Na Lilian Lundo-MAELEZO
MAFANIKIO ya utekelezaji wa mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), nchini Tanzania yamevutia nchi nyingi za Jumuiya ya Madola ambazo zimeomba kuja kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa katika mpango huo.
Hayo yalisemwa na Mtendaji Mkuu wa BRN, Ndugu Omari Issa alipokuwa akiongea na waandishi wa habari baada ya kufungua mkutano mkuu wa wakuu wa utumishi wa umma wa Jumuiya hiyo jana katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julius K. Nyerere jijini Dar es Salaam.
Issa alisema wawakilishi kutoka Uganda wanatarajia kuja kujifunza mafanikio ya mfumo wa BRN baada ya wiki moja au moja na nusu kuanzia huku nchi za Pakistani, Cameroon na Peru zinatarajia kuja kujifunza mfumo huo hapa nchini.
Aliongeza kuwa Tanzania imepongezwa kwa kuwa nchi ya mfano katika Jumuiya ya Madola baada ya kufanikiwa katika kutekeleza mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
“Huu mfumo umeleta matokeo mazuri ambapo uwajibikaji umeongezeka, ufanisi matokeo yapo na mambo katika sekta zilizoingizwa katika mfumo huoyanaendelea, umeme vijijini na maji vijijini vinaonekana” Alisema Ndugu Omari Issa.
Ndugu Omari aliongezea kwa kusema kwamba la muhimu Tanzania ijivunie kwa kuwa imeleta mfumo unaoleta uwajibikaji, uwazi na una utekelezaji ambao umewezesha miradi kufikia malengo.
Mkutano huo wa siku 3 ulihudhuriwa na nchi 15 za Jumuiya ya Madola kati ya nchi 18 zinazounda jumuiya hiyo, huku Tanzania ikiwa ni mwenyeji.
No comments:
Post a Comment