TANGAZO


Monday, March 16, 2015

Maadhimisho ya Wiki ya Maji Mkoa wa Dar es Salaam yazinduliwa rasmi

*Wananchi watakiwa kulinda na kutunza miundombinu
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Said Meck Sadiki akitoa ufafanuzi kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Maji mkoani Dar es salaam. (Picha zote na Aron Msigwa-Maelezo)
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Said Meck Sadiki akizindua mradi wa Maji ya Kisima mtaa wa Mongolandege, Ilala jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Maji mkoani Dar es salaam. Mradi wa Kisima hicho umegharimu kiasi cha shilingi milioni 78. 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Said Meck Sadiki akifungua moja ya bomba la maji la mradi wa Maji ya Kisima mtaa wa Mongolandege, Ilala jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Maji mkoani Dar es salaam. 
Bi. Martha Singano, Mkazi wa Mongolandege akipokea ndoo ya maji kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Said Meck Sadiki mara baada ya  kuzindua  mradi wa Maji ya Kisima katika mtaa huo.

Na Aron Msigwa – MAELEZO.
16/3/2015.Dar es salaam.
TANZANIA inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Wiki ya maji kuanzia tarehe 16 hadi 22, Machi 2015 chini ya Kauli Mbiu isemayo Maji kwa Maendeleo Endelevu. 

Maadhimisho ya mwaka huu yanatoa fursa kwa Mamlaka zinazohusika na usimamizi wa Maji nchini kutathmini huduma wanayoitoa kwa wananchi, kujenga na kuimarisha miundombinu iliyopo katika maeneo mbalimbali nchini. 

Akizindua Maadhimisho ya Wiki ya Maji kwa mwaka 2015 katika Mkoa wa Dar es salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Said Meck Sadiki amesema maadhimisho hayo katika jiji la Dar es salaam pamoja na mambo mengine yataambatana na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) kuzindua miradi maji katika maeneo mbalimbali ya jiji, kutoa elimu kuhusu utunzaji wa vyanzo vya  maji, utunzaji wa miundombinu ya miradi inayojengwa, upokeaji wa maoni na kero za wananchi pamoja operesheni za kukamata baadhi ya watu wanaoiba na kuhujumu miundominu ya maji.

Amesema maadhimisho hayo  mkoani Dar es Salaam yatazindua miradi  ipatayo 9 na kuweka mawe ya msingi katika miradi 2 na kuongeza kuwa chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) mkoa unatekeleza jumla ya miradi 41 ya Visima vya maji katika wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke.

Mhe. Saidi Meck Sadiki ameseama miradi mingine 14 iliyojengwa chini ya ufadhili wa Serikali ya Ubelgiji (BTC) imekamilika na inaendelea kuwahudumia wananchi katika wilaya zote tatu za jiji la Dar es Salaam.

Amefafanua kuwa jiji la Dar es salaam linaongoza nchini kwa kuwa na mahitaji makubwa ya maji huku huduma ya Maji kwa wakazi hao  ikitolewa na Mamlaka ya Maji ya jiji la Dar es salaam (DAWASA) ambayo imekodisha shughuli za uendeshaji huduma kwa DAWASCO. Vyanzo vikuu vya maji katika jiji la Dar es salaam mto Ruvu, Kizinga pamoja na maji yanayopatikana chini ya ardhi.

Amesema mahitaji ya maji kwa wakazi wa jiji na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Pwani kwa sasa ni wastani wa lita 450 kwa siku huku uwezo wa kuzalishaji maji kwa siku ni lita 300  ambazo ni sawa na asilimia 66.7 ya mahitaji yote.  

Ameeleza kuwa upungufu huo unaosababishwa na uwezo mdogo wa mitambo na miundombinu ya kuzalisha maji na kuongeza kuwa Serikali kupitia sekta 6 zilizopewa kipaumbele chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, Maji yamepewa kipaumbele ambapo miradi ya maji 41 mkoani Dar es Salaam itatekelezwa ili kufikia lengo la Serikali la uzalishaji wa lita 710 ambazo zitakua  ni zaidi ya mahitaji mwishoni mwa mwaka 2015.

“Matarajio yangu na mkoa ninaouongoza ni kuhakikisha kuwa tunawapatia watu milioni 3.8 ambao ni asilimia 90 ya wananchi katika jiji la Dar es Salaam huduma ya majisafi na salama mwishoni mwa mwaka 2015” Amesisitiza.

Ameleza kuwa  DAWASA inatekeleza mpango maalum wa kuongeza upatikanaji wa maji jijini Dar es salaam kwa kupanua Mitambo ya Ruvu chini ambayo kazi yake imekamilika kwa asilimia 100, ujenzi wa bomba kuu kutoka Ruvu chini hadi chuo kikuu cha ardhi ambao umekamilika kwa asilimia 93, kazi ya upanuzi wa mtambo wa Ruvu juu na ujenzi wa bomba la maji hadi Kimara ambao umefikia asilimia 55 utakaokamilika mwezi Agosti, 2015.

Aidha, amesema kazi ya uchimbaji wa visima 20 katika awamu ya kwanza imeanza na itakamilika mwezi Agosti mwaka huu ikihusisha pia upanuzi wa mtandao wa usambazaji wa maji katika maeneo yaliyo kandokando ya mabomba makuu kutoka Ruvu chini na Ruvu juu na kunufaisha vitongoji vilivyopo kati ya mji wa Bagamoyo hadi eneo la Tegeta-Mpiji na vitongoji vilivyopo kati ya mji wa Mlandizi –Kiluvya na maeneo ya Mbezi, Kimara na Goba.

Awamu ya pili itahusisha upanuzi wa mfumo wa usambazaji wa maji katika maeneo yote ya jiji yatakayopata maji kutoka Kimbiji na Mpera na maeneo mengine ya jiji yasiyo na mabomba ya usambazaji.

Akitoa ufafanuzi kuhusu mradi wa visima vya dharula katika maeneo yasiyo na maji ya bomba amesema jumla ya visima 48 vimechimbwa katika maeneo mbalimbali ya jiji yakiwemo Kimara,Kimara, Kisukuru, Keko –Chang’ombe, Sandali, Mburahati, Mbagala, Mtoni, Kigamboni ,Gerezani na Ukonga

Katika hatua nyingine Mhe. Saidi Meck Sadiki ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria kwa baadhi ya watu wanaorudisha nyuma juhudi za Serikali za kuwapatia wananchi maji safi kwa kuhujumu miundombinu ya maji ya DAWASCO kwa kuendesha vitendo vya wizi wa maji, mambomba na miundombinu mingine.

Pia ameitaka DAWASCO na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kuanza kuwafuatilia na kuwadhibiti baadhi ya wafanyabiashara wanaowaibia wananchi kwa kununua maji ya DAWASCO kwa gharama nafuu ya shilingi 1 kwa lita na kuyauza kwa zaidi ya shilingi 50.

No comments:

Post a Comment