TANGAZO


Thursday, January 18, 2018

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MREJESHO WA KIKAO CHA BARAZA LA VYAMA VYA SIASA

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Bw. John Shibuda
 
BARAZA la vyama vya siasa nchini limeazimia kwa kauli moja kuwa mjadala wa mapendekezo ya Sheria na Kanuni mpya ya vyama vya siasa, utaanzia kwenye kamati ya Sheria na Utawala Bora, ambayo itajadili mapendekezo ya bango kitita  yaliyokusanywa kutoka kwa wadau mbalimbali  na pia kamati itakuwa na jukumu la kukusanya upya maoni ya mapendekezo ya kutunga sheria na kanuni mpya ya vyama vya siasa.
 
Kauli hiyo ilitolewa kwenye kikao cha kawaida cha Baraza la vyama vya siasa wakati wa kujadili ajenda ya mapendekezo ya Sheria na Kanuni mpya za vyama vya siasa, kilichofanyika leo kwenye ukumbi wa Mkwawa, katika Ofisi ndogo za Bunge Jijini Dar es Salaam.
 
Aidha Kamati hiyo imepewa muda wa mwezi moja wa kuweza kukamilisha mchakato huo, kisha kuwasilisha kwenye Baraza la vyama vya siasa kwa maboresho na wajumbe wakisharidhia yatawasilishwa kwa mamlaka husika kwa ajili ya kukamilisha utaratibu wa utungaji wa Sheria na Kanuni mpya ya vyama vya siasa.
 
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Bw. John Shibuda alisisitiza kuwa kwa sasa Sheria na Kanuni za vyama vya siasa zilizopo zitaendelea kutumika hadi hapo zitakapotungwa Sheria mpya.
 
Pia  Baraza la vyama vya siasa limefanya Uchaguzi wa viongozi wa kamati nne za Baraza la vyama vya siasa. Kila kamati imejipatia mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti ambao wataongoza kamati hizo kwa muda wa miaka miwili ambayo ni kwa mujibu wa sheria.
 
Miongoni mwa viongozi waliochaguliwa ni Bw. John Momose Cheyo kutoka chama cha UDP ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Bw.Salum Mwalimu kutoka chama cha CHADEMA ambaye ni Makamu Mwenyekiti.
 
Kwa upande wa Kamati ya Bunge na Siasa, Mwenyekiti ni Bw. Juju Martin Danda kutoka chama cha NCCR-Mageuzi na Makamu Mwenyekiti ni Mohamed Masoud Rashid kutoka chama cha CHAUMMA.
 
Bw. Hassan K. Almas kutoka chama cha NRA ambaye ni Mwenyekiti na Bw. Said Soud kutoka chama cha AFP ambaye ni  Makamu Mwenyekiti wataiongoza kamati ya Sheria na Utawala Bora wakati viongozi wa Kamati ya Maadili na Mahusiano ni  Bw.Mohammed Ali Abdullah kutoka chama cha Demokrasia Makini ambaye ni Mwenyekiti na Bw.Peter A. Magwira kutoka chama cha DP ndiye Makamu Mwenyekiti.


Viongozi wa kamati za Baraza la vyama vya siasa huchaguliwa kwa kupigiwa kura ya siri na wajumbe wa kila kamati. Mwenyekiti akitokea upande mmoja wa Tanzania, Makamu Mwenyekiti atatokea upande mwingine wa Tanzania. Wenyeviti wa kamati za Baraza la vyama vya siasa, Mwenyetikiti wa Baraza la vyama vya siasa na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la vyama vya siasa ndio huunda kamati ya Uongozi ya vyama vya siasa.

No comments:

Post a Comment