TANGAZO


Thursday, October 2, 2014

Rais Kikwete kuwa Mgeni rasmi katika Kikao cha kazi cha Usimamizi na Uendeshaji wa Elimu Msingi

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, Ndg. Jumanne A. Sagini akizungumza katika kikao kazi cha Usimamizi na Uendeshaji wa Elimu Msingi kinachofanyika katika ukumbi wa Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma kuanzia tarehe 01-03 Oktoba, 2014
Baadhi ya Washiriki wa Kikao cha Kazi cha Usimamizi na Uendeshaji wa Elimu Msingi kinachofanyika  katika ukumbi wa Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma kuanzia tarehe 01-03 Oktoba, 2014.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI Mhe. Hawa A. Ghasia akiwakaribisha wajumbe wa Kikao kazi cha Usimamizi na Uendeshaji wa Elimu Msingi kinachofanyika  katika ukumbi wa Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma kuanzia tarehe 01-03 Oktoba, 2014. Lengo la kikao hicho ni kuainisha Mafanikio na Changamoto katika utekelezaji wa Matokeo Makubwa Sasa katika Sekta ya Elimu.
Na Mwandishi wetu
OFISI ya Waziri Mkuu – TAMISEMI  kwa kushirikiana na Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo wameandaa kikao cha kazi kuhusu Usimamizi na Uendeshaji wa Elimu Msingi kwa Viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri kinachofanyika katika ukumbi wa Chimwaga uliopo Chuo Kikuu cha Dodoma.
Kikao hicho cha siku tatu kinafanyika kuanzia tarehe 01 hadi 03 Oktoba, 2014. Kikao hicho kinalenga katika kuainisha mafanikio na chanagamoto  katika utekelezaji wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya Elimu.
Mgeni Rasmi katika kikao hicho anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.
Mada zitakazowasilishwa katika kikao hicho ni pamoja na Wajibu na Majukumu ya Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI), Pendekezo la kukibadili Chuo Kikuu Huria cha Taifa cha Tanzania na mada juu Utekelezaji wa Mawasiliano Vijijini, Ujenzi wa Mikongo ya Mijini na Watumiaji wa Mwisho pamoja na kuunganisha Shule na Taasisi za Umma katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Mada nyingine ni utaratibu wa kushughulikia malalamiko ya wananchi na watumishi wa Umma, Miongozo ya ujenzi:  mafanikio na changamoto za ujenzi wa shule pamoja na mada kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF).
Aidha, katika kikao hiki kila mkoa utapata nafasi ya kutoa taarifa ya namna zilivyotekeleza  dhana ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika Sekta ya Elimu nchini.
Kikao hiki kimehusisha Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya Wakurugenzi wa  Halmashauri, Maafisa Elimu Mikoa na Wilaya  pamoja na Watendaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI  na Wizara ya elimu na Mafunzo ya Ufundi.

No comments:

Post a Comment