TANGAZO


Saturday, November 25, 2017

WANAWAKE WATAKIWA KUSHIRIKI KATIKA MICHEZO

Waziri wa Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akifyatua bastola juu leo Jijini Dar es Salaam kuashiria Ufunguzi wa Mashindano ya Riadha kwa Wanawake kuelekea Olimpiki ya mwaka 2020 yatakayofanyika Tokyo nchini Japan.
Naibu Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Mhe.Juliana Shonza akizungumza leo Jijini Dar es Salaam katika Ufunguzi  wa Mashindano ya Riadha kwa Wanawake kuelekea Olimpiki ya mwaka 2020 yatakayofanyika Tokyo nchini Japan.Kulia ni Waziri wa Wizara hiyo  Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akimpongeza mshindi wa kurusha kisahani Bi. Mwanjala Abdala kutoka Dodoma wakati wa Mashindano ya Riadha kwa Wanawake kuelekea Olimpiki ya mwaka 2020 yatakayofanyika Tokyo nchini Japan yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Mhe. Juliana Shonza akimvalisha Medali ya ushindi mshindi namba mbili wa kurusha kisahani leo Jijini Dar es Salaam katika Mashindano ya Riadha kwa Wanawake kuelekea Olimpiki ya mwaka 2020 yatakayofanyika Tokyo nchini Japan. Kulia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa Bw. Mohamed Kiganja.
Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Dkt Mwakyembe na Naibu Waziri Mhe. Juliana Shonza wa Wizara ya Habari Sanaa na Michezo wakimvalisha medali ya ushindi mshindi namba moja wa kurusha kisahani Bi.Joyce Barnabas kutoka Dodoma leo Jijini Dar es Salaam katika Ufunguzi wa Mashindano ya Riadha kwa Wanawake kuelekea Olimpiki ya mwaka 2020 yatakayofanyika Tokyo nchini Japan.
Waziri Dkt. Mwakyembe na Naibu Waziri Mhe. Juliana Shonza wa Wizara ya Habari Sanaa na Michezo wakiwa katika picha ya pamoja na wanamichezo pamoja na wafadhili kutoka kampuni ya jiCA ya nchini Japan wanaoshiriki Mashindano ya Riadha kwa Wanawake kuelekea Olimpiki ya mwaka 2020 yatakayofanyika Tokyo Nchini Japan yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.Wa pili kushoto waliokaa ni Balozi wa Japan hapa nchini Mhe.Masahran Yoshida. 

Na Shamimu Nyaki-WHUSM
WANAWAKE nchini wametakiwa kushiriki katika Michezo mbalimbali kwani ni fursa nzuri ambayo inasaidia kupata ajira na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja pamoja na kuitangaza nchi kama ambavyo wanafanya wanamichezo wakiume.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe Dkt. Harrison Mwakyembe alipokuwa akizindua Mashindano ya Riadha kwa wanawake kuelekea Olimpiki ya mwaka 2020 yatakayofanyika Tokyo nchini Japan ambapo amewataka wanawake waliopata fusa ya kushiriki katika mashindano hayo kujituma zaidi na kujiamini ili wapate nafasi ya kushiriki katika Olimpiki hiyo na kuiletea heshima Nchi yetu.

“Leo vitaibuka vipaji vingi vitakavyosaidia nchi yetu kupiga hatua katika mchezo wa Riadha,nawaasa mjitume zaidi muwe na nidhamu pamoja na kujiamini ili mfanye vizuri katika mashindano haya hatimaye mpate nafasi ya kushiriki Olimpki ya  mwaka 2020 kule nchini Japan”.Alisema Mhe. Mwakyembe.

Aidha amewataka waamuzi wa mchezo huo kutumia vizuri taaluma yao kwa kufuata Sheria,taratibu na kanuni walizofundishwa na kutii kiapo walichoapa katika kuchezesha mchezo huo kwa kutoa matokeo sahihi na kwa wakati ili kuepusha manung’uniko.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe.Juliana Shonza amesema Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano kwa wanamichezo wote ambao wapo tayari na wanashiriki katika michezo mbalimbali kwani nia ya Serikali ni kukuza na kuendeleza Michezo hapa nchini.

“Ni fursa ya pekee kwenu vijana na wanawake kwa ujumla kutumia nafasi hii kuonyesha uwezo wenu katika michezo hii ili mpate nafasi ya kushiriki mashindano malimbali duniani na hatimaye mpate ajira itakayowezesha kutengeneza maisha yenu ya baadae.”Alisisitiza Mhe.Shonza.

Naye mwanariadha wa mbio za mita mia Bi. Winifrida Makenji kutoka Shule ya Sekondari Makongo ya Jijini Dar es Salaam ambaye ameingia katika fainali itakayochezwa hapo kesho amesema sifa kubwa ya yeye kufikia hatua hiyo ni kujiamini,kufanya mazoezi pamoja na kufuata maelekezo ya mwalimu.

Mashindano hayo yaliyofadhiliwa na Kampuni ya Ushirikiano ya Japan (jicA) yamehusisha michezo ya Riadha,kurusha mikuki pamoja na Kisahani ambapo yatamalizika kesho katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment