Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete
Na Anna Nkinda – Maelezo, Masasi
20/3/2015
WANAFUNZIwa kike wilayani Masasi wametakiwa kuachana na tamaa za maisha zinazowapelekea kujiingiza katika mapenzi kabla ya wakati na hivyo kupata ujauzito unaowasababisha kukatiza masomo yao.
Ushauri huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wananchi wakiwemo wanafunzi waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya gari la wagonjwa la Hospitali ya Mkomaindo iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo.
Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuna baadhi ya wanafunzi wanapenda maisha mazuri wakati wazazi wao hawana uwezo na hivyo kujiingiza katika mapenzi ili wapate fedha zitakazowafanya wanunue vitu wanavyohitaji.
“Wengine mnadiriki kufanya mapenzi na watu wazima waliowazidi umri msifanye haya mambo kabla ya wakati. Ridhikeni na maisha ya wazazi wenu matokeo yake mtapata mimba na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
“Nawasihi wanangu msiruhusu mazingira ya kupata mimba mkiwa shuleni bali someni kwa bidii na kufanya vizuri katika masomo yenu kwa kufanya hivyo mtakuwa na maisha mazuri hapo baadaye. Wavulana walindeni dada zenu ili wasidanganywe na wanaume, nanyi pia someni muache tabia ya utoro hii itasaidia kuwa na Masasi ya wasomi”, alisisitiza Mama Kikwete.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Maendeleo ya Wilaya ya Masasi bado kuna tatizo kubwa la wanafunzi wa kike kuacha shule kutokana na ujauzito. Mwaka 2013 wanafunzi 35 walipata ujauzito na mwaka 2014 waliopata ujauzito ni 22 na hivyo kukatiza masomo yao.
Akisoma taarifa hiyo Mkuu wa wilaya ya Nanyumbu ambaye ni Kaimu Mkuu wa wilaya ya Masasi Sauda Mtondoo alisema kupungua kwa idadi ya wanafunzi wanaopata ujauzito ni kutokana na kuanzishwa kwa vilabu vya wapinga mimba mashuleni na watuhumiwa wote wa tukio hilo kufikishwa mahakamani na kesi zao zinaendelea.
“Changamoto tunazokutana nazo ni walezi kutotoa ushirikiano kwa vyombo vya sheria pindi watoto wao wanapopata ujauzito, kesi nyingi zinamalizwa kinyemela, watuhumiwa kutoweka pindi wanapohusishwa na ujauzito wa mwanafunzi husika”, alisema Mtondoo.
Mkuu wa wilaya huyo aliitaja mikakati waliyonayo ni kutoa elimu kwa watoto ili wazielewe stadi za maisha, kuimarisha kitengo cha ushauri na unasihi katika shule za sekondari kwa kuwa na walimu na malezi na kuanzishwa kwa klabu za wasichana katika shule zote za Sekondari kwa mantiki ya kupunguza utoro na mimba za utotoni.
Wilaya hiyo ina jumla ya shule za sekondari 37 kati ya hizo za Serikali ni 35 na binafsi mbili na shule za msingi 159 zenye wanafunzi 68,316.
Na Anna Nkinda – Maelezo, Ruangwa
20/3/2015
MKE wa Rais Mama Salma Kikwete ametoa msaada wa madawati 100 kwa shule ya msingi Mnacho iliyopo kijiji cha Ng’au wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi ambayo alifanya mazoezi ya kufundisha kwa vitendo (BTP) wakati akiwa mwanachuo wa chuo cha Ualimu Nachingwea.
Mwishoni mwa mwaka jana Mama Kikwete ambaye kitaaluma ni mwalimu na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alitembelea shuleni hapo na kukuta kuna upungufu mkubwa wa madawati na kuamua kutoa msaada huo ili uweze kukabiliana na tatizo hilo.
Akiongea na wananchi waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya madawati hayo Mama Kikwete aliwasihi wazazi kuhakikisha watoto wao wanakwenda shule, wanasoma na kufaulu katika mitihani yao kwani elimu ni mkombozi wa maisha.
Alisema elimu ni haki ya mtoto hivyo basi wazazi wafuatilie na kuhakikisha watoto wao wanasoma hadi ngazi ya elimu ya juu.
“Naamini kupatikana kwa madawati haya kutaondoa tatizo la watoto kubanana katika madawati yaliyokuwepo. Nawasihi waleteni watoto shule wasome kwani hivi sasa kuna madawati ya kutosha”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ruangwa ambaye ni Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Kassim Majaliwa alimshukuru mama Kikwete kwa msaada wa madawati aina ya plastiki ngumu aliyoyatoa kwa shule hiyo.
Waziri Majaliwa alisema kutokana na changamoto ya upungufu wa madawati uliokuwepo katika shule hiyo Mama Kikwete alimpatia shilingi milioni tano kwa ajili ya kununua madawati 100 ili yaweze kutatua tatizo hilo.
Akisoma taarifa ya shule ya Msingi Mnacho Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa Stephano Ngondo alisema shule hiyo ilianzishwa mwaka 1932 na wamisionari ikiwa inatoa elimu ya msingi na baadaye kurudishwa chini ya usimamizi wa Serikali mwaka 1963 na kuendelea kutoa elimu hiyo mpaka sasa.
Shule hiyo inawanafunzi 371 kati ya hao 177 ni wavulana na 194 wasichana na walimu 10 kati yao wanawake sita na wanaume wanne, vyumba vya madarasa 10 na nyumba za walimu mbili.
Ngondo alisema, “Idadi ya uandikishaji wa wanafunzi shuleni hapo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka na ufaulu umeongezeka. Kwa mwaka 2014 jumla ya wanafunzi 27 walifanya mtihani wa kumalia elimu ya msingi kati ya hao 22 sawa na asilimia 81.84 walifaulu na kujiunga na kidato cha kwanza.
Alizitaja changamoto zinazoikabili shule hiyo ni uhaba wa nyumba za walimu, uchakavu wa vyumba vya madarasa, uhaba wa vyoo vya kudumu hasa vilivyokuwepo kutitia, umiliki wa eneo la shule kwani eneo ambalo shule ipo linamilikiwa na kanisa Katoliki Parokia ya Mnacho na uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Wakati huo huo Mama Kikwete akiwa wilayani Ruangwa alifanya mkutano na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuongea nao mambo mbalimbali yahusuyo chama hicho.
Mama Kikwete ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) wilaya ya Lindi mjini aliwahimiza wajumbe waliohudhuria mkutano huo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftati la kudumu la wapiga kura na kuipigia kura ya ndiyo katiba inayopendekezwa.
“Wakati ukifika mkajiandikishe katika daftari la kudumu la wapiga kura na mvitunze vitambulisho vyenu msivitupe kwani ndivyo vitakavyotumika kuipigia kura ya maoni katiba inayopendekezwa na kuchagua viongozi wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu”, alisisitiza Mama Kikwete.
No comments:
Post a Comment