Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Bibi. Gaudencia Simwanza akiwasilisha mada wakati wa semina maalum kwa wajasiriamali wanawake iliyoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuelekea kilele cha maonesho ya viwanda vya Tanzania jana jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Frank Shija – Maelezo)
Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Bibi. Gaudencia Simwanza akigawa vipeperushi wakati wa semina maalum kwa wajasiriamali wanawake iliyoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuelekea kilele cha maonesho ya viwanda vya Tanzania jana jijini Dar es Salaam.
Na
Jacquiline Mrisho – Maelezo
MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) imetoa wito kwa wazalishaji wa bidhaa za chakula,
dawa, vipodozi na vifaa tiba kujiunga katika vikundi ili waweze kupata mafunzo kwa
urahisi pamoja na kusaidiana kiuchumi.
Gaudencia
amesema kuwa ni lazima kuchunguza kwa makini bidhaa mbalimbali zinazohusisha
afya ya binadamu kwa ajili ya kudhibiti
ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa hizo ili zisiweze kumdhuru mtumiaji hivyo,
mamlaka hiyo haijawekwa kwa bahati mbaya bali ina madhumuni thabiti ya kulinda
afya ya watumiaji wa bidhaa hizo.
“ili
kuhakikisha bidhaa hizo ni salama kwa afya ya mtumiaji ni lazima kuhakikisha
tunatoa elimu na mafunzo kwa wazalishaji
ili waweze kuzalisha kulingana na utaratibu mzuri uliowekwa ndio maana
tunawashauri wajiunge kwenye vikundi ili iwe rahisi kupata elimu pamoja na kupata
nafasi kubadilishana mawazo yanayohusu uzalishaji wa bidhaa zao,” alisema Bi
Gaudencia.
Afisa
Mahusiano huyo ameongeza kuwa, kwa kuwa sifa ya kwanza ya kusajiliwa katika
Mamlaka hiyo ni kuwa na jengo la uhakika na salama kwa ajili ya kuzalishia
bidhaa hizo, hivyo uundaji wa vikundi vya pamoja utasaidia wazalishaji kutafuta
fedha kwa pamoja kwa ajili ya kupata jengo kwani wazalishaji wengi wamekua
wakilalamika kukosa fedha kwa ajili ya jengo la kufanyia shughuli hizo.
Amefafanua
kuwa mbali na vikundi hivyo, Mamlaka hiyo imekua ikitoa elimu kwa wajasiliamali
mbalimbali kupitia ofisi za za kanda zilizopo katika Mikoa 7 nchini ikiwemo ya
Kanda ya Ziwa, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Mashariki, Magharibi,
Kaskazini, Kusini na Kanda ya Kati.
Amewasisitiza
wajasiriamali wote wanaozalisha bidhaa zinazohusisha afya ya binadamu kusajili
majengo yao pamoja na kusajili bidhaa zao ili kupata Hati ya Usajili wa Jengo
pamoja na kibali cha kutengenezea bidhaa hizo mara baada ya kukamilisha
taratibu zote zilizoainishwa kisheria.
TFDA
ni taasisi iliyopo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto iliyoundwa kwa ajili ya kusimamia na kuhakikisha bidhaa zinazohusika
na afya ya mtumiaji zinatengenezwa katika hali ya usafi na usalama.
No comments:
Post a Comment