TANGAZO


Tuesday, October 4, 2016

BALOZI SEIF IDDI AKABIDHIWA HATI MAALUM YA HESHIMA NA UVCCM ZANZIBAR KWA UONGOZI BORA

Naibu Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Tanzania Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Uongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM Zanzibar uliofika kumkabidhi hati maalum ya heshima kwa kuuongoza vyema umoja huo. Wa kwanza kulia kwa Balozi Seif Iddi ni Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar  Ndg. Abdulgharaf  Idriss Juma na kushoto kwa Balozi Seif wa kwanza ni Mkuu wa Utawala wa Umoja huo, Ndg. Salum Simai Tale. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar,  Ndg. Abdulgharaf  Idriss Juma (kushoto) akimkabidhi Naibu Kamanda wa UVCCM Tanzania Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi hati maalum ya heshima kwa kuuongoza vyema umoja huo. Hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar.

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
04/10/2016.
NAIBU Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Tanzania Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi aliwaasa vijana wa Umoja huo ambao ndio muhimili wa CCM kuhakikisha kwamba Viongozi watakaopatikana kwenye uchaguzi ujao wa Chama hicho wanakuwa na uwezo unaokubalika na wanachama watakaowaongoza.

Alisema Tabia ya kuchagua viongozi kwa kutumia vigezo vya nasaba, urafiki au uwezo wa kifedha huzua balaa na malalamiko ya wanachama ndani ya kipindi kifupi baada ya uchaguzi huo na hatimae kupunguza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya  Ilani na Sera za Chama hicho.

Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alitoa nasaha hizo wakati akizungumza na Uongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM Zanzibar ukiongozwa na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar  Nd. Abdulgharaf  Idriss Juma mara baada ya kupokea Hati Maalum ya Heshima kwa kuwa mlezi mwema wa Jumuiya hiyo kikao kilichofanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Alisema Chama cha Mapinduzi kimechoshwa na tabia za baadhi ya wanachama wake wanaojenga tamaa ya kujipenyeza ndani ya fursa za Uongozi wanazoomba kwenye nafasi mbali mbali jambo ambalo baadaye huleta usumbufu na maudhi kwa wale waliowachagua ili wawatumikie.

Balozi Seif alitahadharisha kwamba wanachama wa Chama cha Mapinduzi wanapaswa kuwa makini kuwapima wale wote wanaoomba nafasi za Uongozi kwa vigezo vya kuangalia Historia ya kila anayeomba nafasi hizo.

Naibu Kamanda huyo wa UVCCM upande wa Zanzibar aliwahimiza Vijana na Umoja huo kuendelea kujenga uchumi kwa lengo la kuiongezea nguvu Jumuiya kuendesha mambo yake.

Alisema kutokana na mabadiliko ya dunia yaliyopo hivi sasa si vyema kwa vijana wenye nguvu,uwezo na maarifa ndani ya Jumuiya hiyo kuendelea kuendesha majukumu yao kwa kusubiri kutegemea ruzuku kutoka Makao Makuu ya Chama chao.

Aliwapongeza Viongozi na Wanachama wa UVCCM kwa kutekeleza vyema majukumu yao ndani ya kipindi cha miaka Mitano iliyopita ambapo Umoja huo bado ukiwa ni chombo madhubuti kinachoendelea kuipa sifa CCM hasa wakati Taifa linapojiandaa kuingia kwenye  chaguzi mbai.

Balozi Seif  aliwahimiza Vijana waendelee kushirikiana kwa kuacha majungu, fitna na wawe kitu kimoja katika kukijengea uwezo wa kuendelea kushinda Chama cha Mapinduzi katika chaguzi zote zijazo.

Alitahadharisha wazi kuwa ipo mifarakano mingi inayoshuhudiwa kutokea katika baadhi ya vyama vya siasa Nchini ambayo Vijana na wana CCM wanapaswa kujifunza kutokana na makosa ya vyama hivyo.

Mapema Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM  Tanzania Zanzibar  Nd. Abdulghafar Idriss Juma alisema Umoja  huo uko makini kwa upande wa Kisiasa na Uchumi tokea kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa Zanzibar na ule wa Tanzania.

Hata hivyo Nd. Abdulghafar alisema zipo baadhi ya changamoto zilizojitokeza ndani ya kipindi hicho lakini haziwezi kuepukika kutokana na hulka za udhaifu wa wanaadamu.

Alisema Uongozi wa Umoja wa Vijana hivi sasa umekusudia kukaa na watumishi wake kujadili mipango ya kujiandaa na matembezi ya mshikamano ya kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 kutimia miaka 53.

Kaimu Naibu Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Vijana wa CCM Tanzania Zanzibar alisisitiza kwamba Umoja huo utaendelea kuyaenzi Mapinduzi hayo yaliyomkomboa mnyonge wa Visiwa vya Unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment