Yusta Jonas mkazi wa Hamugembe Manispaa ya Bukoba akipokea rambirambi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu ambayo imetolewa na Serikali pamoja na kampuni ya simu za mkononi ya Halotel.
Mzee Vedasto Kato kutoka mtaa wa Hamgembe Manispaa ya Bukoba akipokea rambirambi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu ambayo imetolewa na Serikali pamoja na kampuni ya simu za mkononi ya Halotel.
Mkuu wa Mkoa wa
Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu (katikati aliyekaa) akiwa katika picha
ya pamoja na wawakilishi wa wanafamilia waliofiwa na ndugu zao wakati wa
tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, mwaka huu.
Na Eleuteri Mangi,
Maelezo, Bukoba
FAMILIA 15 zilizofiwa
na ndugu zao 17 wakati wa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani wa Kagera zimepokea
rambirambi ya jumla ya shilingi milioni 32 ikiwa ni mkono wa faraja kwa msiba
uliwafika familia hizo na taifa kwa ujumla.
Rambirambi hiyo
imetolewa mjini Bukoba na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum
Kijuu kwa niaba ya Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya simu za mkononi
nchini ya Halotel ili kuwashika mkono wafiwa hao kwa kupoteza ndugu na jamaa
zao.
Katika rambirambi
hiyo, Serikali imetoa shilingi milioni 17 na kampuni ya simu ya Halotel imetoa
shilingi milioni 15 ambapo kila familia ya mfiwa amepokea shilingi 1,000,000 kutoka
Serikalini na shilingi 885,000 kutoka kampuni ya Halotel.
Hatua hiyo inapelekea
kila familia ya mfiwa kupokea jumla shilingi 1,885,000 ambapo familia mbili
zilizopoteza ndugu zao wawili wawili wamepokea jumla ya shilingi 3,770,000
ikiwa ni rambirambi kwa kila ndugu aliyefariki wakati wa tukio hilo la tetemeko
la ardhi.
Akikabidhi rambirambi
hiyo kwa familia hizo, Mkuu wa Mkoa wa huo akiwa pia Mwenyekiti wa Kamati ya
Maafa mkoa Meja Jenerali Mstaafu Kijuu amesema kuwa Serikali imetoa rambirambi
hiyo kwa lengo kuwapa pole wafiwa hao kutokana na kuwapoteza ndugu na jamaa zao
wakati wa tetemeko hilo lililotokea
Septemba 10, mwaka huu.
Katika kuwahakikishia
usalama na utunzaji wa fedha walizopokea wafiwa hao, Mkuu wa mkoa huo amewaasa wasikuwa
na akaunti wafungue akaunti katika benki yeyote ili waweze kuziweka fedha hizo walizopokea
ili kuwahakikishia usalama badala ya kutembea nazo mkononi.
Wawakilishi wa familia
zilizopokea rambirambi hiyo ni pamoja na Vedasto Katto (Hamugembe), Geofrey
Gerald (Mafumbo), Alex Felix (Hamugembe), Orestus Aron (Hamugembe), Justa
Mkalisa Jonas (Hamugembe), Albert Tibangayuka (Barabara ya Sokoine), Sheikh
Mikidadi Abdallah (Hamugembe) na Maria Stella John (Hamugembe).
Wanafamilia wengine
waliopokea rambirambi ni Swidick Miyonga (Hamugembe), Jackson Evason
(Rwamishenye), Jasson Rugemalila (Rwome), Augustine Muhigi (Rwome), Edson S.
Rwetabula (Kashenye), Anitha Evalista (Omurushaka) na John Mulokozi Kahangwa (Kanyigo-Kikukwe).
Aidha, mkuu huyo wa
mkoa ameishukuru Kampuni ya simu ya mkononi ya Halotel kwa kuunga mkono juhudi
za Serikali katika kutoa rambirambi na kuwafuta machozi familia za marehemu hao
na kuwahakikishia kuwa Serikali inathamini mchango wao kwa jamii.
Akitoa neno la
shukrani mara baada ya kupokea rambirambi hiyo kwa niaba ya wafiwa wenzake,
Mzee Vedasto Kato kutoka mtaa wa Hamgembe Manispaa ya Bukoba ametoa shukrani kwa
Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuona haja ya
kuwashika mkono baada ya kupoteza ndugu zao.
“Tunaishukuru
Serikali kwa kutujali wafiwa tuliopoteza ndugu zetu wakati wa tetemeko la ardhi
lililotokea katika mkoa wetu mwezi huu na kutuonea huruma katika kipindi hiki kigumu
kilichotuachia majonzi makubwa katika familia zetu” alisema mzee Vedasto.
Mzee Vedasto amesema
kuwa hatua iliyochukuliwa na Serikali katika kuwapa mkono wa pole imewapa faraja
na ameiomba Serikali kuendelea kuwajali wananchi wake kama ilivyokuwa kwao.
Tetemeko la ardhi lilitokea
mkoani Kagera mapema mwezi huu, limesababisha vifo ambapo wananchi 17
waliopoteza maisha yao, majeruhi 440 ambao walitibiwa katika vituo mbalimbali
vya afya pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Pamoja na rambirambi
hiyo, Serikali pia iliwahudumia marehemu waliopoteza uhai wakati wa tukio hilo
kwa kutoa majeneza pamoja na usafiri wa kusafirisha miili ya marehemu hao
kutoka Bukoba mjini hadi kwenye maeneo ambayo familia zao walipo ambapo yalipofanyika
maziko ya wapendwa wao.
No comments:
Post a Comment