TANGAZO


Sunday, December 28, 2014

Nyalandu kufanya Tamasha kubwa Kumshukuru Mungu kutimiza miaka 15 ya Ubunge wake

*Zaidi ya watu 20,000 kuhudhuria

Na Mwandishi Wetu 
Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, Desemba 28, 2014 (kesho J’pili) atafanya mkutano mkubwa kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu na wananchi wa Singida Vijijini na Watanzania wote kwa kutimiza miaka 15 ya ubunge.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Mbunge huyo, Elia Diga, imesema kuwa mkutano huo ambao utaambatana na burudani mbalimbali, utafanyika katika Kata ya Ilongero na utahudhuriwa na viongozi wa Chama na serikali, viongozi wa dini zote na wananchi zaidi ya 20,000 kutoka kata zote zinazounda jimbo hilo na zile za jirani.

Katika mkutano huo, Nyalandu atahutubia wananchi pamoja na kueleza mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi chote cha miaka 15.

Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana mpaka sasa, Nyalandu pia ataeleza wananchi mwelekeo mpya wa jimbo hilo na mahali anapopenda lifike.

Viongozi wote wa CCM Wilaya ya Singida wakiongozwa na mwenyekiti wake, watahudhuria mkutano huo na kutoa hotuba fupi kwa wananchi.

Wasanii nyota wanaotamba nchini wakiongozwa na kundi la Makomandoo, Rose Muhando, Christina Shusho, H-Baba, Mchekeshaji Steve Nyerere na Bendi ya New Life Bandi watakuwepo kukonga nyoyo.

Pia kutakuwepo na vikundi  mbalimbali vya ngoma za asili vikiwemo Njagmba, Ilongero Group na vingine vingi vitakuwepo kutoa burudani.

No comments:

Post a Comment