Baadi ya waandishi wa
habari wakimsikiliza Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu na Makazi
wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraimu Kwesigabo leo jijini Dar es Salaam
alipokuwa akizungumzia suala la mfumuko wa bei nchini. (Picha zote na Eleuteri
Mangi-MAELEZO)
WANANANCHI wameombwa
kutoa ushirikiano wa dhati kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kupitia ofisi za
takwimu za mikoa wakati wa ukusanyaji wa takwimu mbalimbali kwa lengo la kutoa
taarifa zilizo sahihi kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa Mkurugenzi
wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu na Makazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw.
Ephraimu Kwesigabo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar
es salaam.
Kwesigabo amesema kuwa pamoja
na mambo mengine Ofisi ya Taifa ya Takwimu ndiyo yenye mamlaka ya kutoa taarifa
za mfumuko wa bei nchini ambapo kwa mwaka huu unaonesha umepungua kwa baadhi ya
bidhaa za vyakula kuanzia kipindi cha mwezi Oktoba 2013 hadi Oktoba 2014.
Kwesigabo amesema kuwa mwenendo
wa bei za bidhaa za vyakula zilizoonesha kupungua bei kwa mwezi Oktoba 2014
zikilinganishwa na mwezi Oktoba 2013 ni pamoja na bei za mahindi asilimia 7.2,
unga wa mahindi asilimia 5.5 na unga wa ngano asilimia 4.4.
Bidhaa nyingine za
vyakula zilizoonesha kupungua bei ni ulezi asilimia 3.5, tambi asilimia 2.2,
samaki asilimia 4.6, mihogo asilimia 2.1 na sukari imepungua kwa asilimia 4.6.
Aidha, Kwesigabo
amesema kuwa mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Oktoba 2014 umepungua hadi
asilimia 5.9 kutoka asilimia 6.6 tofauti na hali ilivyokuwa mwezi Septemba
2014.
"Hii inamaanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei
za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Oktoba 2014 imepungua ikilinganishwa na
kasi iliyokuwepo mwaka ulioishia mwezi Septemba 2014” alisema Kwesigabo.
Kwa upande wa mfumuko
wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi Bw. Kwesigabo amesema kuwa umepungua kwa
asilimia 0.2 ikilinganishwa na kupungua kwa asilimia 0.4 kama ilivyokuwa kwa
mwezi Septemba mwaka huu, huku fahirisi za bei za taifa zimepungua hadi kufikia
149.70 kwa mwezi Oktoba 2014 kutoka 149.93 za mwezi Septemba 2014.
Kwesigabo amezitaja
bidhaa zilizochangia ongezeko la fahirisi za bei nchini kuwa ni pamoja na vitafunwa
vinavyotokana na unga wa nagano kwa asilimia 2.4, unga wa mahindi kwa asilimia
0.1, samaki kwa asilimia 1.7,ndizi za kupika kwa asilimia 7.5, mbogamboga kwa
asilimia 2.2, viazi mviringo kwa asilimia 1.5 na sukari kwa asilimia 1.6.
Aidha, amesema uwezo wa
shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za jamii umefikia
shilingi 66 na senti 80 kwa mwezo Oktoba 2014 kutoka mwezi Septemba 2010
Kuhusu ulinganifu
mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki amesema kuwa
una mwelekeo unaofanana na kueleza kuwa mfumuko wa bei nchini Kenya umepungua
hadi kufikia asilimia 6.43 kwa mwezi Oktoba 2014 ikilinganishwa na asilimia
6.60 za mwezi Septemba mwaka huu, huku Uganda ikiwa na mfumuko wa bei
umeongezeka hadi asilimia 1.8 kwa mwezi Oktoba mwaka huu ikilinganishwa na 1.4
za mwezi Septemba.
No comments:
Post a Comment