Mhandisi wa Kiwanda cha Matrekta Mbweni Haji Wa Haji Makame akimpatia Maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi moja ya Mashine zinazotumika Kiwandani hapo.
Balozi Seif akiangalia Mashine inayotumika katika uburugaji wa mashamba ya Mpunga.
Mkuu wa Kitengo cha Ufundi katika Kiwanda cha Matrekta Mbweni Mhandisi Moh’d Omar Moh’d (wapili kulia) akimueleza Balozi Seif juhudi za Kiwanda hicho licha ya utengenezaji wa vyombo vya moto lakini pia hutoa mafunzo ya Ufundi kwa vijana wanaomaliza masomo ya sekondari. Wa mwanzo kutoka Kulia ni Mhandisi mwenzake wa Kiwanda hicho Haji Wa Haji Makame. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
17/3/2015.
UKOSEFU wa fungu maalum la matumizi pamoja na upungufu wa vipuri vya utengenezaji wa vyombo vya moto katika Kiwanda cha Matrekta Mbweni ndio changamoto ya msingi inayosababisha watendaji wa kiwanda hicho kufanya kazi katika kiwango kisichoridhisha.
Mkuu wa Kitengo cha ufundi katika kiwanda hicho Mhandisi Moh’d Omar Moh’d alieleza hayo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefanya ziara ya ghafla kwenye karakana ya Kiwanda hicho kuangalia uwajibikaji wa watendaji hao hapo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mhandisi Moh’d Omar Moh’d alisema changamoto hiyo kubwa wakati mwengine hupelekea baadhi ya Taasisi za Umma na hata zile binafsi husita kupelekea vyombo vyao vya moto kwa ajili ya kupata huduma za matengenezo ya kiufundi.
Alisema Kitengo hicho licha ya kwamba hakina kifungu cha fedha lakini watendaji wake hulazimika kufanya kazi wakati wote kutegemea huduma wanazozipokea kituoni hapo hasa zile za Matrekta ya Wizara ya Kilimo na Mali Asili.
Alieleza kwamba Kiwanda hicho hivi sasa kimepokea Matrekta kadhaa kutoka Wizara ya Kilimo na Mali Asili ambayo yanahitaji marekebisho ya kiufundi ili yawahi kurejea kutoa huduma za kilimo mashambani Unguja na Pemba.
Mkuu huyo wa Kitengo cha Ufundi Kiwanda cha Matrekta Mbweni alifahamisha kwamba Kitengo hicho hivi sasa kinaendelea na mpango wa kushirikiana na Kampuni ya ufundi ya Mahindra ya Nchini India kwa lengo la kujiimarisha kiufundi ili kiendelee kutoa huduma za Kimataifa.
Mhandisi Moh’d alifafanua kuwa wataalamu wa Kiwanda hicho wako katika hatua ya kukamilisha mapendekezo yatayopelekwa kwenye Uongozi wa Kampuni hiyo ya Mahindra kwa hatua zaidi.
Alieleza kwamba Mpango huo wa maombi umeainisha pia namna Kiwanda hicho kinavyotaka kujiimarisha zaidi katika utoaji wa mafunzo ya ufundi ngazi ya cheti kwa vijana wanaoamua kuchukuwa fani hiyo.
“ Tunaendelea kufundisha vijana wetu wanaomaliza masomo yao ya sekondari kwa vile tayari tumeshapata idhini ya Nacte na tunafarajika zaidi kwa vile masomo ya vijana hao huambatana na mazoezi ya vitendo hapa hapa Kiwandani “. Alisema Mhandisi Moh’d.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwapongeza watendaji wa Kiwanda cha Matrekta Mbweni kwa juhudi wanazoendelea kuchukuwa katika utekelezaji wa majukumu yao licha ya changamoto zinazowakabili kila siku.
Balozi Seif alielezea faraja yake kutokana kwamba vifaa na mashine nyingi zilizopo Kiwandani hapo bado zinaendelea kutumika tokea kuanzishwa kwa Kiwanda hicho mwaka 1967.
“ Kazi mnazozifanya mnastahiki kupongezwa hasa ikizingatiwa kwamba mashine zenu ni zile zile mnazozitumia za mwaka 1967 “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliufahamisha Uongozi wa Kiwanda hicho pamoja na watendaji wake kwamba Serikali Kuu itaangalia namna itakavyoweza kusaidia kukwamua changamoto zinazokikabili Kiwanda hicho.
No comments:
Post a Comment