Mtaalam wa matumizi ya teknolojia ya simu katika utoaji wa elimu Dk. Paul Kim, akionesha teknolojia hiyo inavyofanyakazi. |
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
25/2/2012, Dar es salaam.
Imeelezwa kuwa Tanzania itapiga hatua katika sekta ya elimu na kuongeza uelewa miongoni mwa wanafunzi iwapo matumizi ya teknolojia ya simu na kompyuta katika kufundishia yatazingatiwa kuanzia elimu ya msingi mpaka vyuo vikuu.
Akizungumza na wadau wa elimu na mawasiliano leo jijini Dar es salaam mtaalam wa matumizi ya teknolojia ya simu katika utoaji wa elimu kutoka chuo kikuu cha Stanford kilichoko Calfonia nchini Marekani Dkt. Paul Kim amesema hivi sasa dunia inabadilika kutoka hatua moja kwenda nyingine na kusisitiza kuwa matumizi ya teknolojia ya simu na kompyuta katika sekta ya elimu hayaepukiki.
Amesema matumizi ya teknolojia hiyo yameendelea sana katika nchi zilizoendelea za bara la Ulaya , Amerika na baadhi ya nchi za Asia huku akisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo katika bara la Afrika yanaendelea kuongezeka kwa kasi ukilinganisha na miaka iliyopita.
“Ufanisi wa matumizi ya teknolojia ya simu na kompyuta pamoja na mabadiliko yake kwa maendeleo ya elimu duniani kote unahitaji utayari na ushiriki wa watu, viongozi wa nchi husika na taifa kwa ujumla” amesema Dkt. Kim.
Amefafanua kuwa yeye kama mtaalam wa matumizi ya teknolojia ya simu na kompyuta kwa kushirikiana na Shirika la Seed Empowerment yuko nchini Tanzania kushirikiana na kufanya kazi pamoja na wadau mbalimbali wa elimu kutoka taasisi mbalimbali za serikali na binafsi, vyuo vya elimu na sayansi, vyuo vikuu, shule za msingi na sekondari ili kuhakikisha kuwa teknolojia hiyo inapatikana na matumizi yake yanakuwa endelevu nchini.
Amesema pamoja na Tanzania kukabiliwa na changamoto mbalimbali za matumizi ya teknolojia hii atatumia uzoefu wake na utaalam wake kwa kushirikiana na mamlaka husika za elimu katika kuhakikisha kuwa teknolojia ya matumizi ya simu katika utoaji wa elimu nchini inaendelea na kukua kwa kasi.
“ Ninajua matumizi ya teknolojia ya Kompyuta na simu katika kufundishia hapa Tanzania bado yako chini lakini kwa kutumia uzoefu wangu wa chuo kikuu Stanford, Marekani na uzoefu wa nchi yangu ya Korea ya Kusini nilikozaliwa ambayo maendeleo yake katika matumizi ya teknolojia hii yalianza taratibu kwa kushirikiana kikamilifu na wadau wa Tanzania tutaweza kuinua kiwango cha elimu kwa matumizi ya teknolojia hii”.
Kwa upande wake Bi. Zamaradi Saidi mdau na mshiriki wa mkutano huo ambaye ni mtaalam wa Elimu na mafunzo amesema mpango huo kwa Tanzania unalenga kuingia katika mfumo wa elimu kuleta teknolojia ya kufundishia katika sekta ya elimu katika ngazi zote na kuusifu mpango huo kuwa utawawezesha wanafunzi kujifunza kutokana na programu zilizoandaliwa ambazo zitawafaa wanafunzi wenye ulemavu.
Pia amefafanua kuwa mpango huo utawawezesha wanafunzi na walimu kuwa na uelewa wa matumizi ya vifaa vya kompyuta kutokana na tatizo la kuwepo kwa baadhi ya shule na vyuo ambavyo vimekuwa vikipatiwa misaada ya kompyuta lakini hazitumiki kutokana na uelewa mdogo wa wanafunzi na walimu.
Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yatasaidia kuboresha mfumo wa ufundishaji na kuwajengea uwezo wanafunzi kuwa wabunifu na kuepuka tabia ya kukariri masomo hivyo kuongeza uelewa wao na kuwafanya walimu kubaki kama wawezeshaji.
Naye mkufunzi na kaimu mkuu wa kitengo cha teknolojia maalum (ASTU) kutoka Taasisi ya Elimu na Teknolojia ya Chuo Kikuu Huria Tanzania Bw. Cosmas Mnyanyi amesema kuwa licha ya mpango huo kuwa na manufaa makubwa na mchango mkubwa wa maendeleo ya elimu endapo utatumika hapa nchini bado mfumo wetu wa elimu una vikwazo mbalimbali vikiwemo ukatazaji wa matumizi ya simu kwa wanafunzi hivyo mkakati huo unahitaji kutolewa elimu ili kuleta ufanisi utakaporuhusiwa kutumika nchini.
No comments:
Post a Comment