Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akimkabidhi mchango wa Shilingi 400,000/- kwa kila kikundi miongoni mwa vikundi 14 vya Ushirika wa Akina Mama vilivyomo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “ A “.
Balozi Seif akikabidhi Seti moja ya Jezi na Mipira kwa kila Timu ya Soka miongoni mwa timu nne zilizomo ndani ya Jimbo la Matemwe.
Balozi Seif akiangalia hodhi linalojengwa kwa ajili ya kuhifadhia maji kwenye Msikiti Mkuu wa Kijiji cha Mvuleni Kidoti Jimbo la Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Balozi Seif akiuagiza Uongozi wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Kijiji cha Mvuleni kufanya Tathmini ya uenzi wa Vyoo ili uwahi kufunguliwa katika muda muwafaka uliopangwa. (Picha zote na Hassan Issa– OPMR – ZNZ)
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
14/4/2015.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewakumbusha wananchi hasa akina mama nchini kuwaunga mkono viongozi wenye mwelekeo wa kuwasimamia vyema katika harakati zao za maendeleo, kiuchumi na ustawi wa Jamii.
Alisema takwimu ya idadi ya watu Nchini inaoonyesha wazi kwamba Wanawake ndio wenye uwezo wa kutumia kura zao katika kuchaguwa Viongozi watakaowafaa kwenye maeneo yao kutokana na wingi wao.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kumbusho hilo wakati akikabidhi Vipaza Sauti kwa ajili ya Jumuiya ya Kuhifadhi Quran pamoja na Sherehe za Siku Kuu ya Kiislamu ya Kijiji cha Matemwe Wilaya ya Kaskazini “A” Mkoa wa Kaskazini Unguja akitekeleza ahadi aliyoitowa wakati wa Siku Kuu ya Mfunguo Tatu uliopita akiwa mgeni rasmi.
Hafla hiyo iliambatana pia na Balozi Seif kukabidhi seti za Jezi na Mipira kwa Timu Nne wa Jimbo la Matemwe ambapo Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi akakabidhi fedha taslim kwa baadhi ya vikundi 14 vya Ushirika vya Akina Mama wa Wilaya ya Kaskazini “A” vifaa vyote vikiwa na thamani ya shilingi Milioni 7,860,000/-.
Balozi Seif alisema huu ni mwaka muhimu kwa Taifa la Tanzania ambapo Wananchi wanapaswa kuwa makini katika kufanya uamuzi muafaka wa kura ya maoni pamoja na uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba.
Alisema uwamuzi wa Wananchi hao endapo hautazingatia hatma yao ijayo ya miaka mitano kwa kuchaguwa viongozi makini na imara wasijetafuta visingizio vya lawama kwa viongozi watakaowaweka madarakani.
Mapema Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akitekeleza ahadi yake ya kuviwezesha Baadhi ya Vikundi vya Ushirika vya akina Mama wa Wilaya ya Kaskazini “A “ alisisitiza umoja na mshikamano miongoni mwa Wananchi wa Wilaya hiyo.
Mama Asha alisema mshikamano huo ndio njia pekee itakayowawezesha wananchi hao kuendelea na shughuli zao za kujitafutia riziki katika hali ya amani na utulivu.
Alitanabahisha kwamba yapo Mataifa kadhaa duniani yakiwemo yale ya Bara la Afrika ambayo baadhi ya wananchi wake walijaribu kuichezea amani na hivi sasa tayari wameshatumbukia katika dimbwi la vurugu zilizozaa maafa yaliyoacha makovu yatayoendelea kukumbukwa milele na Mataifa hayo.
Baadhi ya Vikundi vipatavyo 14 vya ushirika wa akina Mama wa Wilaya ya Kaskazini “ A “ vilikabidhiwa fedha taslim shilingi Laki nne kila kimoja ambavyo ni Lamoyoni hulioni, Apewaye hupokea, Atowaye Allah pamoja na Riziki Haiwanwi.
Vyengine ni Hatujali Kitu, Tumia Jasho lako, Tushukuru Mungu, Haraka Sio Mwendo, Kheir Liwe, Tumia Jasho Lako,Wema Si Maneno, Wema wa Maskini hauna sifa, Mtaji wa Maskini pamoja na Mwanzo Mgumu.
Timu wa Mpira wa miguu zilizokabidhiwa seti za Jezi na Mipira ni pamoja na Kikobweni United, Mabundi Sports Club, Kilima Juu Sports Club pamoja na Chimbuko Sports Club.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipata fursa ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Kijiji cha Mvuleni Kidoti Jimbo la Nungwi.
Balozi Seif ambae aliridhika na hatua iliyofikiwa ya ujenzi huo aliuagiza Uongozi wa Msikiti huo kufanya tathmini ya makisio ya ujenzi wa vyoo vya Msikiti huo ili kukamilisha kazi yote.
Ufunguzi Rasmi wa Msikiti huo wa Ijumaa wa Mvuleni Kidoti unatarajiwa kufanywa hivi karibuni na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Braza la Mapinduzi Al – Hajj Dr. Ali Mohammed Shein.
No comments:
Post a Comment