TANGAZO


Sunday, October 12, 2014

WILAYA YA SAME NA MWANGA ZAPATA KIASI CHA SHILINGI BILIONI 56.10 KUTOKA MFUKO WA MAENDELEO YA UCHUMI WA KUWAIT

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa serikali  Dr. Servacius Likwelile akiwa na ujumbe kutoka mfuko wa maendeleo ya uchumi wa Kuwait wakisubiri kutiliana saini mkataba wa  makubaliano ya kuanzisha mradi wa maji katika Wilaya ya Same na Mwanga. Aliye kulia  kwake ni Bw. Abdulwahab A. Al- Bader  ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dr. Servacius Likwelile akitia saini makubaliano ya mradi wa maji katika Wilaya ya Same na Mwanga. Aliye kulia kwake Bw. Abdulwahab A. Al- Bader  ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa maendeleo ya uchumi wa Kuwait. Waliosimama nyuma ni  Bi. Suzan Mkapa, Mkurugenzi wa sheria kutoka Wizara ya Fedha na wengine ni wataalam kutoka Kuwait.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dr. Servacius Likwelile na  Bw. Abdulwahab A. Al- Bader  ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa maendeleo ya uchumi wa Kuwait wakibadilishana mikataba hiyo baada ya kutiliana saini.
Wajumbe kutoka Tanzania na Kuwait wakishangilia kwa furaha baada kusainiwa kwa mkataba wa kuanzisha mradi wa maji katika Wilaya ya Same na Mwanga. (Picha zote na Ingiahedi Mduma-Wizara ya Fedha  tukiwa Washington DC)
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa serikali  Dr. Servacius Likwelile, mchana wa leo ametiliana saini makubaliano ya mkataba wa kuanzisha Mradi wa Maji katika Wilaya ya Same na Mwanga. 
Dr. Likwelile alisaini Mkataba huo kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mfuko wa maendeleo ya uchumi wa Kuwait . Aliye wakilisha Mfuko huo ni Bw. Abdulwahab A. Al- Bader  ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko.

Aidha katika kutiliana saini Mkataba huo Dr. Likwelile alimueleza Bw. Abdulwahab A. Al- Bader kuwa, Serikali ya Tanzania inatambua kuwa mfuko umetoa Dola za Kimarekani milioni 34.0 sawa na shilingi Bilioni 56.10 za Kitanzania kwa ajili ya kusaidia mradi wa maji katika Wilaya ya Same na Mwanga. Hivyo inatoa shukrani zake za dhati kwa nchi ya Kuwait na hasa kwa mfuko huu wa maendeleo ya kiuchumi.

“Msaada huu tulioupata leo utaisaidia Serikali kutatua tatizo la maji katika wilaya ya Same na Mwanga, hii inaonyesha  ni jinsi gani mfuko huu wa Kuwait unavounga mkono na kutekeleza jukumu zima la kushiriki katika masuala ya kijamii na ya kiuchumi kwa nchi yetu ya Tanzania, hivyo tunaomba muendelee kutusaidia”. Alisema Dr. Likwelile.

Dr. Likwelile alimueleza Bw. Abdulwahab A. Al- Bader kuwa, kama anavyofahamu  gharama za mapendekezo ya mradi mzima ni Dola za Kimarekani  million 110.43 na hii inahitaji uchangiaji kutoka katika mifuko mingine kama BADEA, mfuko wa maendeleo wa Saudia , Mfuko wa Kimataifa wa OPEC  na Serikali kuchangia fedha kusaidia mradi huu. 

"Kwa hili sina wasiwasi nalo kwani ninafuraha kujua kwamba umeshakubaliana na ninaujasiri kuwa jitihada zako zitafanikiwa." Alisema. 

“Mradi huu wa  maji wq wilaya ya Same na Mwanga unalenga kusaidia kuwepo kwa maji kwenye jamii mbalimbali zilizopo kwenye mradi huo.” Aliongeza Dr.Likwelile.
Aliendelea kusema kuwa,mradi huo utakapo kamilika :
(i)                 utaongeza kiwango cha watu wengi kuweza kupata maji safi na salama ya  kunywa.
(ii)               Uchumi wa Same na Mwanga utaimarika pamoja na hali ya afya kwa jamii nayo itakuwa imara hasa kwa maeneo yale yanayoguswa na mradi.
(iii)              Hali ya maisha ya watu wa Same na Mwanga itainuka.
“Mafanikio ya ukamilishaji wa mradi huu ni muhimu sana kwa uchumi wa jamii na maisha bora kwa watu wa wilaya ya Same na Mwanga”. Alisema Likwelile.

Dr. Likwelilie alimalizia kwa kusema kuwa“Tanzania na Kuwait ni marafiki wa muda mrefu sana, hivyo tutazidi kushirikiana na kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa”.
Hali ya hewa ya mjini Washington Dc. ni mvua za vipindi na baridi kiasi.
Imetolewa na:
Ingiahedi Mduma
Msemaji
Wizara ya Fedha
Washington D.C

11/10/2014

No comments:

Post a Comment