TANGAZO


Thursday, June 7, 2018

TAARIFA YA CUF KWA UMMA KUHUSU WALIOIBA FEDHA ZA RUZUKU CUF KUJIANDAA KUJIBU MASHTAKA MAHAKAMANI

THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF–Chama Cha Wananchi)


TAARIFA KWA UMMA NA VYOMBO VYA HABARI

WALIOIBA FEDHA ZA RUZUKU CUF WAJIANDAE KUJIBU MASHTAKA MAHAKAMANI:

Imetolewa Leo Tarehe 7 June, 2018

1.      THE CIVIC UNITED FRONT [CUF-Chama Cha Wananchi] Kinaungana na Watanzania wote kuwapongeza wabunge wake, wakiongozwa na Mhe. Mohamed Juma Khatib Mbunge wa Jimbo la Chonga, kwa kutekeleza wajibu wao vizuri na kuibua UFISADI WA FEDHA ZA UMMA unaofanywa na matapeli wa kisiasa, vibaraka na wasaliti ndani ya CUF kwa njia ya Ruzuku ya serikali kwa vyama vya siasa nchini. 

2.      Katika kikao cha bunge Tarehe 5/6/2018, wakati akichangia bajeti ya wizara ya Fedha kwa mwaka wa 2018/2019, Mhe. Khatib aliomba bunge lijadili na kupitisha azimio la Katibu Mkuu wa CUF-Chama cha Wananchi Mhe. Seif Sharif Hamad ahojiwe na vyombo husika ili aeleze ni kwa nini hakufunga na kuwasilisha taarifa ya mahesabu ya Chama kwa mwaka wa fedha wa serikali ulioishia Tarehe 30/6/2016 na kueleza ni wapi zilopo takriban Tshs. bilioni 2 zinazodaiwa kulipwa kwa CUF Chama cha Wananchi kutoka ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa Nchini, Jaji Francis Katabazi Mutungi.

3.      kwa bahati mbaya Lipumba na genge lake wamerukia suala hilo na kulitafsiri kama kutowajibika kwa wabunge hao wa CUF-Chama cha Wananchi wakieleza kuwa eti wanalinda hadhi ya Maalim Seif na kushindwa kuwakilisha matatizo ya wananchi wa majimbo yao. Huu ni upotoshwaji wa hali ya juu wa dhamira njema ya wabunge hao ambayo lengo ni kulinda matumizi mabaya ya Ofisi za Umma na Fedha za walipa kodi ambao ni za Watanzania wote.

4.       Taarifa ya CAG imebaini kupelekwa 5% tu ya fedha iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika bajeti ya serikali ya mwaka 2017/2018. Kutopelekwa fedha za maendeleo kwenye majimbo ya wabunge hao kumewasababishia wapiga kura wao huduma mbovu na kuongezeka kwa kero. Mbunge anapohoji juu ya matumizi mabaya ya fedha za serikali na kukubali mtu yeyote ambaye anaonekana kuhusika na ubadhilifu wa fedha za umma ahojiwe na kuchukuliwa hatua, Mbunge huyo anastahili kupongezwa. Na huo ndio utekelezaji wa jukumu la msingi la kuisimamia na kuishauri serikali. 

5.      Ni ajabu akatokea mtu akabeza mchango adimu uliotolewa na wabunge hao na kuona posho na mishahara wanayolipwa ni hasara wakati akiwashangilia mazuzu wanaokaa bungeni kupiga makofi muda wote mithili ya mashabiki wa mchezo wa mpira wa Simba na Yanga.

6.      CAG kaeleza wazi kuwa Katibu Mkuu wa chama cha siasa ndiye anastahili kisheria kuwasilisha taarifa ya mahesabu ya Chama kwa ukaguzi. Kwa maana hakuna mbadala wa Katibu Mkuu kuhojiwa kuhusiana na taarifa za hesabu za chama cha siasa.  Ndio maana tunaungana na wabunge wote wanaotaka makatibu wa vyama vya siasa visivyowasilisha hesabu za vyama vyao kwa CAG kwa ukaguzi wahojiwe na panapo ushahidi wa ufisadi wawajibishwe.

7.      Ifahamike kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ibara ya 27(2) inamtaka kila raia kuwa mlinzi wa raslimali za Taifa pale inapotamka ifuatavyo ; "Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu,  na kuendesha uchumi wa Taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao”.

8.      Wabunge wa CUF-Chama cha Wananchi wametekeleza wajibu wao wanastahili kupongezwa. Na anayepaswa kuhojiwa ni yule mwenye dhamana na mamlaka ya kisheria kwa mujibu wa Katiba ya CUF ambaye ndiye Katibu Mkuu, Maalim Seif.  Mwizi wa fedha za umma mahala pake kwa kujieleza ni Mahakamani na wala si vinginevyo. Sakaya na wenzake wasubiri wakajieleze mbele ya Mahakama.

9.      Si jukumu jipya kulinda Hadhi ya Maalim Seif sharif hamad lazima ilindwe na kila mpenda haki na mpigania ukombozi wa nchi. Maalim seif ndiye Kiongozi na Katibu Mkuu wa CUF mgombea Urais aliyeshinda Uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 Zanzibar.

10.  Lengo na kazi za bunge sio kuwasilisha matatizo ya wananchi, ni kuisimamia serikali, kuishauri serikali na kuwawakilisha wananchi katika usiamamizi huo, kwa kuhoji pale inapobidi matumizi ya mali , fedha za umma. Kupanga bajeti ya serikali kwa niaba ya wananchi na kuisimamia matumizi yake.

11.  Ni mwaka mmoja sasa Wabunge wachache vibaraka na wasaliti wa CUF wamejipakazi ya kuitetea CCM ndani ya Bunge na kuacha jukumu lao la msingi kama Wawakilishi wa wananchi. Huku wakitafuta huruma na kujipendekeza ili waendelee kulindwa na vyombo vya Dolan a serikali ya CCM kwa uvamizi walioufanya ndani ya CUF.

12.  Ni hoja ya kitoto kudhani kuwa eti Umaarufu na Uimara wa kisiasa wa MAaalim seif Sharif Hamad upo dhahiri shahiri na haitaji eti kuishi kisiasa kwa kutumia Hoja ya wabunge wa CUF bungeni juu ya wizi wa Fedha za Ruzuku ya CUF uliofanywa na Lipimba, Jaji Mutungi na washirika wao.

13.  Lipumba, Sakaya na Kambaya mnapaswa kuwaomba radhi Watanzania kwa wizi wa Fedha za umma mlioufanya hali ya kuwa si Viongozi Halali wa CUF. Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lililoketi Tarehe 28/8/2016 liliwasimamisha uanachama na baadae Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Tarehe 27/9/2016 kuwafukuza uanachana aidha, Mkutano Mkuu Maalum wa Tarehe 21/8/2016 uliridhia MAAMUZI YA LIPUMBA KUJIUZULU NAFASI YA UENYEKITI WA CUF TOKA MWAKA 2015 AGOSTI 5.    

14.  KATIBU MKUU yupo Ofisini kwake MaKao Makuu ya Chama cha CUF Mtendeni, Unguja Zanzibar akiendelea na Majukumu yake ya kila siku kama Kawaida. Kwa mujibu wa katiba ya CUF ibara ya 90 NA 93 Maalim Seif Sharif Hamad ndiye CHIEF ACCOUNTING OFFICER na wala si vinginevyo.

15.  SEHEMU YA SABA YA KATIBA YA CUF INAELEZA UWEPO WA VIONGOZI WA KITAIFA NA KAZI ZAO IBARA YA (90). Nanukuu “Kutakuwa na Viongozi Wakuu Kitaifa wa Chama wafuatao:- (a) Mwenyekiti wa Taifa,  (b) Makamu Mwenyekiti, (c) Katibu Mkuu. Katiba ya CUF imeeleza Katibu mkuu wa Chama na kazi zake kuwa ni pamoja na; Ibara ya (93) Kutakuwa na Katibu Mkuu wa Chama ambaye atachaguliwa na Mkutano Mkuu wa Taifa na atakuwa na majukumu yafuatayo:- 93 (a) Atakuwa Mtendaji Mkuu wa Chama na pia mwajibikaji mkuu wa shughuli zote za utendaji za Chama Kitaifa. 93(i) Atakuwa mwajibikaji mkuu wa mambo yote ya fedha na mali za Chama katika ngazi ya Taifa (CHIEF ACCOUNTING OFFICER).

Aidha,
16.  IBARA YA 125 (r) YA KATIBA YA CUF INAELEZA “Viongozi Wakuu wa Kitaifa” NI KINA NANI; HII ina maana ya Mwenyekiti wa Taifa, Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu wa Chama. MSISITIZO: HAKUNA NA WALA HAIKUELEZWA KUWA NAFASI YA “KAIMU KATIBU MKUU” HAPA KUWA NI KIONGOZI MKUU WA KITAIFA. HATA KAMA KWELI KATIBU MKUU ANGEKUWA HAYUPO.

“KAIMU KATIBU MKUU SI CHEO CHA KIKATIBA KWA MUJIBU WA KATIBA YA CUF”

17.  Hoja ya msingi ni kushindwa Kuwasilisha taarifa ya fedha kwa CAG kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 na 2017/2018 kutokana na fedha hizo kuingia mifukoni mwa watu na kushindwa kuwa na vielelezo  [Returns/Supporting Docoments] za matumizi yake kwa ajili ya Ukaguzi. Mathalani Tshs. Milioni 300 zilizoingizwa katika Akaunti Na.2072300456 ya benki ya NMB tawi la Temeke na baadae kuingizwa katika akaunti ya mtu binafsi Na.41401600207 ya NMB Handeni yenye jina la Mhina Masoud Omary. JE KWA MAZINGIRA HAYA unapeleka nini kwa CAG kwa ajili ya UKAGUZI?

18.  Hoja ni kwamba Msajili Mutungi alimjulisha Katibu Mkuu kwa barua ya Tarehe 10/10/2016 na kusitisha kutoa Ruzuku ya CUF kutokana na Mgogoro uliokuwepo. Wakati huo hata huyo anayeitwa Kaimu Katibu Mkuu hayupo wala hajulikani alipo. Msajili Mutungi hajawahi kumjulisha Katibu Mkuu kuwa sasa anaanza kutoa Ruzuku ya CUF kuifuta barua yake ya awali. Januari 6, 2016 akaingiza fedha kiasi cha Tshs milioni 369 kwa akaunti ya wilaya ya CUF NMB tawi la Temeke bila Katibu Mkuu kujua.  Sula la msingi la kujiuliza Je huo Mgogoro umemalizika?

19.  Pia hoja si imetumika vizuri au vibaya. Hoja fedha za Ruzuku zimezuiliwa na Mahakama Kuu kutolewa. Ni vipi Msajili Mutungi alizitoa fedha hizo? Je alikuwa anapata asilimia ngapi ya mgawo wa fedha hizo?

20.  Tumeona Sakaya na genge lake wanakimbilia katika Hoja ya matumizi ya Tshs milioni 600 za Mkutano Mkuu wa Mwaka 2016 huu ni upuuzi uliopevuka. Hoja ni Tshs Bilioni 2 zilizotolewa na Jaji Mutungi kati ya January 2017 mpaka May, 2018. Lakini pia Haijapata kutokea Tanzania mtu kununua kesi ya UFISADI kama alivyofanya Sakaya, hii yote ni kutaka kuficha wizi wa fedha za umma uliofanywa na Lipumba, Mutungi na Sakaya, Masoud Muhina na washirika wao.

21.  Kwa nini hesabu za CUF hazijakaguliwa na CAG? Lipumba na genge lake wameshindwa kuwasilisha Taarifa ya fedha za wizi walizopokea toka kwa Msajili Jaji Mutungi.

Mwisho:

Tunaitaka Serikali ya awamu ya Tano kama kweli inajinasibisha na kusimamia Rasilimali za Taifa kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Khatibu, Wabunge wa CUF, na Spika wa Bunge kufanya ukaguzi lazimishi wa fedha za Umma na Jaji Mutungi, Maalim Seif, Lipumba na genge lake wahojiwe wamezipeleka wapi Bilioni 2 za Chama cha CUF katika kipindi hiki ambapo mashauri yanaendelea Mahakamani.

CUF NI TAASISI IMARA YENYE VIONGOZI MAKINI

HAKI SAWA KWA WOTE

____________________________________
MBARALA MAHARAGANDE
NAIBU MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI
NA MAHUSIANO NA UMMA
MAWASILIANO: 0784 001 408/0715 062 577

No comments:

Post a Comment