TANGAZO


Tuesday, March 24, 2015

Msimu wa Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) 2015 wazinduliwa

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, Pamela Kikuli, akizungumza na waandishi wa habari, wakati wa uzinduzi wa Tuzo ya Mwanamuziki Bora ya Kili Music Award, Dar es Salaam jana. Kushoto ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Godfrey Muingereza. (Na Mpigapicha wetu)

Na Mwandishi wetu 
Dar es salaam 23, 2015. 
Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kwa kushirikiana na Kilimanjaro Premium Lager leo wamezindua rasmi msimu mwingine wa tuzo za muziki Tanzania unaojulikana kama Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA). Uzinduzi huu ulifanyika kwenye ukumbi mpya wa LAPF uliopo barabara ya Ali Hassan Mwinyi jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Meneja wa bia ya Kilimanjaro, Bi. Pamela Kikuli amesema muda wa kuwatunza wasanii wa muziki waliofanya kazi nzuri zilizokubalika na wengi umewadia. “Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, ni bia ya watanzania, na imejikita katika kuwaletea burudani na pia kutoa majukwaa ambayo yanawapa Watanzania fursa ya kukuza vipaji mbalimbali, likiwemo jukwaa la muziki la Kilimanjaro Tanzania Music Awards.” Aliendelea “Na hii tumeithibitisha kwa juhudi za makusudi za kutenga fungu kubwa na kuongeza ushiriki wa wataalaam mbali mbali kwenye fani husika ili kuziendeleza, kuzikuza na kuziongezea thamani tuzo hizi mwaka hadi mwaka sambamba na umaarufu kuongezeka kwenye medani za Kimataifa.”

Kilimanjaro Premium Larger inawekeza zaidi ya billion moja shilingi za ki Tanzania kuhakikisha ubora wa hali ya juu unajitokeza kwenye mchakato mzima wa tuzo hizi. “Bia ya Kilimanjaro itaendelea kuwekeza kwenye mambo yetu na kuyasimamia kikwetu kwetu!” Pamela Kikuli.

Msimu huu hauna mabadiliko makubwa sana katika vipengele wala mfumo wa kuwapata wateule, bali kuna maboresha kwenye njia za upigaji kura ili kuongeza ufanisi na pia kuendeleza utaratibu wa kufanya mambo yetu ya KTMA ki kwetu kwetu. Kwa mfano Tanzania sasa inawatu zaidi ya milioni mbili na laki tano kwenye whatsapp, KTMA imewarahisishia kwa kuongeza njia hiyo kwenye mchakato wa kupendekeza na kupiga kura.

Mchakato wa kuwapata wateule utapitia ngazi mbali mbali hadi kuwapata washindi na kutangazwa kwenye usiku wa utoaji tuzo.

Ratiba ya KTMA 2015:


Tukio
Mwezi
Tarehe
1
Uzinduzi
Machi
23
2
Mchakato wa Mapendekezo/Entries
Machi/Aprili
30/19
3
Academy
Aprili
25
4
Kutangaza wateule
Aprili
27
5
Semina ya Wateule
Aprili
30
6
Kura za ushindi
Mei
 1-31
7
Gala Night
Juni
13

Upande mwingine BASATA ilitangaza kuanza kwa kura za mapendekezo kutoka kwa wapenzi wa muziki nchini. “Kama tulivofanya mwaka jana na mwaka huu Tanzania itatoa maoni ya nani aingie kwenye kinyang’anyiro.” Alisema Katibu Mtendaji wa BASATA Nd. Godfrey Mngereza.

Kura za maoni zitaanza tarehe 30/Machi hadi 19/Machi 2015. Shabiki ataweza kupendekeza nani ama nyimbo zipi ziwemo kwenye vipengele vyote vya KTMA 2015. Kwa mfano: Wimbo bora wa mwaka, shabiki wa muziki ana nafasi ya kupendekeza nyimbo zote tano ambazo anaona ni bora na zina kidhi vigezo vya BASATA kwa mwaka 2015. “Ni muhimu kuelewa kwamba mapendekezo yote ni lazima yatokane na vigezo vya BASATA. Kama wimbo haukupata umaarufu, haukushika chati, haukupigwa kwenye vyombo mbali mbali vya burudani (yaani media channels), hauwezi kuwa na vigezo vya kupendekezwa’ alisema Bw. Mngereza.

Kura mwaka huu kwenye ngazi zote zitapigwa kwa njia kuu tatu; mtandao, Whatsapp na SMS. Njia zote hizi zitahitaji namba hai ya simu ili kukamilisha zoezi. Kipindi cha kupiga kura za kuchagua washindi utaratibu wa namba moja ya simu kupiga kura moja utaendelea. Haijalishi njia ipi mpiga kura atatumia lakini namba moja kura moja kwa kipengele kimoja. “Ukipigia kura kipengele kwa njia ya whatsapp, hautaweza kuipigia kura tena kipengele hicho kwa kutumia SMS au kwenye mtandao”. Alifafanua Pavel Gabriel wa Auditax International.

Njia za kupiga kura ni kama zifwatazo:

  1. Whatsapp – 0686 528 813.
  2. SMS – 15415.
  3. Mtandao – www.ktma.co.tz
BASATA wameendelea kusisitiza usimamizi wa maingizo ya nyimbo kuendelea kufanywa kwa umakini mkubwa na kwa kushirikiana kwa karibu zaidi na AUDITAX INTERNATIONAL – kampuni inayosimamia mchakato mzima. Katibu Mkuu wa BASATA alisisitiza kwamba ‘Kama kuna wimbo ulifungiwa na BASATA hautaruhusiwa kushiriki kwenye mchakato’ BASATA.


Katibu Mkuu wa BASATA amehimiza mashabiki wa muziki watumie fursa kuwapendekeza wasanii wanaowashabikia kazi zao kwenye vipengele husika kuanzia tarehe 30.03.2015. BASATA wameshauri kuzingatia vigezo vya kila kipengele ambavo vitachapishwa kwenye magazeti na kuwekwa kwenye mitandao mbali mbali.

No comments:

Post a Comment