tamko la kumtaka Katibu Mtenfdaji wa Baraza Joyce Ndalichako na Baraza
lake kufuata vizuri kanuni na sheria za Baraza hilo.
Aidha ameongeza kuwa
Jumuiya yao imesikitishwa na baadhi ya wanafunzi ambao wamevunja sheria na
kutumia njia za udanganyifu wa aina mbali mbali katika kujibu mitihani yao.
Kwa mujibu wa Takwimu
ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar wanafunzi wasiopungua 13,000 wa
shule za Serikali na binafsi walifanya mtihni ambapo wanafunzi 60 tu
walibahatika kufaulu daraja la Mwanzo.
Wanafunzi 160
walibahatika daraja la Pili, wanafunzi 776 walifaulu Daraja la Tatu, Wanafunzi
8150 walipata Daraja la Nne, Wanafunzi 2948 walifeli kabisa ambapo kwa upande
wa walioufutiwa matokeo ni wanafunzi wasiopungua 1000.
No comments:
Post a Comment