TANGAZO


Friday, October 7, 2016

WAZIRI UMMY ATOA MISAADA KWA WAATHIRIKA WA TETEMEKO MKOANI KAGERA, AAHIDI KUPELEKA WATAALAMU KUFANYA TATHMINI ILI KUEPUSHA MAGONJWA YA MLIPUKO

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu akitoa taarifa kwa Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kuhusu hatua iliyofikiwa na serikali katika kurejesha hali baada ya tetemeko lilitokea mkoani humo ambapo pia alimshukukuru Waziri Ummy kwa Misaada aliyoitoa wakati wanakabiliana na maafa ikiwemo, Madawa, Vifaa tiba na madktari iliyowezesha kusaidia kwa kiasi kikubwa waathirika wa tetemeko.(Picha zote na Eluteri Mangi-Maelezo) 
Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiongea na Mkuu wa Mkoa wa Kagera na kuipongeza kamati ya mkoa kwa namna walivyojipanga kukabiliana na athari za tetemeko pamoja na kuwahudumia waathirika. 
Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu misaada iliyotolewa na Bohari ya Madawa (MSD) waliotoa Dawa na Vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 30. 
Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu mashuka 250 yaliyotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Na Eleuteri Mangi-Maelezo
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameahidi kutuma timu ya wataalam kutoka Idara ya Magonjwa ya Mlipuko ili kuja kushirikiana na timu ya Mkoa ili kufanya tathmini ili kuweza kuepusha magonjwa ya mlipuko hasa katika kipindi hichi ambacho mvua zimeanza kunyesha mkoani humo.

Akiongea wakati akikabidhi misaada kwa mkoa wa kagera Meja jenerali Mstaafu Salum Kijuu Waziri Ummy amesema anatambua kipindi hiki cha mvua huwa ni tishio kwa magonjwa ya mlipuko hivyo wizara itachukua hatua ya kutuma wataalam pamoja na kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na magonjwa hayo.

“Nafahamu tuko kwenye kipindi cha mvua nyingi ambacho mara nyingi magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu huibuka, hivyo kabla ya hayo kutokea kama tahadhari sisi kama wizara tutatuma wataalam kuja kufanya tathmini na kutoa elimu ya namna ya kujikinga” Alisema Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy amekabidhi misaada ya Dawa na Vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 30 vilivyotolewa na Bohari kuu ya Dawa (MSD) kwa mkuu wa mkoa wa kagera Meja jenerali Mstaafu Salum Kijuu kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko mkoani humo.

Pia Waziri Ummy amekabidhi mashuka 250 yaliyotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa ajili ya Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati mkoani kagera.

Akiwa katika ziara kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko la ardhi Waziri Ummy amewataka watumishi katika sekta ya afya mkoani humo kuweka mkakati wa kuweka mazingira safi kwenye maeneo yote yaliyoathiriwa na tetemeko.

Wakati huo huo Waziri Ummy ametembelea Kituo cha kulea wazee na watu wasiojiweza cha Kiilima kilichopo katika Halmashauri ya Bukoba na kuagiza wazee hao kupatiwa chakula cha milo mitatu ili kulinda afya zao.


Akizungumza baada ya kupokea misaada hiyo mkuu wa mkoa wa kagera Meja jenerali Mstaafu Salum Kijuu amewaomba wadau wengine kuendelea kutoa misaada kwa ajili ya kurejesha hali baada ya maafa kutokea.

No comments:

Post a Comment