Mwanahabari kutoka Uganda, Nancy Kacungira ni mshindi wa Tuzo la kwanza la kumuenzi aliyekuwa mtangazaji wa BBC, Komla Dumor.
Tuzo hilo BBC World News Komla Dumor Award, lina lengo la kuendelea kuimarisha uandishi wa habari kuhusu Afrika.
Mtangazaji huyu wa kituo cha televisheni cha KTN cha Kenya,alichaguliwa miongoni mwa washiriki wapatao 200.
Mshindi huyo atakuwa makao makuu ya BBC, mjini London kwa miezi mitatu na pia kutuma taarifa za habari za BBC Televisheni , radio na mtandao kutoka barani Afrika.
Tuzo hilo lilianzishwa ili kumuenzi Komla Dumor, mtangazaji wa BBC, aliyeaga dunia ghafla akiwa na umri wa miaka 41.
Bi Kacungira alisema: " nimeshtushwa, lakini pia kufurahishwa sana kwa kupokea habari hizi.
Nimepokea kwa unyenyekevu mkubwa ushindi wa tuzo hili".
"Hili ni tuzo la bara hili ninalolipenda na ambalo nimejitolea kulihudumia, kwa kutekeleza jukumu langu la kutoa taswira halisi ya bara ambalo kwa muda mrefu taarifa zake zimekuwa zikipotoshwa na kuongezewa chumvi.'
"Kuwa sehemu ya kumbukumbu ya Komla ni heshima kubwa, nikama ndoto.''
''Nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu ili kuthibitisha uaminifu niliyoonyeshwa kwa kupewa tuzo hilo.''
'Pia nitahakikisha kwamba mazao yake hayanifaidi mimi tu".
Wahariri wamsifu
Mmoja ya waamuzi, Mhariri wa habari, wa Idhaa ya BBC Afrika, Vera Kwakofi,alimsifu bi Kacungira.
'' Nancy ni mwerevu sana na ana upeo mpana wa mawazo na ujuzi unaojitokeza mara moja."
"Nimefurahi kwamba katika Nancy tumempata mwanahabari mwenye kipaji na ari,
''mtu anayestahili kuwa mshindi wa tuzo tulilolianzisha kwa jina la Komla."
Nancy amekulia Uganda ambapo alihitimu kutoka chuo kikuu cha Makerere, mjini Kampala.
Ana ujuzi wa zaidi ya miaka 14 katika fani ya uwanahabari kwani amefanya kazi katika mshirika kadha ya habari nchini Kenya, Uganda na Tanzania.
Pia ana shahada ya uzamifu katika mawasiliano kutoka chuo kikuu cha Leeds.
Kwa wakati huu yeye ni mtangazaji wa habari za usiku za Kiingereza katika kituo cha televisheni cha KTN na pia ni mhariri wa mtandao wa Kijamii wa shirika hilo.
Washiriki wawili waliibuka nambari mbili: Leila Dee Dougan kutoka Afrika Kusini na Paa Kwesi Asare kutoka Ghana.
Komla hasahauliki
Komla Dumor alikuwa mtangazaji raia wa Ghana mwenye kipaji cha kipekee ambaye katika maisha yake mafupi alikuwa na mvuto wa ajabu nchini Ghana, Afrika na ulimwenguni.
Aliwakilisha ule upande wa Afrika wa ujasiriamali na umahiri.
Kutokana na uwanahabari wake dhabiti na kipaji chake cha kuelezea habari kwa uweledi mkubwa , Komla alifanya kazi bila kuchoka ili kutoa taswira halisi ya Afrika kwa ulimwengu.
BBC inashukuru shirika la Standard Chartered na wahisani wengine kwa misaada yao.
No comments:
Post a Comment