Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Wananchi wa Shehia yha Maziwani Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Kituo cha Afya kilichojengwa na Wananchi wenyewe.(Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)
Afisa Mdhamini Wizara ya Afya Kisiwaini Pemba Bibi Shdya Shaaban Seif kitoa maelezo mbele ya Balozi Seif juu ya muelekeo wa huduma za Afya zitakazotolewa Kwenye Kituo cha Afya cha Maziwani mara baada ya kukamilika ujenzi wake.
Balozi Seif aliyeambatana na Mfanyabiashara Maarufu Zanzibar Said Nasser Bopar wakimkabidhi msaada wa magodoro na vifaa mbali mbali Afisa Mdhamini wa Wizara ya Afya Pemba Bibi Shadya Shaaban kwa ajili ya Hospitali ya Wete.
Balozi Seif na Mfanyabiashara Said Bopar wakikamilisha utoaji wa Vifaa mbali mbali kwa ajili ya Hospitali ya Wete akiwa katika ziara ya siku Tatu Kisiwani Pemba.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akimpatia zawadi ya siku kuu mgonjwa Bibi Time aliyelazwa katika Hospitali ya Wete Kisiwani Pemba akipatiwa huduma za matibabu.
Na Othman Khamis Ame, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
8/6/2018.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema azma ya Serikali kuwafikishia huduma ya umeme wananchi wa vijiji vilivyomo ndani ya Shehia ya Maziwani Wilaya ya Wete, bado iko pale pale baada ya kukamilika kwa kazi ya upelekaji huduma ya umeme katika Kisiwa cha Uvinje.
Alisema zoezi la upelekaji Umeme katika Kisiwa cha Uvinje litakapokamilika, Wahandisi wa Shirika la Umeme Zanzibar {ZECO} watahamishia kazi zaokatika shehia ya Maziwani pamoja na Vijiji vyengine vya jirani kwa vile tathmini hali ya mradi huo imeshakamilika.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alieleza hayo, wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Shehia ya Maziwani mara baada ya kukagua kituo cha afya kilichojengwa kwa nguvu za wananchi wenyewe kikifikia hatua ya uwezekwaji.
Alisema upelekaji umeme uvinje ni ahadi aliyoitoa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein, wakati akizindua umeme Kisiwa cha Fundo, ambapo Wahandisi wa ZECO kwa sasa wamehamia huko kutekeleza ahadi hiyo.
Alisema wakati serikali imeweza kupeleka mradi mkubwa wa umeme katika kisiwa cha Fundo, basi haiwezi kuwasahau wananchi wa maziwani na vijini jirani kufikishiwa huduma hiyo.
“Bado dhamira ya Serikali kuwafikishia huduma za umeme wananchi wake iko pale pale, hivyo wananchi wa maziwani na nyinyi mtanufaika na huduma hizo za umeme pia muda si mrefdu”. Alisema Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba huduma ya umeme sio anasa kwa Karne ya sasa bali ni moja ya kichocheo kikubwa cha kukuza uchumi hasa katika lengo la kuwasaidia wananchi kuimarisha Miradi yao ya kimaendeleo.
Akizungumzia ujenzi wa kituo cha Afya cha Maziwani kilichojengwa na Wananchi wenyewe, Balozi Seif, aliwashukuru wananchi hao kwa juhudi zao za kuhakikisha kujengwa kituo hicho cha afya, ambacho tayari kimeshagharimu zaidi ya Shilingi Milioni 10 iikiwa ni nguvu kazi na michango ya wananchi.
Alisema Sera ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwepo kwa huduma za Afya kila baada ya Kilomita tano bado inaendelea ili kuwasogezea wananchi wake huduma bora za afya kuwa karibu nao.
“ Ukweli hatua iliyofikiwa ya Ujenzi wa Kituo chenu cha Afya inaridhisha na kupongezwa ambapo kazi iliyobakia itabebwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya kukamilisha hatua zote zilizobakia”. Alisema Balozi Seif.
Akitoa Taarifa ya wananchi wa Maziwani kuhusu Ujenzi wa Kituo cha Afya Katibu wa Kamati ya Ujenzi huo Nd. Hamad Kombo Hamad alisema Jengo hilo tayari limeshagharimu Shilingi Milioni 10 kwa hatua iliyofikiwa, huku milioni 11 zikihitajika ili kukamilisha.
Nd. Hamad alisema kukamilika ka kwa kituo hicho kutasaidia kupatikana kwa huduma za Afya katika vijiji Vinne vilivyozunguuka Shehia ya Maziwani kikiwemo Jitenge, Tondooni, Mwane, Maziwani.
Katibu huyo w Kamati ya Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Shehia ya Maziwani aliiomba Serikali kupitia Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar inayosimamia Miradi yaTasaf kusogeza miradi inayosimamiwa na Mfuko huo ili isaidie kupunguza ukali wa Maisha wa Wananchi hao.
Kwa upande wake Afisa Mdhamini Wizara ya Afya Kisiwani Pemba Bibi Shadiya Shaaban Seif alisema ujenzi wa kituo cha afya Maziwani utasaidia kuwapunguzia masafa marefu wananchi wa shehia hiyo ambao kwa sasa hulazimika kufuata huduma za afya masafa marefu.
Alisema Wizara ya Afya imejipanga kutoa huduma mbali mbali wakati kitakapokamilika kituo hicho ikiwemo afya ya mama na mtoto, chanjo, kwa vile Shehia ya Maziwani inakadiriwa kuwa na Watoto 135 walio na mwaka mmoja, watoto 390 wenye umri wa miaka mitano na wanawake wenye umri wa kujifungua 612.
Akitoa taarifa ya kitaalamu juu ya upelekeaji umeme katika shehia ya Maziwani, Mhandisi wa ZECO Ali Faki Ali, alisema kazi ya upelekaji umeme katika shehia hiyo imeshakamilika.
Mhandisi Ali Faki alisema gharama ya jumla mradi huo inakisiwa kufikia shilingi Milioni 109 itakayojumuisha kazi ya ujenzi wa laini kubwa, laini ndogo pamoja na upachikaji wa Tansfoma yenye nguvu za KV 50.
Akikabidhi Misaada mbali mbali iliyotolewa na Mfanyabiashara maarufu Zanzibar Said Nasser Nassor (Bopar) kwa hospitali ya Wete, Balozi Seif alisema suala la afya ni la kila mtu, hivyo aliwataka wafanya biashara wengine kufuata nyayo za mfanya biashara huyo katika kuchangia huduma za matibabu.
Aidha aliutaka Uongozi wa Wizara ya Afya Pemba pamoja na wafanyakazi wa Hospitali ya Wete kuhakikisha wanavitunza vifaa hivyo walivyopatiwa na kuacha udokozi ambao hujitokeza kwa baadhi ya watendaji wasio waaminifu ili vidumu kwa muda mrefu.
Alisema Serikali pekee haina uwezo wa kukamilisha kila katika kutoa huduma kwa Wananchi wake bila ya kupata msaada kutoka kwa Wazalendo wa Taifa hili wakiwemo Wafanyabiashara huu wanaowajibika kuunga mkono juhudi za Serikali za kutoa huduma hizo.
Akimkaribisha kuzungumza na Wafanyakazi wa Hospitali ya Wete Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Omar Khamis Othman alimshukuru Mfanya Biashara Said Nasser Bopar kwa uamuzi wake wa kusaidia huduma za Kijamii ikiwemo Sekta ya Afya.
Mh. Omar valisema kutoa ni moyo unaohitaji uzalendo na upendo na sio utajiri kwani wapo wengi wenye uwezo kamili wa kusaidia huduma na ustawi wa Wananchi lakini bado wazito wa kufanya hivyo.
No comments:
Post a Comment