Washiriki wa Mafunzo wakifuatilia hotuba ya ufunguzi ya ufunguzi wa kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (hayupo pichani) kushoto ni Bw. Denis Mongula kutoka Ofisi ya Mwnasheria Mkuu wa Serikali
Washiriki wa Mafunzo wakifuatilia kwa makini mada kuhusu Sheria Dhidi ya Utakatishaji fedha haramu ya mwaka 2006 iliyowasilishwa na Bw.Robert Kassim (hayupo pichani)
Bi Rhoda Martin ,Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Dodoma akitoa neno la shukrani mara baada ya mafunzo hayo kufunguliwa rasmi.
Picha ya pamoja ya washiriki wa mafunzo kuhusu utakatishaji
fedha haramu na utaifishaji mali zilizopatikana kwa njia zisizo halali. Kutoka
kushoto waliokaa ni Bw. Ayub Mwenda, Mkurugenzi Msaidizi (uendeshaji
Mashtaka), Bw. George Masaju-Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi Mary Lymo-Mkurugenzi
Msaidizi (Makosa ya Rushwa na Udanganyifu) na kulia ni Bw. Angaza
Mwipopo, Wakili wa Serikali Mfawidhi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa
wa Dodoma.
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI kwa kushirikiana na wadau wa
mapambano ya kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu na utaifishaji wa fedha
zilizopatikana kwa njia isiyo halali imeendelea kufanya jitihada katika
kuongeza uelewa na kujenga uwezo wa Watendaji wake pamoja na kuendelea kuweka
mifumo ya Kisheria na Kiutawala kupambana na kudhibiti makosa yanayohusu
utakatishaji wa fedha haramu na utaifishaji wa mali iliyopatikana kwa njia ya
uhalifu.
Hatua hizo zimefikiwa kutokana na kuendelea
kuimarika kwa mbinu zinazotumiwa na wahalifu katika kutenda vitendo vya
kihalifu, vikiwemo vitendo vya kutakatisha fedha haramu, ambazo zimekuwa
zikibadilika kila siku, na hivi sasa wahalifu wanatumia maendeleo yaliyoletwa na
Sayansi na Teknologia kupitia kompyuta
na njia ya Teknolojiaya ya Habari na
Mawasiliano kutenda makosa ya uhalifu yanayozalisha fedha haramu.
Katika kutekeleza azma yake hiyo,
Serikali imeandaa Mswada wa Sheria ya Miamala ya Kielekroniki wa Mwaka 2015 (The Electronic Transaction Bill, 2015) na Mswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao wa Kompyuta ya Mwaka 2015 (The Computer and Cyber Crimes Bill, 2015) ambayo
itawasilishwa katika Mkutano wa 19 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ikiwa ni
mkakati wake wa kuendelea kupambana na
kudhibiti makosa yanayohusu utakatishaji fedha haramu na utaifishaji mali
zilizopatikana kwa njia isiyo halali.
Vilevile, Serikali imeendelea
kuchukua hatua ya kuwajengea uwezo
wataalamu ili kuimarisha uwezo wao katika utekelezaji wa Sheria Dhidi ya Utakatishaji Fedha Haramu ya mwaka 2006, ambapo
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, leo (18 Machi,2015) amefungua mafunzo ya pamoja
yanayowahusisha Waendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
pamoja na washiriki kutoka Mahakama na
Vyombo vya Upelelezi nchini ili
kuwawezesha watendaji hao kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko
katika mazingira na mbinu mpya za kutenda makosa hayo.
Akieleza umuhimu wa mafunzo hayo, Ndugu
Masaju amesema kuwa uelewa wa watendaji wengi katika vyombo vya Uchunguzi,
Uendeshaji Mashtaka na Mahakama kuhusu masuala haya bado ni mdogo
hivyo kulazimika kuchukua hatua na jitihada katika kuongeza uelewa pamoja na
ukweli kwamba zipo Sheria mahsusi za Makosa haya na nyinginezo kama Sheria
Dhidi ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 1984 ambazo zimeweka masharti ya utaifishaji
wa mali zinazotokana na uhalifu na Sheria Dhidi ya Utakatishaji wa Fedha Haramu
ya 2006 inayotambua makosa mengine (predicate
offences) yanayozalisha fedha haramu.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametumia
fursa hiyo kuwasihi washiriki wa mafunzo
hayo kutolala kwani wahalifu wako macho na wanatumia njia mpya kila siku kutenda
uhalifu ambapo kumekuwa na ongezeko la makosa ya rushwa, madawa ya kulevya na
udanganyifu ambayo yanachochewa na tamaa ya kupata mali.
“Ni vizuri mkafahamu bayana kuwa iwapo mtalala, wahalifu kwa upande wao,
hawasubiri Serikali iweke mifumo ya kudhibiti au kujenga uwezo wa watendaji
wake. Kinyume chake, wanatumia mwanya huo kutenda uhalifu na kutakatisha mali
zinazotokana na uhalifu huo ili isiwe rahisi kuwakamata na kutaifisha mali
hizo”.
Ndugu Masaju pia ameeleza kuwa
wahalifu wanatumia fursa iliyoletwa na
maendeleo ya mifumo ya Mawasiliano na Teknolojia (TEHAMA) katika biashara
mbalimbali kutakatisha fedha zinazopatikana
kwa njia ya uhalifu na kuzisafirisha haraka katika nchi
nyingine ili kuficha uhalisia wa mali hizo kwa dhamira ya kuepuka kukamatwa na vyombo vya uchunguzi
hapa nchini ambapo ametoa rai kwa washiriki wa mafunzo kutumia vizuri fursa
waliyoipata kujifunza na kupata majibu ya changamoto mbalimbali wanazokabiliana
nazo katika utendaji kazi ili kuongeza kuongeza ufanisi na kuhakikisha wahalifu
hawafaidiki na uhalifu wanaoufanya.
Awali, akimkaribisha Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Bw.Ayub Mwenda ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi anayeshugulikia
Usimamizi na uratibu wa uendeshaji wa Mashtaka ya Jinai kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali alieleza kuwa Serikali
inatoa uzito mkubwa katika suala la kukabiliana
na uhalifu na mashauri yanayohusu masuala ya utakatishaji fedha hivyo nguvu na uelewa wa pamoja vinahitajika kutoka
kwa wadau wote ikiwa ni pamoja na
kuendelea kushirikiana ili kujiimarisha zaidi katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment