TANGAZO


Sunday, October 12, 2014

Maalim Seif Shariff Hamad aipinga Katiba Inayopendekezwa

Maalim Seif Shariff Hamad

Na Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
KATIBU mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amesema kitendo cha bunge maalum la katiba kupuuza maoni ya wananchi yaliyotolewa kupitia rasimu ya tume ya mabadiliko ya katiba ni kuikandamiza Zanzibar na wananchi wake.
Akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama hicho katika viwanja vya Demokrasia, Kibanda Maiti mjini Zanzibar, maalim Seif alisema kufanya hivyo ni uharamia unaofaa kulaaniwa na kwamba chama chake kitaipinga katiba hiyo wakati wa kura ya maoni.
Alisema kuwa rasimu ya Jaji Warioba iliyowasilishwa katika bunge maalum la katiba ilitoa nafasi ya Zanzibar kujitawala na kujiamulia mambo yake kwa mfumo wa muungano wa serikali tatu na  kupunguza idadi ya mambo ya muungano kutoka 22 hadi 7 jamboambalo limekiukwa na katiba inayopendekezwa iliyokadhiwa kwa marais Dkt. Jakaya Kikwete na Dkt. Ali Mohammed Sheni.

“Kupunguzwa kwa Mambo ya muungano kutoka 22 hadi 7 katika rasimu ya Warioba ulikuwa ni uamuzi wa kuivua Tanganyika koti la Muungano, jambo ambalo limerudishwa katika katiba iliyopendekezwa na huu ni ujanja wa dhahiri wa kutaka kupora hadhi na mamlaka ya Zanzibar, jambo ambalo tutalipinga kwa nguvu zetu zote”, alisema Maalim Seif.

Akizungumzia kauli za baadhi ya viongozi wa Serikali ya Zanzibar, kuwa serikali inakubaliana na katiba iliyopendekezwa na kwamba katiba hiyo inaipa fursa zaidi ya kujiendeshea mambo yake, Maalim Seif alisema hizo ni kauli za watu binafsi kwa kuwa hakuna kikao chochote cha Baraza la Mapinduzi, kilichofanyika kuijadili rasimu hiyo.
Aliongeza kuwa bunge hilo, kuongeza sura inayohusu mambo ya ardhi na kutoa uwezo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kuigawa Zanzibar katika Mikoa, wakati likijua ardhi sio miongoni mwa mambo ya Muungano ni ukiukwaji wa matakwa ya katiba ya Zanzibar, jambo ambalo linaweza kuwa chanzo cha mgogoro kati pande hizo za Muungano.
"Wanatufanya kama sisi ni watoto wadogo na wanatumia Muungano kama kichaka cha kuinyonya na kuiminya wakati wakijua dhahiri kuwa jambo hilo, ni kuipunguzia hadhi na mamlaka ya Zanzibar, kuijiamulia mambo yake, jambo ambalo halikubaliki”, alisema Maalim seif na kuahidi kushirikiana na wadau wengine kulipinga jambo hilo.

Aidha aliwataka marais jakaya kikwete na ali mohammed sheni kulinda heshima zao kwa kusikiliza matakwa ya wazanzibar na watanzania  waliyoyatoa kupitia rasimu ya jaji warioba kwa juwa kinyume chake ni kuikwamisha rasimu ya change katika kura ya maoni wakati utakapofika.

“Tunamwambia Rais Kikwete na Dkt. Sheni wasikubali kuingizwa mkenge na kina Chenge (Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Katiba) na Sitta (Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba) na wenzao kwani katiba hii waliyopendekeza haitopita kwa kuwa haina uhalali kwa kuwa imekosa sifa muhimu”, alisema Maalim.

Aliongeza kuwa anashangazwa na kauli ya Rais Kikwete kuwa watu wanaikosoa katiba iliyopendekezwa na kuhoji katiba bora ni ipi, Maalim alisema katiba hiyo, haina ubora kwa kuwa imekosa maridhiano na imepuuza maoni ya wananchi.

“Watu wanaipinga na hawaikubali katiba hii kwa kuwa haikuzingatia maoni ya wananchi, kutopatikana kwa maridhiano miongoni mwa Wabunge na wabunge wa upande mmoja kuamua kuchukua mamlaka ya kujiundia katiba inayokidhi matakwa ya chama chao, inakuwaje na ubora anaousema rais Kikwete?”, Alihoji Maalim Seif.
Akizungumzia suala la Wazanzibar wanaotuhumiwa kufanya makosa ya ugaidi kupelekwa Tanzania Bara na kushitakiwa, alisema jambo hilo ni kinyume cha Sheria kwa kuwa sheria za Tanzania zinaruhusu mtu aliyefanya kosa kuweza kushtakiwa katika eneo alilofanyia makosa hayo na hata kama kuna haja ya kupelekwa mahali pengine ni lazima taratibu zifuatwe na kwamba warudishwe ili washtakiwe kama wana makosa.

Alisema kufanyika hivyo, bila ya kuzingatiwa matakwa ya sheria ni dharau kwa Zanzibar kwa kuwa mfumo wa Sheria na Mahakama za Zanzibar zina uwezo wa kushughulikia masuali hayo na kwamba hayajawahi kutokea katika Awamu Tano za Serikali ya Zanzibar, isipokuwa katika awamu ya sita, ya Dkt. Amani Karume.

Alisema suali hilo, lilitokea kwa wazee walioandika barua ya kudai nchi ya Zanzibar katika Umoja wa Mataifa na kupelekwa Tanzania Bara kushtakiwa kabla ya Rais huyo, kutoa amri watu hao warudishwe baada ya kuwahoji aliyekuwa Waziri Kiongozi wa wakati huo, Shamsi Nahodha na Mkurugenzi wa Mashtaka wa wakati huo, Othman Masoud, ambaye wiki iliyopita alifutwa kazi na Rais wa Zanzibar.
Mapema aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki kabla ya kufukuzwa uanachama katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mansour Yussuf Himid, aliwataka viongozi wa kisiasa kuwa na mapenzi na watu wanaowaongoza kwa kusimamia matakwa yao kwa kuwa watu hao, wana matumaini makubwa juu yao.

“Lazima viongozi wa kisiasa muwe na huruma na umma kama huu kwani una matarajio makubwa na mnapowapuuza hakuna jambo jengine linalowastahikia zaidi ya laana toka kwa watu hawa na Mwenyezi Mungu aliyewatuma”, alisema Mansour na kuwataka wananchi wawe watulivu na kuwasikiliza viongozi wao.

Naye mwanasiasa mkongwe wa Zanzibar ambaye ni miongoni mwa waasisi wa Muungano, Hassan Nassor Moyo, alisema kuwa ataendelea kuupinga mfumo wa serikali mbili uliopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba wakati wowote kwa kuwa mfumo huo, hauna maslahi kwa Zanzibar na watu wake zaidi ya kuunufaisha upande wa pili wa Muungano na ndio maana upande huo hawataki kuachana nao.
“Mimi naujua zaidi Muungano huu, na siwezi kuacha kuupinga kwa kuwa hauna maslahi na unaikandamiza Zanzibar, suluhu inakuja baadhi ya watu kutokana na kuwa na manufaa nao wanapuuza na kufanya wanavyotaka, hatukubali”, alisema Mzee Moyo.

No comments:

Post a Comment