TANGAZO


Friday, October 7, 2016

MAWAZIRI WA FEDHA WAJADILI NAMNA YA KUPAMBANA NA UTAPIAMLO NA UDUMAVU WA AKILI WA WATOTO

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt. Philip Mpango (wa kwanza kushoto), akisikiliza kwa makini hotuba ya Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Jim Yong Kim, katika mkutano  uliowahusisha Mawaziri wa Fedha kutoka nchi kadhaa duniani kama vile Cameroon, Ethiophia, Senegal na Indonesia ambapo rais huyo aliwataka mawaziri hao wasimamie rasilimali fedha vizuri  hasa katika suala la kukabiliana na changamoto ya utapiamlo na udumavu wa akili kwa watoto waliochini ya umri wa miaka mitano, mkutano uliofanyika Jijini Washington DC, Marekani. 
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiwasilisha hotuba kuhusu ni jinsi gani Tanzania imejipanga kukabiliana na tatizo la utapiamlo na udumavu wa akili kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano, alipomuwakilisha Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Jijini Washington DC, Marekani. 
Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Jim Yong Kim akimpogeza Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, baada ya kuwasilisha hotuba kwa niaba ya Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo kuhusu watoto kupata lishe bora wakati wa kuzaliwa na kusisitiza wakinamama wanyonyeshe watoto ipasavyo ili kuondokana na tatizo kubwa la utapiamlo ambalo mara nyingi huwakumba watoto wanapokuwa wadogo na kusababisha kupoteza nguvu kazi ya Taifa, Jijini Washington DC. 
Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Jim Yong Kim akiwa na Mawaziri wa Fedha wa Afrika akiwemo na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philiph Mpango(wa nne kutoka kulia),Jijini Washington DC. 
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (kushoto), akibadilishana mawazo na baadhi ya wajumbe wengine.

Benny Mwaipaja, MoFP,Washington DC
7.10.2016
MAKAMU wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Benki ya Dunia na wadau wengine wa maendeleo kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha ili kutatua changamoto ya utapiamlo na udumavu wa akili kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano kwenye nchi masikini na zinazoendelea ili kujenga kizazi chenye afya kwa maendeleo endelevu ya mataifa hayo.

Makamu wa Raisa metoa wito huo, Mjini Washington, Marekani kwenye hotuba iliyosomwa kwaniaba yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, wakati wa mkutano ulioandaliwa na Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Jim Kim, ulioshirikisha Mawaziri wa Fedha na wadau wengine kutoka nchi zaidi ya 180 wanaoshiriki mkutano wa Mwaka wa Benki hiyo na Shirika la Fedha Duniani (IMF )

Amesema kuwa licha ya Tanzania kufanikiwa kupunguza utapiamlo na kiwango cha udumavu kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka 5 kutoka asilimia 42 hadi kufikia asilimia 34, bado idadi kubwa ya watoto wanaokadiriwa kufikia milioni 2.7 wamedumaa akili huku wengine laki sita wakikabiliwa na utapiamlo mkali.

Mhe.Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kwa kutambua changamoto hiyo,, Serikali imepanga kutumia kiasi cha dola milioni 115, sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 254, kukabiliana na tatizo hilo katika kipindi cha miaka mitano kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa miaka Mitano, kuanzia mwaka 2016/2021.

Ameitaka jumuiya ya Kimataifa kuunga mkono juhudi za mataifa masikini na zinazoendelea ili kuwaokoa mamilioni ya watoto wanaokabiliwa na tatizo hilo hivyo kuathiri mustakabali wa watoto kielimu na kimaisha.

Kwa upande wake Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Jim Kim, amesema kuwa asilimia 43 ya watoto waliochini ya umri wa miaka mitano wanaokadiriwa kufikia milioni 250 katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati wamedumaa na kukabiliwa na utapiamlo mkali unaoletwa na umasikini pamoja na ukosefu wa elimu kuhusu umuhimu wa kuwapatia watoto lishe bora na unyonyeshaji wa maziwa ya mama.

Ameahidi kuwa Benki hiyo itatenga fedha kupitia miradi mbalimbai inayotekelezwa kwa ufadhili wake na kushirikisha sekta binafsi ili lengo la kunusuru watoto katika hali hiyo ya utapiamlo na udumavu wa akili liweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Ameyataka Mataifa kuwekeza fedha katika ujenzi wa miundombinu ya sekta ya afya, elimu, maji, na usalama wa chakula, kuwajali na kuwapenda watoto ili malengo ya kukomesha tatizo hilo, yafikiwe kama yalivyopangwa. 

No comments:

Post a Comment