TANGAZO


Friday, August 28, 2015

Tume ya Uchaguzi kuwachulia hatua kali za Kisheria wananchi waliojiandikisha zaidi ya mara moja katika Daftari la kudumu la Wapiga kura

Mkuu wa Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dkt. Sisti Cariah (katikati) akiwaonyesha waandishi wa habari utaratibu wa uhifadhi wa fomu za taarifa za wananchi waliojiandisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, jana, Alhamisi (Agosti 27, 2015)Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Kombwey
Ofisa TEHAMA katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Adolf Kinyelo akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu mfumo uhifadhi wa taarifa za wananchi katika daftari la kudumu la wapiga kura jana, Alhamisi (Agosti 27, 2015) Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Kombwey. 
Mkuu wa Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dkt. Sisti Cariah akitoa  ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu uhakiki wa taarifa za wananchi katika daftari la awali la wapiga kura jana, Alhamisi (Agosti 27, 2015) Jijini Dar es Salaam. 
Watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), David Charles (kushoto) na Ikabodi Chimoto wakichapisha nakala za daftari la awali la uhakiki wa taarifa za wananchi waliojiandisha katika Daftari la wapiga kura jana, Alhamisi (Agosti 27, 2015) Jijini Dar es Salaam. 
Mtumishi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Hassani Shamo akihakiki  taarifa za wananchi waliojiandisha katika la wapiga kura jana, Alhamisi (Agosti 27, 2015) Jijini Dar es Salaam. 
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Kombwey akimkabidhi Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi (ACP) Benedict Wakulyamba daftari maalumu lenye taarifa za wanachi waliojiandisha zaidi ya mara wakati wa zoezi la uandikishaji wa wananachi katika daftari la kudumu la wapiga kura katika sehemu mbalimbali nchini jana, Alhamisi (Agosti 27, 2015) Jijini Dar es Salaam . 
1.    Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC), Kailima Kombwey akiwaoyesha waandishi wa habari daftari maalum lenye taarifa za wanachi waliojiandisha zaidi ya mara wakati wa zoezi la uandikishaji wa wananachi katika daftari la kudumu la wapiga kura katika sehemu mbalimbali nchini jana, Alhamisi (Agosti 27, 2015) Jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Ismail Ngayonga) 

Na Anitha Jonas- MAELEZO.
Dar es Salaam
27.08.2015
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka wananchi 52,078 waliojiandisha kwa zaidi ya mara moja katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia mashine za kieletroniki (BVR) wajisalimishe mara moja katika Ofisi za Tume hiyo au kwa Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kabla ya hatua kali za kisheria kuchuliwa dhidi yao.

Aidha NEC inatarajia kuyakabidhi majina ya watu wote waliowekewa pingamizi ya uraia wakati wa zoezi la uandikishaji wananchi katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa Idara ya Uhamiaji kwa ajili ya uthibitisho wa uraia wao hapa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Alhamisi Agosti 27, 2015, Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Kombwey amesema Ofisi yake imekabidhi orodha ya majina hayo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Ernest Mangu kwa ajili ya kuwachulia hatua mbalimbali za kisheria dhidi ya wananchi hao.

Kwa upande Kamshina Msaidizi wa Jeshi la Polisi (ACP), Benedict Wakulyamba alisema Ofisi yake imeyapokea majina hayo na itaanza mara moja zoezi la uchuguzi ikiwemo kuwahoji watuhumiwa hao ili kujua sababu ni ya kufanya vitendo hivyo kinyume na sheria ya uchaguzi.

Akizungumzia zoezi la uandikishaji wapiga kura katika mfumo wa BVR lililomalizika hivi karibuni nchini, Kombwey alisema NEC imeandikisha zaidi ya wananchi milioni 23.7 nchi nzima kwa kutumia mfumo wa  BVR, ambapo taarifa zao zimehifadhiwa katika sehemu tano ambazo ni BVR Mashine, kompyuta mpakato (Laptop), Kadi ya kumbukumbu (VCD) na diski mweko (flash disk) pamoja na kifaa maalum cha kuweka taarifa (Server).

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa uchaguzi alisema katika kila kitambulisho cha mpigakura kilichotolewa na mfumo wa BVR kina taarifa mbalimbali ikiwemo za NEC na sehemu aliyojiandikisha, tarehe aliyojiandikisha, na namba BVR  mashine iliyotumika kujiandikisha pamoja majina la mwandishaji, hivyo kwa wale wanaosema kuna vitambulisho bandia vimekamatwa ni vyema  waviiwasilishe katika ofisi ya NEC kwa ajili kuvifanyia uchunguzi au uhakiki.

Katika hatua nyingine, Kombwey alitoa ufafanuzi juu ya suala la vyama vya siasa kuzingatia ratiba zao za kampeni, pamoja na kuwepo na mgongano wa taarifa kuhusu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kunyimwa uwanja wa jangwani kwa ajili ya kufanyia uzinduzi wa kampeni zao Agosti 29, mwaka huu.

“Vyama vyote vya siasa vilikuwa na uongozi wa NEC na kujadili juu ya ratiba zao za kampeni na Chadema walisema uzinduzi wa kampeni zao ni tarehe 29/08/2015 katika jiji la Dar es Salaam lakini hawakuonyesha ni wapi watafanya kampeni hizo ila kama wameambiwa uwanja wa jangwani umeshachukuliwa basi watafute uwanja mwingine katika eneo lolote la ndani ya jiji la Dar es salaam”, alisema Kombwey.


Naye Mkurugenzi wa Tehama wa NEC Dkt. Sisti Kariah alisema Tanzania ni nchi ya tatu katika Bara la Afrika kutumia mfumo wa BVR na mfumo huo ni mzuri kwani una uwezo mkubwa ikiwemo uhifadhi wa taarifa zote zilizoandikishwa katika mfumo huo.

No comments:

Post a Comment