TANGAZO


Sunday, November 9, 2014

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais Dk. Ali Mohamed Shein awahutubia wananchi wa Kisiwani Pemba


Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza na wananchi na Wana-CCM wa Mikoa ya Pemba, Uwanja wa Gombani ya Kale, Kisiwani Pemba leo. (Picha zote na Ikulu)

Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein akiionesha Katiba Inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba wakati alipokuwa akizungumza na wananchi na wanaCCM wa Mikoa ya Pemba, Uwanja wa Gombani ya Kale, Kisiwani Pemba leo.

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar


RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa yeye haendeshi nchi kimabavu bali anafuata Sheria na Katiba ya nchi huku akisisitiza kuwa CCM itashinda mwaka 2015.



Hayo aliyasema leo katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Gombani ya Kale, Chake Chake Pemba ambapo madhumuni makubwa ya mkutano huo ni kupongezana kwa kutimiza miaka minne tangu CCM kuongoza pamoja na kufafanua juu ya Katiba mpya inayopendekezwa.



Dk. Shein alisema kuwa anashangazwa na viongozi wa CUF wanaosema anaongoza nchi kimabavu na kueleza kuwa wanasema hivyo kwa sababu ya kutokana na kutokuwa tayari kuyafuata wanayoyataka ambayo yako kinyume na sheria na taratibu za nchi zilizopo.

Kutokana na mafanikio makbwa yaliopatikana katika uongozi wa CCM ikiwa ni miongoni mwa kutekeleza Ilani ya CCM aliwataka WanaCCM kuamini kuwa mwaka 2015 CCM itashinda kwa kishindo na hilo walijue na kutembea kifua mbele kulieleza.



Alisema kuwa ndani ya miaka minne mafanikio makubwa yamepatikana na kuwakakikishia wananaCCM kuwa CCM itashinda mwaka 2015 kwani njia nyeupe na kuwa mwisho wa CUF.

Kwanza hawana rekodi wala historia na namna ya kufika Ikulu kwani Ikulu imeanza na ASP na hivi sasa niCCM. "hatutaki kuandikia mate wino upo, wembe ni ule ule",alisema Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein.



"...uchaguzi wa mwaka 2015 utakuwa huru na wa demokrasi na utakuwa wa amani na utulivu na utakuwa wa wazi na uchaguzi huo ndio tutakaohakikisha tunaizika CUF, ili tuendelee kuoingoza Zanzibar na kuhakikisha CUF haiingii Ikulu"alisema Dk. DShein.



Sambamba na hilo alitumia fursa ya kumpongeza Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuongoza nchi na kuhakikisha katiba iliyopendekezwa inapatikana.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa CCM wakiwemo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Idd, pamoja na WanaCCM na wananchi  kutoka maeneo mbali mbali ya kisiwa cha Pemba.

Alieleza kuwa Kongamano lililofanyika kisiwani Unguja pia, litafanyika kiwani Pemba na kueleza kuhusu zao la karafuu  kupitia Shirika la Biashara la ZSTC limepata mafanikio na kusisitiza kuwa zao la hilo halitobinafsishwa.



Aidha, alieleza kuwa Serikali ilifanya juhudi za makususdi katika kupiga vita suala la magendo na kuwapongeza wananchi wa Pemba kwa kushirikiana na Serikali  katika kupambana na magendo na kueleza juhudi za Serikali za kupandisha bei za karafuu.

Pamoja na hayo, alieleza kuwa uamuzi wa kuliimarisha zao la karafuu umefanaywa kwa makusudi katika kuhakikisha Ilani ya CCM inatekelezwa kwa vitendo.

Dk. Shein alichukua fursa hiyo kuwapongeza waliokuwa Wajumbe wa Bunge hilo la Katiba ambao walitoa ufafanuzi kwa Wananchi na WanaCCM waliohudhuria katika mkutano huo.



Alisisitiza kuwa tarehe 30, April mwakani ndio siku ya kupiga kura na kueleza kuwa anaamini Wazanzibari wote wataipigia kura ya ndio Katiba hiyo huku akieleza kuwa wale wote waliotoka katika Bunge la Katiba hawakutumia demokrasia wala hawakuwatendea haki wananchi.



Dk. Shein pia alimpongeza aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba Mhe. Samuel Sita, Makamo wake Mhe.Samia Suluhu pamoja na Wajumbe wengine wote walioshiriki kikamilifu katika kutoa  Katiba hiyo mpya.

Alisema kuwa kwa wale wote wanaotaka mamlaka kamili, jambo hilo katika Katiba hiyo hamna, na badala yake katika Katiba hiyo mna serikali mbili na kueleza kushangaa na kudaiwa mamlaka kamili ya Zanzibar.

Alisema kuwa baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 Zanzibar ilipata Jamhuri yake ambapo hadi Umoja wa Mataifa ikajulikana na hata Tanganyika ikapata Uhuru wake mwaka 1961 na  kupata mamlaka kamili na ndipo marehemu mzee Karume na marehemu Mwalimu Nyerere  wakaunganisha nchi na ndio ikaundwa Tanzania.

Dk. Shein alisisitiza kuwa kwa mujibu wa hati ya Muungano itakuwepo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye Mamlaka yake Kamili na kueleza kuwa serikali hiyo itaendelea kuwepo kwani ina mamalaka yake yote Tatu, Baraza la Wawakilishi, Baraza la Mapinduzi na Mahakama pamoja na  alama zake zote.



"unaposema unataka mamlaka kamili ndani ya serikali mbili kikatiba na kisheria ni kukataa Muungano,  hivyo  kwa hili waelewe kuwa Muungano uliopo hauvunjiki hata siku moja"laisema Dk. Shein.

Alisema kuwa CCM isisingiziwe kama imeunda Katiba peke yake bali ni vizuri ijulikane kuwa CCM imetoa maoni kama ilivyotakiwa kwani ndani ya Bunge hilo pia walikuwepo Wajumbe wengine 201 ambao nao waliiunga mkono katika hiyo.



Dk. Shein alisema kuwa  katika Katiba hiyo Kero zote za Muungano zimetatuliwa ni kwa ajili ya hatima ya Tanzania na hatima ya Zanzibar pamoja na watu wake.



Alisema kuwa Wajumbe na Wabunge waliowachagua kisiwani Pemba hawakuwatendea haki wananchi waliowachagua hiyo ni kutokana na kutoka katika Bunge la Katiba ambapo wangewatetea wananchi hao.

Alisema kuwa hatua kubwa sana imepatikana katika sekta ya elimu, na kusema kuwa hivi sasa Zanzibar ina vyuo vikuu vitatu na Tawi la SUZA linaandaliwa huko Mchangamdogo kisiwani Pemba.

Alisema kuwa kabda ya Mapinduzi waliopata Shahada ya kwanza hawakuzidi 5 hadi ambapo hivi sasa  Zanzibar ina vyuo Vikuu vitatu ambapo hadi Januari  mwaka huu jumla ya wanafunzi  4485 waliokuwepo katika vyuo vikuu  ambavyo ni SUZA, Tunguu na Chukwani.

Alisema kuwa tayari Serikali imeadaa mfuko maalum kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kuweza kujiajiri wenyewe na kusisitiza kuwa anapata tabu sana kwa wale viongozi vigeugeu ambao wamo katika serikali anayoionhoza ambao wanasema kuwa wananchi hawaajiriwi.

Nayo risala ya WanaCCM  wa kisiwa cha Pemba ilitoa pongezi kwa mafanikio makubwa yaliopatikana kisiwani humo ndani ya miaka minne ya uongozi wa Dk. Shein sambamba na kusimamia vyema Ilani ya chama hicho na kueleza mafanikio ya kufikisha umeme kisiwa cha Makongwe na kisiwa Panza vyote vya huko Pemba.

Risala hiyo ilieleza mafanikio makubwa yaliopatikana kisiwani humo ikiwa ni pamoja na maendeleo makubwa yaliopatikana hasa katika uimarishaji wa barabara za Kaskazini na Kusini mwa kisiwa hicho ambazo zimeimarika na kuweza kuziunganisha sehemu hizo kwa barabara za lami.

Aidha, risala ilieleza mafanikio yaliopatikana kisiwani humo katika sekta ya afya, elimu, biashara na kuongezwa kwa bei ya karafuu ambayo imewasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wa Pemba na kuwainua kimaisha na kiuchumi. "Wewe Dk. Shein ndio mwenye mamlaka ya kutangaza bei ya karafuu na sio mwengine" alisema Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba Abdalla Mshindo. 

Pia, risala hiyo ilieleza na kupongeza juhudi kubwa za Dk. Shein katika kusimamia amani na utulivu huku ikieleza kutotishwa na maneno ya upinzani ambao wamejiunga na kujiita UKAWA na kusisitiza kuwa WanaCCM wa kisiwa hicho hawaiogopi wala hawatishwi na UKAWA na kuahidi kuipigia kura ya ndio Katiba hiyo wakati ukifika.

Nae Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 Mzee Hamid Ameir aliwataka WanaCCM kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ya maoni itakapofika na kutoa salamu za wazee wenzake wa Unguja kwa wanaCCM wa Pemba.



Katika Mkutano huo viongozi mbali mbali ambao ni miongoni mwa  waliokuwa Wajumbe wa  Bunge la Katiba walitoa maelezo kadhaa sambamba na elimu juu ya Katiba inayopendekezwa na kuelezea Ibara kadhaa za Katiba hiyo huku wakisisitiza kupigiwa kura ya ndio Katiba iliyopendekezwa wakati utakapofika.



Naye aliyekuwa Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Asha Bakari alisisitiza haja ya kupelekwa hoja binafsi ya kukataa Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika Baraza la Wawakilishi kwani tayari CUF wameshajiunga na UKAWA.

"Wanasema tumeufyata, sasa nauliza aliyeufyata nani..sisi au wao...vyako vyako na wenzako vikikupata vyako peke yako... ndugu zangu hamjachoka kudanganywa" alisema  Asha Bakari huku akisema na kuwapongeza akina baba waliokuwemo kwenye Bunge la Katiba kwa kukubali hamsini kwa hamsini.



Aidha, Wajumbe hao walieleza kuwa CUF hawakuwatendea haki Wazanzibari kwa kukimbia katika Bunge la Katiba ' Mtu mkifukuzana na ukimpita na akiaza kukwambia tutaonana wewe ujue kashindwa"laisema Ramadhan Abdalla Shaaban Waziri wa Maji, Nishati, na Ardhi.

Nae Balozi Seif  Ali Idd alisema kuwa Wajumbe wa CCM wa Bunge la Katiba lililopita wamemtetea Rais wa Zanzibar ambapo Katiba hiyo inaonesha wazi hivi sasa kuwa Rais wa Zanzibar atakuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kuwa Katiba hiyo  inatoa fursa kwa Zanzibar kuchimba mafuta yake wenyewe sambamba na kutengeza Sera yake wenyewe na kuwataka WanaCCM wasikubali kudanganywa. "Dk. Shein hawezi kuutetea ugaidi".

Balozi Seif alisisitiza kuwa Dk. Shein hatokuwa tayari kuwatetea waliokamatwa na kutuhumiwa katika sakata la ugaidi na ndio maana viongozi wa CUF wanasema kuwa  yeye na Dk. Shein wanaongoza kimabavu na kutoa mfano kwa kijana wa kizanzibari aliyehusika na mripuko katika ubalozi wa Marekani na kwenda kuhukumiwa nchini humo "Mbona huyu hawasemi kwa nini kenda hukumiwa Marekani"aliuliza Balozi Seif.

No comments:

Post a Comment