TANGAZO


Friday, June 8, 2018

WATAALAMU WA ARDHI WAUSIFIA MFUMO MPYA WA UPIMAJI ARDHI

Mkurugenzi msimamizi wa shughuli za miradi ya Urasimishaji Ardhi Vijijini (LTA) - Iringa, Mustapha Issa, akielezea jinsi mfumo mpya wa upimaji ardhi ‘MAST’ unaotumia simu za kisasa unavyofanya kazi ya upimaji wa vipande vya ardhi. Mafunzo hayo yalifanyika hivi karibuni mkoani Iringa. 
Afisa Mipango Miji na Vijiji wa Halmashauri ya Mvomero, Morogoro, Sadoth Kyaruzi akichangia jambo wakati wa mafunzo ya mfumo mpya wa upimaji ardhi ‘MAST’ yaliyofanyika hivi karibuni mkoani Iringa. 
Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya mfumo mpya wa upimaji ardhi ‘MAST’ yaliyofanyika hivi karibuni mkoani Iringa akihoji  kutaka kufahamu nini hufanyika baada ya kukuta taarifa ya mteja imekosewa au eneo lina mgogoro. 
Timu ikikagua mchoro wa shamba husika kupitia mipaka/ alama walizokuwa wakionyeshwa na mwenye shamba wakati wa mafunzo ya mfumo mpya wa upimaji ardhi ‘MAST’ yaliyofanyika hivi karibuni mkoani Iringa.

Na Mwandishi Wetu.
WATAALAMU 16 toka Halmashauri za Wilaya ya Morogoro, Mvomero, Bahi, Kongwa, Kilolo na Mufindi walio chini ya Idara ya Ardhi, maliasili na mazingira wamejengewa uwezo juu ya utumiaji wa mfumo mpya na rahisi wa upimaji ardhi unaofahamika kwa jina la ‘Mobile Application for secure tenure’ (MAST).
Akizungumza mkoani Iringa wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya darasani pamoja na ya vitendo yaliyoandaliwa na Shirika la PELUM Tanzania, Mratibu wa PELUM, Donati Senzia alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwapatia elimu wataalamu hao ili waweze kuutumia mfumo huo kwenye Halmashauri zao kupitia miradi ya upimaji ardhi.
“Shirika letu liliona ni muhimu maafisa wanaoshughulikia masuala ya ardhi kuendelea kujifunza njia bora na rahisi za upimaji na utoaji hatimiliki na ndiyo maana tuliamua kuwashirikisha wenzetu wa Mradi wa Urasimishaji Ardhi Vijijini kutoa mafunzo haya kwa jumla ya wataalam wa ardhi 16 ili kurahisisha kazi zao”, alisema Senzia.  
Senzia ameongeza kuwa kupitia ziara hiyo ya mafunzo amegundua kuwa kama shirika la PELUM lingetumia mfumo huo lingeweza kupima zaidi ya vijiji 28 na kuvuka lengo la mradi kwa kugawa hatimiliki mapema zaidi kwa kila kijiji kilichomaliza kupimwa kwani mfumo huo unaweza kudurufu jumla ya hatimiliki 200 kwa siku.
Akifafanua jinsi mfumo huo unavyofanya kazi, Mkurugenzi msimamizi wa shughuli za miradi ya Urasimishaji Ardhi Vijijini (LTA) - Iringa, Mustapha Issa amesema kuwa mfumo huo unaotumia simu za kisasa ulitengenezwa kwa ajili ya uhakiki wa maslahi katika upimaji wa vipande vya ardhi.
“Lengo letu kuu ni kuhakikisha mfumo huu unatumika nchi nzima kwani mpaka sasa tumeshatoa elimu hii kwenye Halmashauri nane nchini, Wizara ya ardhi maendeleo na mkazi, Tume ya Taifa ya usimamizi wa mipango ya matumizi bora ya ardhi, Chuo kikuu cha ardhi pamoja na mashirika binasfi manne” alisema Issa.
Issa ameongeza kuwa mbali na kuwa mfumo huo unatoa ajira kwa vijana wengi ikiwemo wapimaji wasaidizi, pia mfumo huo hutumia muda mfupi katika upimaji, uchukuaji taarifa, utunzaji taarifa pamoja na utoaji wa hatimiliki.
Nae Afisa Ardhi wa Wilaya ya Bahi, Georgina Kallaghe amesema mfumo huo utapunguza muingiliano wa kutambua picha sahihi ya muhusika kwani fomu zikikaa muda mrefu picha zinaweza kujichanganya kwenye fomu za wamiliki wengine na muda mwingine taarifa za mteja hupotea ama kuliwa na panya hivyo kusababisha upotevu wa taarifa wakati wateja wanaporudishiwa kufanya uhakiki wa taarifa zao muhimu.
Ameongeza kuwa mfumo huo unaweza kutumiwa na mtu yeyote kwani huchukua na kuhifadhi taarifa za mmiliki wa kipande cha ardhi moja kwa moja zikiwemo taarifa za mchoro wa kipande husika cha ardhi pamoja na picha ya muhusika mara tu baada ya mpimaji kuridhika na taarifa za mmliki tofauti na ilivyo sasa hadi umsubiri ama kumtafuta Afisa mipango miji ama mpima ardhi achore mchoro husika.
Kwa upande wake Afisa Mipango Miji na Vijiji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Fred Mgeni ameelezea utofauti uliopo kwenye kipimo hicho cha MAST kuwa kipimo kinachotumika sasa kina mapungufu ya uhakiki kuanzia mita 1-10 jambo ambalo halitakiwi kwani inashauriwa walau mapungufu hayo yasizidi mita 1-3.
Pia Afisa Mipango Miji na Vijiji wa Halmashauri ya Morogoro Andrea Biashara amesema mfumo huo unatumia gharama ndogo kwa sababu unatoa hatimiliki zenye picha zisizo na rangi.
”Napenda kutoa rai kwa Makamishina wa Ardhi wa Vijiji pamoja na wataalamu wengine toka Wizarani kuendelea kufanya hivyo kama sehemu ya kuwezesha hati nyingi kutolewa kwani gharama ya wino wa rangi kwa mashine kubwa inayotoa hati nyingi inafika hadi milioni sita jambo ambalo halmashauri nyingi haziwezi kulileba,” alisema Biashara.

No comments:

Post a Comment