Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete
Na Anna Nkinda – Maelezo, Masasi
20/3/2015
JAMII imehimizwa kuhamasisha kinamama wajawazito kujifungua katika vituo vya afya ambako watasaidiwa na wakunga wenye ujuzi kwa kufanya hivyo vifo vya kinamama na watoto wachanga vinavyotokana na tatizo la uzazi vitapungua.
Mwito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wananchi waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya gari la wagonjwa la Hospitali ya mji wa Masasi ilijulikanayo kwa jina la Mkomaindo iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo.
Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema mtoto wa kike akibeba mimba katika umri mdogo, mama mjamzito asipohudhuria kliniki mapema na kwa muda uliopangwa na kutojifungua katika vituo vya afya mama anaweza kupata matatizo ikiwa ni pamoja na kupotea maisha wakati wa kujifungua.
“Wanaume mnapaswa kuunga mkono juhudi hizi katika kipindi cha ujauzito kina mama waondolewe majukumu ya kazi nzito muwe nao karibu, wahurumieni na kujiepusha na aina yoyote ya unyanyasaji. Wawezesheni wake zenu kuhudhuria kliniki na kupima ujauzito kipindi chote cha ujauzito na ifikapo tarehe ya kujifungua wasindikize katika vituo vya afya.
“Pale watakapogundulika kuwa na matatizo ya kujifungua wapeni ushirikiano wa kutosha ikiwemo rasilimali fedha kwa ajili ya huduma yoyote ya rufaa itakayohitajika”, Mama Kikwete alihimiza.
Kwa upande wa vifo vya watoto alisema hutokana na kutokuwa na uwezo kama vile fedha za kumpeleka mama mjamzito aliyeshindwa kujifungua, kumuwahisha mtoto Hospitali mara apatapo matatizo kama vile ya kupumua, homa, na kuharisha.
Mama Kikwete alisema , “Huduma ya gari la dharula la wagonjwa ni muhimu sana katika kuokoa maisha ya watu. Taarifa za kila siku zinaonyesha ni jinsi gani kina mama wajawazito wanapoteza maisha kutokana na kucheleweshwa kufika katika vituo vya afya”.
Aidha Mwenyekiti huyo wa WAMA aliupongeza uongozi wa wilaya hiyo na watumishi wa sekta ya afya kwa kupunguza kasi ya maambukizi ya VVU kutoka asilimia 5.07 hadi kufikia 2.13 kwa mwaka 2014 ukilinganisha na mwaka 2013 ambapo kasi ya maambukizi ilikuwa asilimia 7.13.
Akisoma taarifa ya Idara ya afya Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya mji wa Masasi Dkt. Albano Nditi alisema katika mji huo kuna vituo nane vinavyotoa huduma ya afya ya uzazi na mtoto ambazo ni upimaji wa kina mama wajawazito na watoto, kuzalisha na ufuatiliaji wa makuzi ya watoto.
Dkt. Nditi alisema idadi ya wasichana wanaobeba mimba wakiwa na umri wa chini ya miaka 20 ni kubwa hali hiyo inatokana na uelewa mdogo wa jamii juu ya athari za kubeba mimba katika umri mdogo. Pia asilimia 55 ya wanawake wajawazito wanaoanza kliniki hawakamilishi mahudhurio yote manne kwani waliowengi huanza kliniki wakiwa wamechelewa.
Alifafanua, “Kwa mwaka 2014 kina mama waliojifungua katika vituo vya kutolea huduma ni ni 4,762 kati ya hao wenye umri wa chini ya miaka 20 ni 1541 na zaidi ya miaka 20 ni 3,221. Waliojifungulia majumbani na kwa wakunga wa jadi ni 278 kati ya hao wenye umri wa chini ya miaka 20 ni 68 na zaidi ya miaka 20 ni 210”.
Vifo vilivyotokana na uzazi kwa mwaka jana vilikuwa 22, tatizo la vifo vya uzazi bado ni kubwa hii inatokana ana uhaba wa watumishi wenye ujuzi, mahudhurio duni ya kina mama Kliniki, kuchelewa kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya wakati wa kujifungua na uhaba wa vifaa kwenye wodi ya wazazi”.
Alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni upungufu wa madaktari, wauguzi wenye ujuzi, maafisa afya mazingira na madereva, upungufu wa magari ya kubebea wagonjwa, upungufu na uchakavu wa majengo, uhaba wa vitanda na mashuka katika wodi za wagonjwa na ukosefu wa vituo vya kutolea huduma za afya katika baadhi ya maeneo hasa yaliyo pembezoni mwa mji.
Kuhusu Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) Dkt. Nditi alisema jumla ya kaya 274 kati ya 28,875 zilizopo katika mji huo zimejiunga na mfuko hali hiyo inatokana na mwitikio na uelewa mdogo kutoka kwa wananchi juu ya kujiunga na huduma hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Masasi Andrew Mtumusha alimshukuru Mama Kikwete kwa msaada wa gari alilowapatia na kusema kuwa litaokoa vifo vingi vya wakinamama wajawazito, watoto na wanaume ambavyo vinatokea pale ambapo mgonjwa anacheleweshwa kufikishwa Hospitali kubwa kutokana na tatizo la usafiri.
“Ninakupongeza kwa moyo wa huruma na upendo ulionao, nakuomba uendelee kutukumbuka zaidi na zaidi kwenye mambo mbalimbali. Nina kuahidi gari hili litatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa ya usafirishaji wagonjwa bila upendeleo wowote”, Mtumusha alishukuru.
Taasisi ya WAMA iliamua kukabidhi gari hilo liliopatikana kwa kushirikiana na Shirika la Sayeed Corporation katika Hospitali ya Mkomaindo kutokana na wakina mama wengi kuhitaji huduma ya usafiri ili waweze kufika Hospitali kwa wakati na uwepo wa huduma ya mama na mtoto ambayo inatolewa mahali hapo.
No comments:
Post a Comment